Dk Biteko atoa maagizo sekta ya mafuta na gesi akitaka ufanisi

Muktasari:
- Naibu waziri huyo amesema hatavumilia kuona wawekezaji wakisumbuliwa na kuwekewa urasimu usiokuwa na maana.
Dodoma. Naibu Waziri Mkuu, Dk Doto Biteko ametoa maagizo matano kwa Shirika la Maendeleo la Petroli Tanzania (TPDC) kubwa akisisitiza masuala ambayo yataongeza ufanisi wa sekta hiyo.
Dk Biteko ametoa maagizo hayo leo Jumatano Aprili 30, 2025 wakati akizindua mpango mkakati wa muda mrefu wa Shirika la Maendeleo la Petroli wa mwaka 2025-2030.
Maagizo mengine aliyoyatoa Dk Biteko Kwa TPDC ni kuharakisha kukamilisha mchakato wa vitalu vya gesi, kuondoa urasimu kwa wawekezaji, kushirikisha sekta binafsi katika mpango mzima na kuimarisha mifumo ya usambazaji wa gesi.

Naibu Waziri Mkuu amesema hatavumilia kuona mambo hayo yakijitokeza badala yake anatamani kuona Watanzania wakipata neema kupitia mpango huo.
"Wakati fulani mnatengeneza urasimu mwingi kwa wawekezaji ambao hata haustahili ilimradi ninyi mmeona inafaa hivyo, hatuwezi kufika na nikiona hilo usishangae nakuja kwako bila hodi," amesema Dk Biteko.

Kiongozi huyo amesema katika kipindi hiki Watanzania wameamka kwani wanahitaji huduma ya gesi kuliko wakati mwingine na unafika muda hata Serikali inajiuliza ianze kutoa huduma kwa yupi na kumwacha yupi.
Kwa upande wa watumishi ametaka wafanye tathimini ya mpango wa awali wa 2018- 2024 kwa nini ulifeli ili yasiyetokea katika Mpango wa muda mrefu.
Amewataka watumishi hao kujiimarisha katika mpango wa gesi ili kupunguza uagizaji wa mafuta nje ya nchi.
Hata hivyo amesisitiza huduma bora kwa wananchi wa Songosongo ambako ndiko chanzo cha gesi lakini wananchi wake bado hawajanufaika kama inavyopaswa.

Mwenyekiti wa Bodi ya TPDC Katibu Mkuu Kiongozi Mstaafu Balozi Ombeni Sefue amesema mpango wa kuwa na rasilimali ni hatua moja lakini kuanza kuitumia ni hatua nyingine kwani kuna wakati wanalazimika kuchelewa kuanza kutoa huduma ili wakamilishe baadhi ya mambo.
Balozi Sefue amesema suala la umakini ndilo linasababisha uchelewaji wakati mwingine kwani lazima majadiliano yawe ya kujiridhisha kwa pande zote.

Hata hivyo amesema ndoto yao ni kuona TPDC inakuwa kampuni kubwa ya mafuta kimataifa ambayo itatoa ushindani na huduma nzuri kwa wananchi.
Waziri wa Maji na Nishati wa Zanzibar, Hassan Shaibu Kadwale amesema licha ya Taasisi hiyo kutokuwa ya Muungano lakini anatumaini kuwa safari ya mafanikio kwa Tanzania ndiyo inaanzia hapo.