Beatrice: JB alinileta Bongo Movie

Muktasari:
- mwigizaji huyu amesema ili filamu zinazozalishwa Bongo ziendelee kuwa na ubora ni muhimu kuongeza uwekezaji pamoja na waigizaji na waongozaji kupata elimu ya sanaa.
Wahenga walisema safari moja huanzisha nyingine, kauli hii imejidhihirisha kwa mwigizaji Beatrice Taisamo ambaye alijikuta akianza safari ya uigizaji alipokuwa mwalimu wa ngoma na maigizo katika Taasisi ya Sanaa na Utamaduni Bagamoyo (TaSuBa).
“Nafikiri mwaka 2012 au 2011, kuna Wamarekani flani walikuwa na kampuni yao inaitwa MFDI waliotengeneza filamu ya ‘Siri ya Mtungi’ walikuja hapa TaSuBa wakafanyisha watu ‘audisheni’ namshukuru Mungu nilipata nafasi kwa hiyo nikafanya nao kazi na hiyo tamthilia ‘Siri ya Mtungi’ ndiyo ilikuwa ya kwanza kwangu kuifanya.
“Baada ya hapo nikafanya nao tena filamu ya ‘Tunu’ na ‘Fatuma’ baada ya kazi tatu nikaingia kwenye Bongo Movie, kazi ya kwanza nikafanya na Jacob Steven ‘JB’ iliitwa ‘Haikufuma’ kwa hiyo naweza kusema JB ndiyo alinitoa upande ule akanileta upande huu na wengine wakaanza kuniona,” anasema.
Beatrice aliongezea kuwa waliotengeneza tamthilia ya Siri ya Mtungi walipofika TaSuBa walimkuta tayari ameshakuwa mtumishi wa taasisi hiyo kwani alianza tangu mwaka 2010.
Kutokana na umaarufu wake alioupata kutoka kwenye kazi mbalimbali za uigizaji alizowahi kufanya anasema imewafanya baadhi ya watu kufika kwenye taasisi hiyo kwa ajili ya kusomea sanaa.
“Niseme kwa hiki ninachokifanya imekuwa motisha kubwa sana kwa wanafunzi wetu, wanafurahi ninapokuwa nao darasani kuna wengine ambao siwafundishi lakini bado wanafurahia uwepo wangu.
Hata hivyo, mwigizaji huyu amesema ili filamu zinazozalishwa Bongo ziendelee kuwa na ubora ni muhimu kuongeza uwekezaji pamoja na waigizaji na waongozaji kupata elimu ya sanaa.
“Unajua kitu kikubwa ni kuwa makini lakini pia ukiwa na malengo utapambana na lazima utatengeneza kitu kilicho bora, unaweza kukuta mtu anapambana lakini hana kipato, hizi kazi zinahitaji kipato, ” anasema.
Mbali na filamu mbalimbali alizowahi kucheza Beatrice kwa sasa ni mwigizaji wa tamthilia ya Jua Kali ambapo anaigiza kama mama yake Luka huku muonekano wake kwenye tamthilia hiyo akiwa kama mlokole na pia mlemavu wa miguu.
“Kwenye Jua kali naigiza kama mlokole lakini maisha yangu halisi mimi siyo mlokole ila nampenda Mungu.
“Nilipoambiwa sini yangu ni ya namna gani, niliipenda kwa sababu nilikuwa napenda kuona nafanya kitu cha tofauti ambacho kinaweza kunifanya niwe wa pekee,” anasema.