Samia aonya ramli chonganishi kuelekea Uchaguzi Mkuu

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan akizungumza na Watemi wa kabila la Wasukuma mara baada ya kutembelea Kituo cha Utamaduni na Makumbusho ya Wasukuma Bujora, Kisesa mkoani Mwanza Juni 21, 2025.
Muktasari:
- Machifu na watemi wametakiwa kudumisha mila, desturi na tamaduni za Kitanzania kwa kuwa ni kielelezo cha uhai wa tamaduni zilizorithiwa kutoka kwa mabibi na mababu.
Mwanza/Dar. Rais Samia Suluhu Hassan amewataka viongozi wa kimila, hususani waganga wa kienyeji kujiepusha na ramli chonganishi kuelekea Uchaguzi Mkuu wa Oktoba, 2025 ili zisilete uvunjivu wa amani.
Akizungumza kwenye tamasha la utamaduni la Bulabo lililofanyika Bujora, wilayani Magu, mkoani Mwanza leo Jumamosi Juni 21, 2025 amesema kipindi hiki waganga hao watatembelewa na watu mbalimbali wanaotaka kugombea nafasi za uongozi.
"Ombi langu hasa kwa ndugu zetu wa kimila... waganga wale wa kienyeji, kipindi hiki wanaoomba kupata nafasi mbalimbali watawatembelea, na wanapowatembelea niombe sana tusifanye ramli chonganishi kwa sababu hizo ndizo zinavunja amani kwenye uchaguzi," amesema.

Amewaambia kama mgombea atakwenda na fedha, wazile na kumwambia atashinda bila kusambaza chuki.
“Kama anakuja na fungu we kula fungu, umemuona atashinda mwambie utashinda, umemuona hatashinda mwambie baba we nenda tu mambo mazuri, kula pesa yako nenda kalale,” amesema na kuongeza:
“Lakini tusifanye ramli chonganishi kuwa naona kama utashinda lakini kuna katibu wako huyu wa mkoa kama hakupendipendi hivi, hapana, twende tufanye mambo kwa murua ili watu wote waende vizuri, tumalize uchaguzi vizuri.”
Pia, amewaomba machifu na watemi kudumisha mila, desturi na tamaduni za Kitanzania kwa kuwa ni kielelezo cha uhai wa tamaduni zilizorithiwa kutoka kwa mabibi na mababu.
Amesema sehemu nyingine ya tamaduni za Kitanzania ni kuchagua viongozi katika chaguzi mbalimbali, hata machifu wanachaguana muda ukiisha.
"Lakini kisiasa tuna mila na tamaduni ya kuchaguana kila baada ya miaka mitano," amesema akiwataka machifu kuhamasisha wananchi kujitokeza wakati ukifika ili wachaguliwe viongozi watakaoiletea nchi maendeleo.
"Niwaombe machifu wenzangu, watemi na viongozi wa kimila kuendelea kuliombea Taifa letu… tunakwenda kwenye uchaguzi, uchaguzi uwe wa amani, watu waende wachaguane kwa amani, tumalize vizuri," amesema.
Kuhusu matamasha
Akizungumzia matamasha ya kiutamaduni, Samia amesema Serikali imeamua kuyakuza na kudumisha utamaduni, mila na desturi zilizopo nchini kwani kutunza utamaduni ni sehemu muhimu ya kulinda maadili ya nchi.
“Utamaduni hubeba na kurithisha imani, tabia na maadili yanayofaa kutoka kizazi kimoja kwenda kingine. Maadili kama heshima, uwajibikaji, uaminifu na mshikamano, hujengwa na kuimarishwa kupitia mila na desturi na taratibu za kiutamaduni za eneo husika,” amesema.

Amesema karne ya sasa ambayo kuna mabadiliko ya teknolojia, uchumi na kijamii, utamaduni ndiyo unabaki kuwa utambulisho utakaosaidia kujua nani ni nani, anatoka wapi na anataka nini.
“Utamaduni ni muhimu katika kukabiliana na mmomonyoko wa maadili ambao katika ulimwengu wa sasa kuna shinikizo kubwa la kuiga tamaduni ngeni ambazo haziendani na maisha na maadili ya Mtanzania, hatimaye kuvuruga amani na utulivu wa jamii,” amesema.
Samia amesema ni vyema kulinda utamaduni, kuuendeleza na kurithisha maadili mema kwa vizazi vijavyo.
Tamasha la Bulabo amesema ni jukwaa muhimu la kuweza kurithisha, kuhifadhi na kuendeleza mila na desturi njema za Kitanzania ambazo ni msingi wa utambulisho utamaduni wa Taifa.
“Hivyo ni vyema kuendelea kudumisha mila na desturi za Kitanzania kwani ni kielelezo cha uhai wa tamaduni zilizorithiwa kutoka kwa mabibi na mababu,” amesema.
Rais Samia alipata fursa ya kutembelea mabanda yenye vitu na zana za kiutamaduni.
Tafiti kufanyika
Awali, akimkaribisha Rais Samia kufungua tamasha hilo, Waziri wa Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo, Profesa Palamagamba Kabudi alisema wizara imeanza matayarisho ya awali ya kulifanya tamasha la Bulabo kuwa sehemu ya urithi wa utamaduni wa dunia.

