Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Wabunge waibua hoja tano bajeti Dk Biteko

Muktasari:

  • Wabunge wameendelea kuchangia makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara ya Nishati kwa mwaka 2025/26, huku wakiibua mambo matano.

Dodoma. Mambo matano yamejitokeza wakati wabunge wakijadili makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara ya Nishati kwa mwaka 2025/26, miongoni mwao ni pamoja na suala la kukatika mara kwa mara kwa umeme.

Mambo mengine ni fidia kwa wanaopisha miradi ya umeme, mitungi ya gesi kutupwa baada ya kutumika, fedha za CSR za bwawa la Mwalimu Nyerere (JNHPP) pamoja na vituo vya mafuta kujengwa kiholela.

Wabunge wamesema hayo leo Jumanne Aprili 29, 2025, wakati wakichangia makadirio hayo yaliyowasilishwa na Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk Doto Biteko bungeni jana.

Dk Biteko ameliomba Bunge kumuidhinishia Sh2.24 trilioni, na kati ya fedha hizo Sh2.16 trilioni sawa na asilimia 96.5 ya bajeti yote ya wizara na taasisi zake ni kwa ajili ya miradi ya maendeleo.

Akichangia mjadala huo, Mbunge wa Kiteto (CCM), Edward Ole Lekaita amesema Kiteto mkoani Manyara umekuwa na shida ya kukatika kwa umeme.

Mbunge wa Kiteto(CCM), Edward Ole Lekaita akichangia mjadala wa makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara ya Nishati kwa mwaka wa fedha 2025 / 2026 yanayotarajiwa kupitishwa leo bungeni jijini Dodoma. Picha na Hamis Mniha

“Siyo kukatika tu, ni kukatika kwa muda mrefu kunakowaunguzia wananchi vifaa vyao. Ilileta kero kubwa. Niliwahi kumwambia Naibu Waziri (Judith Kapinga – Naibu Waziri wa Nishati) na Mkurugenzi wa REA (Wakala wa Umeme Vijijini) kuelezea hili jambo,” amesema.

Amesema anafahamu kazi iliyokuwa ikiendelea ya kurekebisha mifumo ya zamani, lakini shida nyingine ni kwamba Kiteto wanapata umeme kutoka kwenye laini moja kutoka Dodoma, na kwamba wakati mwingine mji mzima wa Kiteto hauna umeme.

Ole Lekaita amesema kama wakijenga kituo (switching station) jirani na wakawa na laini nyingi kwenda Kiteto, itasaidia katika kukabiliana na changamoto hiyo, ameongeza kuwa gharama yake ni Sh3 bilioni.

Naye Mbunge wa Nkenge (CCM), Florent Kyombo amesema, ingawa wabunge wengine wamelalamikia suala la umeme kukatika mara kwa mara, Wilaya ya Misenyi, mkoani Kagera hukumbwa na tatizo hilo zaidi kutokana na mvua nyingi.

Mbunge wa Nkenge (CCM), Florent Kyombo akichangia mjadala wa makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara ya Nishati kwa mwaka wa fedha 2025 / 2026 yanayotarajiwa kupitishwa leo bungeni jijiniDodoma. Picha na Hamis Mniha

“Lakini tuone ni jinsi gani Serikali imejipanga. Pamoja na kupata mvua nyingi, isiwe sababu ya adha ya kukatika kwa umeme. Nimefuatilia sana, na ukiwasikiliza wataalamu wanasema ni vegetation (miti kuwa mirefu sana), migomba inakuwa chini ya waya,” amesema.

Hata hivyo, amesema urefu wa migomba hauwezi hata kufika nusu ya urefu ambao waya zimefungwa pamoja na vidhibiti radi, hivyo akaomba suluhu mahsusi kwa Wilaya ya Misenyi juu ya changamoto hiyo.

Wakati wabunge wakieleza hayo, ripoti ya ufanisi wa sekta ndogo ya umeme iliyotolewa Machi mwaka huu inaonyesha kuwa ukatikaji wa umeme ulipungua kwa asilimia 48 kutoka mara 26 (2022/23) hadi mara 14 (2023/24).

Pia, ripoti hiyo ilieleza kuwa muda wa kukatika kwa umeme ulipungua kwa asilimia 64 kutoka dakika 1,536 mwaka 2022/23 hadi dakika 554 mwaka 2023/24.

Aidha, Kyombo ameomba Dk Biteko wakati akihitimisha bajeti yake, atoe jibu kuhusu fidia ya wananchi waliopisha mradi wa Kakono, Wilaya ya Misenyi, Kagera, waliopisha mradi watalipwa lini.

Amesema Julai 2024, Serikali ilisema tathmini imefanyika na wanadai Sh1.6 bilioni, lakini hadi sasa hawajalipwa.

“Wakati unahitimisha, angalau wananchi wa Misenyi wasikie fidia hiyo italipwa lini. Mwaka jana ulisema watalipwa, lakini hadi sasa bado. Kwa sababu wana imani na Serikali ya Mama Samia, wanaamini watapata majibu,” amesema.

Suala la fidia pia liliibuliwa na Mbunge wa Busekelo (CCM), Atupele Mwakibete, aliyesema wananchi wake waliotakiwa kupisha mradi wa umeme wa Lumakali walielezwa watalipwa tangu 2018/19.


Ameomba Serikali kuwalipa wananchi hao wanaodai Sh264 bilioni ili waondoke na kufanya shughuli zao maeneo mengine.

Kuhusu ujenzi kiholela wa vituo vya mafuta, Mwakibete amesema maeneo mengi yana vituo karibu karibu, na akaomba Serikali kuweka usalama kwenye maeneo hayo.

“Ajali ikitokea, ni hatari kwa wananchi wanaoishi maeneo hayo na pia kwa wafanyakazi wanaofanya kazi kwenye vituo hivyo,” amesema.

Kwa upande wa mitungi ya gesi, Mbunge wa Viti Maalumu, Sophia Mwakagenda amesema bado elimu inahitajika, kwani baadhi ya wananchi hutupa mitungi ya gesi waliyopewa na Serikali baada ya kuisha.

Mbunge viti maalumu, Sophia mwakagenda akichangia mjadala wa makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara ya Nishati kwa mwaka wa fedha 2025 / 2026 yanayotarajiwa kupitishwa leo bungeni jijini Dodoma. Picha na Hamis Mniha

“Watu wabaya wasiotakia mema nchi hii wanauza mitungi hiyo kama chuma chakavu. Kuna haja ya kuweka ukali zaidi na ulinzi wa raslimali hizi za Taifa letu,” amesema Mwakagenda.

Kuhusu CSR, Mbunge wa Morogoro Kusini (CCM), Innocent Kalogeris amesema bwawa la umeme la Mwalimu Nyerere limekamilika, lakini suala la CSR halijapata majibu licha ya kulizungumzia mara kwa mara.

Amesema Serikali imekuwa ikisema watakutana na viongozi wa mikoa ya Morogoro na Pwani, lakini bado hakuna taarifa rasmi.

“Nakuomba kaka yangu, wakati unajibu hoja za wabunge, utuambie wana Morogoro na Pwani lini tutapata haki yetu ya CSR. Tunakwenda kwenye uchaguzi; wananchi watatuuliza,” amesema.

Amesema anatamani kushika shilingi ya mshahara wa Dk Biteko wakati wa bajeti ili atoe majibu kuhusu suala hilo.

Mjadala huo utahitimishwa leo Jumanne jioni kwa Dk Biteko kujibu hoja mbalimbali zilizotolewa na wabunge tangu jana.