Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Kutoka dereva teksi hadi mwigizaji nyota wa Siri ya Mtungi

Daudi Michael Tairo

Muktasari:

Mwaka huo huo, Duma alijiunga na kundi la Bahari Artist Group lililokuwa chini ya Mwalimu Joseph Mwasa na Jafari Makatu, ambapo aliweza kujifunza mbinu mbalimbali za uigizaji pamoja na kutunga stori ikiwamo kuandaa (andiko la filamu (‘script’).

Si jambo rahisi kuamini kwamba Daudi Michael Tairo, anayefahamika zaidi kwa jina la Duma ndani ya tamthilia ya Siri ya Mtungi, aliwahi kuwa dereva teksi kwa miaka minne mfululizo.

Duma anasema haikuwa rahisi kwake kuacha kazi hiyo, bali alitumia muda mrefu kuhakikisha anabadili fani yake na kukijenga kipaji cha uigizaji, ambapo ilimchukua muda kukubalika kwani kila kazi aliyokuwa akiifanya haikuweza kuwa na ubora uliotakiwa.

“Baada ya kumaliza shule nilikaa muda mrefu sana kijiweni, baadaye mwaka 2007 niliamua kujifunza udereva na kuanza kuendesha teksi maeneo ya Mabibo. Unajua kadri siku zilivyokuwa zikiendelea katika maisha yangu nilikuwa na shauku ya kuona nafanya kitu kikubwa zaidi hususani katika masuala ya sanaa,” anasema Duma.

Lakini Duma anasema alikuwa na kipaji tangu akiwa shule, na alikuwa anaona wivu jinsi filamu za Kitanzania zinavyoendelea, huku nyingine zikishindwa kufanya vizuri hasa kufikisha ujumbe.

“Mara kwa mara kila nikikaa kuangalia filamu, niliona hazikidhi viwango, nilifikiria kwamba ni wakati mwafaka kuangalia namna ya kuondokana na tatizo hilo, kukosoa baadhi ya mambo haikuwa na faida yoyote kwangu, lakini kwa kuwa nina kipaji niliamua kujiunga na kundi la sanaa ili kuongeza ujuzi zaidi,” anasema.

Mwaka huo huo, Duma alijiunga na kundi la Bahari Artist Group lililokuwa chini ya Mwalimu Joseph Mwasa na Jafari Makatu, ambapo aliweza kujifunza mbinu mbalimbali za uigizaji pamoja na kutunga stori ikiwamo kuandaa (andiko la filamu (‘script’). Chini ya walimu wa kundi la Bahari, aliweza kuonyesha uwezo wake wa sanaa kutoka moyoni na kudhihirisha uwezo wake. Duma alikaa katika kundi hilo kwa kabla ya kuamua kujitegemea katika filamu na kushirikishwa katika baadhi ya filamu zinafikia zaidi ya 25.

Kati ya filamu hizo ni pamoja na filamu ya “My Blood” akiwa kama mhusika mkuu, katika kazi hii alikuwa kinara wa filamu namba mbili alitumia jina la Maliki. Aliwahi kuhusika katika filamu ya “Money Desire”, “Its Too Lets” na filamu nyingine nyingi.

Anasema kwa kuzingatia ubora alioupata kwa kundi lake la awali pamoja na filamu alizoigiza, aliamua kuanzisha studio yake iliyojulikana kama D.Production na kufanikiwa kutoa filamu yake ya kwanza ya ‘Upside Down’ ambayo aliweza kuiigiza kwa ustadi mkubwa.

“Hii ni filamu yangu ya kwanza kuiandaa, lakini haikuweza kufanya vizuri “Upside Down”, ni kati ya filamu zilizowahi kunipa shida wakati wa kuziandaa, kwani nilihitajika kuigiza kama kichaa nikiwa kati kati ya jalala kuu la Kigogo ,lakini nilifanikiwa na kweli jamii ilikubali japokuwa haikufanya vizuri sana sokoni,” anasema akiitaja nyingine iliyompa shida kuiandaa kuwa ni “Its Too Late” aliyoigiza kama anabaka.

Akielezea juu ya kazi yake hiyo, anasema ameweza kufanikiwa kutoa filamu nne ambazo ni ‘Upside Down”, “Where Is Love” na “Fake Pregnant,” “Aunt Suzzy” na “Magic Money.”

Kuhusu filamu ya “Fake Pregnant”, anasema aliumiza kichwa kuiandaa “lakini inanipa faraja kubwa kwani imejaa mafundisho hata wadau wameipokea kutokana na simu zao walizonipigia’ anasema Duma na kufafanua kuwa filamu hiyo ina wasanii kama Ester Flavian, Soud Ally, Amina Kibiki, Ayubu Santana na Mboto.

Siri ya Mtungi

Duma anasema haikuwa rahisi yeye kutengeneza sehemu ya kwanza ya Tamthilia ya Siri ya Mtungi inayoonyeshwa kupitia ITV na Channel 10. “Nakumbuka nilipata “dili” hili siku 30 baada ya kuachia filamu yangu ya “Magic Money” ninaita ‘dili’ kwa kuwa ni kazi iliyobadilisha maisha yangu kwa kiasi kikubwa. Novemba 9, 2012 niliachia filamu yangu ya Magic Money na Desemba 9, 2012 Siri ya Mtungi ilianza kuonyeshwa rasmi katika Televisheni ya ITV na Channel 10, kwa kweli ulikuwa ni mwaka mzuri kwangu,” anasema Duma.

“Nimejifunza mambo mengi, unajua wenzetu wanaigiza vizuri zaidi na kunakuwa na uhalisia, uhalisia wa kazi husika, japokuwa waigizaji tunakumbana na changamoto nyingi hasa katika umaliziaji wa kipande husika lakini ni changamoto zinazotujenga,” anasema Duma anayetarajia kuachia filamu yake mpya “Kinyongo” inayotarajiwa kuachiwa hivi karibuni.

Akielezea sehemu iliyompa changamoto wakati wa uandaaji wa tamthilia ya Siri ya Mtungi inayotarajiwa kuanza kuonyeshwa tena sehemu ya pili wiki chache zijazo, anasema ni pale alipokuwa na wasichana wengi waliokwenda kumfumania mdogo wake.

Malengo yake

Duma anasema anataka kwenda kusomea fani hiyo ya sanaa nje ya nchi hususani uandaaji ili kuwa na studio kubwa ya masuala ya filamu hapa nchini.

Anasema soko la filamu kwa wakati huu limekuwa kutokana na kuongezeka kwa filamu sokoni zinazalishwa kila kukicha na wandaaji wanaotaka kuona mara zote filamu zinaingia sokoni, hali hiyo ni tofauti kabisa na kipindi cha nyuma ambacho tulikuwa tukishuhudia filamu moja ikitamba sokoni kwa zaidi ya miaka miwili hadi mitatu.

Historia yake

Daud Michael Tairo “Duma” alizaliwa mwaka 1984 mkoani Tanga katika Wilaya ya Korogwe, kwa mama yake ni mtoto wa pekee wakati kwa baba yake ni wa tatu. Alipata elimu katika Shule za Msingi Msasani na Sinza.

Alijiunga na Sekondari ya Sinza hadi kidato cha tatu, lakini kutokana na matatizo ya kifamilia, aliachana na shule na kuanza kujihusisha na masuala ya ufundi makanika (gereji), baadaye alijifunza udereva na kuanza kuendesha teksi.