"Tupo katika hatua za mwisho kuwasilisha pendekezo hilo Unesco (Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni) ili sherehe hizi zitambuliwe kuwa urithi wa utamaduni usioshikika wa dunia unaosimamiwa na Unesco," amesema.
Amesema pia wanaendelea na utafiti wa sherehe za kimila za makabila mengine ili nayo yaorodheshwe kwenye utamaduni wa urithi wa dunia usioshikika.
Profesa Kabudi amesema tayari wamemaliza kazi ya kuandaa mwongozo wa utamaduni na maadili ya Mtanzania ambao umekuwa rejea kwa makundi mbalimbali ya kijamii na kujikita katika kupunguza viashiria vya mmomonyoko wa maadili unaosababishwa na watu wachache.
Pia mwongozo wa wazee wa kimila, hususan machifu katika kuenzi maadili ya Mtanzania na tayari rasimu ya kwanza imetolewa maoni na makundi mbalimbali ya kijamii, wakiwamo machifu wenyewe na sasa maoni hayo yanachakatwa.
“Mwongozo huo utakapoanza kutumika, utasaidia kuondoa mgongano wa utekelezaji wa jukumu la kuenzi maadili ya Mtanzania kwa kuwa umebainisha namna Serikali inavyoweza kushirikiana na viongozi wa kimila, kidini na viongozi wa kijamii kuenzi na kulinda maadili yetu,” amesema.

Katibu wa Machifu nchini, Aron Mikomangwa amesema tamasha hilo linalenga kuwawezesha machifu wa Tanzania kuzungumza kuhusu masuala ya kiutamaduni, kuonyesha utamaduni wa Kanda ya Ziwa, kukuza ufahamu na asili ya utamaduni wa Mwafrika na kurithisha tunu chanya za kitamaduni kwa vizazi vilivyopo na vijavyo.
Tamasha hilo limehudhuriwa na machifu kutoka nchi nzima na baadhi ya wageni kutoka nje ya nchi wanaopenda tamaduni za Kisukuma wakiwamo kutoka, Afrika Kusini, Canada na Oman.
Machifu hao wamemkabidhi Rais Samia kiti cha kichifu kwa awamu ya pili wakisema wamekubaliana kuwa, Rais Samia ambaye walimpa uchifu na kumuita Chifu Hangaya kukikalia tena kwa miaka mitano, kikiwa kimechongwa kwa taratibu za kijadi.
Mikomagwa amesema pia litahamasisha wananchi kujitokeza kupiga kura katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba, 2025, kulinda maadili, mila na mazingira.

Amemuomba Rais tamasha lifanyike chini ya ofisi yake na kufadhiliwa. Pia amemuomba awe mlezi wa tamasha hilo, liandaliwe na machifu wa Bulabo, uwanja ujengwe ili udumishe kumbukumbu ya yeye kusimikwa kuwa chifu Hangaya lakini pia kuendeleza maonyesho ya utamaduni.
Rais Samia amesema tamasha hilo litakuwa chini ya Wizara ya Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo, akikubali ombi la kuwa mlezi na kujengwa kwa uwanja ambao utaitwa jina la Chifu Hangaya na kuendelea kuandaliwa na machifu hao.
Mwenyekiti wa Umoja wa Machifu Tanzania, Chifu Anthonia Sangalali amesema wataendelea kumlinda Rais Samia kwa kuwa anaheshimisha mila na utu, hivyo machifu hawataruhusu aguswe katika uongozi wake.
Katika tamasha hilo, machifu wametoa ng'ombe watatu wa maziwa kwa ajili ya Rais Samia.
Askofu Mkuu wa Kanisa Katoliki Jimbo Kuu la Mwanza, Renatus Nkwande amempongeza Rais Samia kwa kuleta maendeleo ya kiuchumi na ya kijamii, akimshukuru kwa kutoa kibali cha utunzaji na umiliki wa nyara za Serikali katika kituo cha makumbusho Bujora akisema ni jambo linaloonyesha utambuzi wa nafasi ya utamaduni wa Kiafrika.
Ameshauri machifu kutumika kukumbusha jamii jadi njema ili kulinda maadili nchini.

"Uwepo wa viongozi wa kijadi ni kielelezo tosha kuwa hata sisi Waafrika tupo, tulikuwepo hata kabla ya ujio wa wageni. Kubeza kila cha kwetu na kuhusudu cha kigeni ni mawazo potofu, tuwaenzi wazee wetu hawa.
"Tukumbuke tulipotoka na tukumbushwe jinsi tulivyoishi… tuliishi kwa upendo, kwa amani hata kama kilitokea chochote kimsingi katika historia unaona yalikuja machafuko baada ya wageni kufika," amesema.
Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Said Mtanda amesema tamasha hilo lina nia ya kuenzi mila na utamaduni wa Mtanzania ambao Rais amekuwa kinara wa kuhifadhi utamaduni, kwani ndiye aliyeanzisha tamasha la Kizimkazi na ni mlezi wa muda mrefu wa tamasha la Bulabo.