Rais Samia aonya utunzaji wa amani, azindua mradi wa maji

Muktasari:
- Rais Samia amesema kwa kuwa kuna utulivu, wahisani na wafadhili wanachangia na kutoa mikopo nafuu kwenye miradi.
Mwanza. Serikali imewataka Watanzania kudumisha amani na utulivu, kwa ajili ya maendeleo na sifa nzuri ya Tanzania.
Rais Samia Suluhu Hassan amebainisha hayo leo Juni 20, 2025 jijini Mwanza wakati akizungumza na wananchi wa Butimba, akiwaeleza kwamba Tanzania ina amani na utulivu na utashi wa kisiasa katika kutekeleza miradi ya maendeleo. Amewataka kutulia na kufanya kazi.

“Kama ni maendeleo, Tanzania ina maendeleo, kama ni utashi wa kisiasa, utashi wa kisiasa wa kuleta maendeleo ndani ya Tanzania upo na utaendelea kuwepo.

“Niwaombe ndugu zangu kutunza amani na utulivu. Tulete utulivu wa kisiasa nchi yetu ibakie kuwa na Amani... Tutulie tufanye kazi zetu tulete maendeleo,” amesema Rais Samia.
Amesema kwa kuwa kuna utulivu, wahisani na wafadhili wanachangia na kutoa mikopo nafuu kwenye miradi.
“Mkianza kutawanyana hapa, hakuna litakalofanyika na hili ndilo wengine wanapenda litokee, niombe sana ndugu zangu tuweke sifa ya nchi yetu...Tanzania ni salama twende tukafanye kazi,” ameongeza.
Mradi wa maji
Akizungumza mradi wa maji, Rais Samia amesema ziara zake mbili mkoani Mwanza alikutana na kilio cha wananchi wakililia maji.

Akiwaambia chanzo hicho kilichojengwa kwa zaidi ya Sh71 bilioni kitaboresha upatikanaji wa maji safi na salama kwa wakazi 450,000 wa jijini Mwanza na viunga vyake.
Amezishukuru taasisi na wadau wa maendeleo walioshirikiana na Serikali kutoa ruzuku na mikopo nafuu kutekeleza mradi huo, ambao wawakilishi wake wameahidi ushirikiano wa utekelezaji wa mradi wa maji Butimba kwa awamu ya pili.
“Uwekezaji uliofanywa na unaoendelea kufanywa umeghalimu fedha nyingi sana. Hivyo niwaombe wote tulinde na tutunze miradi hii ili iwe endelevu kwa kizazi hiki na kijacho,"ameeleza Rais Samia.

"Mradi huu umehusisha ujenzi wa matundu vyoo 107 katika maeneo ya umma ikiwemo ma-shuleni, masokoni na stendi za magari na mabasi,"amesema Rais Samia.
Katika hatua nyingine, Rais Samia mewataka wakazi wa Kanda ya Ziwa kutunza mazingira hasa yanayozunguka Ziwa Victoria kwakuwa ndiyo chanzo kikuu cha upatikanaji maji.

"Naagiza juhudi za kuhifadhi mazingira ziendelee kufanyika kikamilifu kwa kushirikiana na taasisi zote. Huu ni mradi mkubwa lazima tutunze mazingira ili ziwa liendelee kuwepo na liwepo kwa vigezo vyake lisikauke tukarudi tena huko nyuma,"ameeleza.
Aida, amewataka wananchi kulipa ankara za maji ili zitumike kuendesha miundombinu na kutoa huduma hiyo endelevu, huku akiwataka watumishi wa idara ya maji kutobambikizia wananchi malipo ya ankara za huduma hiyo.
Mradi wa maji Butimba
Akitoa taarifa kwa Rais Samia, Katibu Mkuu Wizara ya Maji, Mwajuma Waziri amesema mradi huo utazalisha lita milioni 48 za maji kwa siku.
Waziri wa Maji, Jumaa Aweso amesema kulikuwa na kitendawili kigumu kwa wakazi wa Mwanza, walikuwa wakihoji kwanini maji ya Ziwa Victoria yanapelekwa mikoa mingine wakati wenyewe hawana.

"Moja ya kilio chenu Ziwa victoria litumike kutatua changamoto za maji. Nataka niwambie wana Mwanza, Kanda ya Ziwa baada ya dhiki siyo ziki, baada ya dhiki ni faraja,"amesema.
Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Said Mtanda amesema mahitaji ya maji mkoani Mwanza ni lita milioni 172 kwa siku na uwezo wa uzalishaji kwa sasa ni lita milioni 138 kutoka chanzo cha Capripoint na Butimba.

Amesema hali ya upatikananji wa maji Mwanza imeongezeka kutoka asilimia 57 mwaka 2021 hadi asilimia 85 mwaka 2025 sawa na ongezeko la asilimia 27.
Amesema tayari miradi 80 ya vijijini imekamilishwa mkoani humo yenye thamani ya Sh81.3 bilioni.