Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Samia: Viongozi wa dini ponyeni mioyo ya watu

Muktasari:

  • Rais Samia Suluhu Hassan amewataka sungusungu kutoa ushirikiano na kufanya kazi karibu na wakuu wa mikoa na wilaya, wakurugenzi wa halmashauri na wakuu wa taasisi mbalimbali kulinda usalama wa wananchi na miundombinu.

Mwanza. Rais Samia Suluhu Hassan amewataka viongozi wa dini kuponya mioyo ya Watanzania katika kipindi hiki kuelekea Uchaguzi Mkuu wa Oktoba, 2025 akieleza inatokea migogoro, kugombana na kutofautiana.

Amesema hayo leo Ijumaa Juni 20, 2025 alipozungumza kwenye hafla ya siku ya Sungusungu iliyojumuisha mikoa mitano ya Kanda ya Ziwa katika uwanja wa CCM Kirumba, jijini Mwanza. Jeshi hilo la jadi limetimiza miaka 42 tangu kuanzishwa.

Hafla hiyo pia ilihudhuriwa na sungusungu, viongozi wa dini na bodaboda wanaojulikana kama maofisa usafirishaji.

Rais Samia amesema kikatiba Tanzania haina dini, lakini Watanzania wana dini zao, akitoa shukrani kwa kuundwa umoja wa amani unaoweza kushughulikia changamoto za kidini zinapojitokeza.

“Lakini pia unaweza kushughulikia migogoro au changamoto zinazojitokeza na kuiacha nchi yetu ibaki salama. Ninyi ndio madaktari wa nyoyo zetu, niwaombe mwendelee na kazi adhimu ya kulea na kuponya nyoyo zetu, hasa pale tunapofarakana,” amesema na kuongeza:

“Kipindi hiki cha kuelekea uchaguzi tutakwazana, tutagombana, tutatofautiana. Niwaombe wadau wa amani kuingia na kufanya kazi ya kuponya nyoyo zetu ili nchi yetu ibaki salama. Nimuombe Mungu awawezeshe muifanye kazi hiyo kwa weledi mkubwa.”

Wito kwa sungusungu

Kuhusu sungusungu amewataka kutoa ushirikiano na kufanya kazi karibu na wakuu wa mikoa na wilaya, wakurugenzi wa halmashauri na wakuu wa taasisi mbalimbali kulinda usalama wa wananchi na miundombinu.

“Utunzaji wa amani, utulivu na usalama ndani ya nchi ni jukumu letu sote. Hivyo walinzi wa jadi ‘sungusungu’ ninyi ni walinzi wa mila zetu zile, si potofu na desturi zetu. Amani na utulivu wa Taifa letu ninyi ndio walinzi wa mambo yote hayo,” amesema Samia aliyeridhia kuwa mtemi wa Sungusungu na kuongeza:

“Tushirikiane ipasavyo na viongozi wakiwamo Jeshi la Polisi kuimarisha amani katika maeneo yetu, hasa katika kipindi hiki sote tuwe macho, tuwe walinzi wa wenzetu, walinzi wa jamii zetu tunakoishi.”

Awali, mwakilishi wa sungusungu, Richard Bundala akitoa salamu alimwomba Rais Samia apokee hadhi ya utemi akisema wamefufua shughuli za ulinzi wa jadi katika maeneo yao ili kushirikiana na vyombo rasmi vya usalama wa Taifa.

Amesema sungusungu walianzishwa miaka ya 1980 kama jibu la wananchi kukabiliana na uhalifu uliokuwa ukishamiri, hasa wizi wa mifugo na mauaji katika maeneo ya Kanda ya Ziwa.

Amesema jukumu la kulinda nchi ni la kila Mtanzania, hivyo ushiriki wa vikundi vya jadi katika ulinzi, bado ni halali na wa kuungwa mkono.

“Tunatoa wito kwa Watanzania wote kushiriki kwa vitendo katika ulinzi wa nchi yetu. Sababu zilezile za mwaka 1971 bado zipo leo,” amesema.

Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani, Daniel Sillo ameagiza vijiji ambavyo havina vikundi vya sungusungu mkoani Mwanza vikamilishe uundwaji wake, akisema ni msaada katika ulinzi na vimefanikiwa kuzuia uhalifu katika maeneo yao.

Amesema Mkoa wa Mwanza wenye vijiji 544, kati ya hivyo 461 ndivyo vina vikundi vya sungusungu.

Sillo amesema sungusungu 55,000 mkoani Mwanza wanatambuliwa au kufanya kazi kwa ushirikiano wa karibu na Jeshi la Polisi katika wilaya za Kwimba, Misungwi, Magu na Sengerema.

“Jeshi la Polisi Mkoa wa Mwanza na mikoa ya Kanda ya Ziwa limekuwa likiendelea na mpango wa utoaji elimu kupitia polisi jamii, mafunzo mbalimbali yakiwamo ya kuwezesha sungusungu hutolewa kupitia wakaguzi wa kata au polisi kata,” amesema.

Sillo amesema lengo la mafunzo ni kushirikisha jamii katika kuzuia uhalifu kabla haujatendekea, kuibua vikundi vya ulinzi shirikishi na kuhuisha vikundi vya ulinzi wa jadi na kutoa elimu ya sheria inayotumika kwa sungusungu.

Ameliagiza Jeshi la Polisi kuendelea kushirikiana na machifu wa sungusungu wa ngazi zote za kanda, mikoa na wilaya kwa lengo la kuendelea kutoa elimu kwa vikundi vyote ili kuongeza uelewa na ufanisi wao katika utawala wa himaya zao.

Katibu Tawala wa Mkoa wa Mwanza, Balandya Erikana amesema hafla hiyo imehusisha sungusungu kutoka mikoa ya Mwanza, Shinyanga, Simiyu, Geita na Tabora.

Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Said Mtanda amesema Wilaya ya Kwimba ina sungusungu 36,000 ambao wamewakilishwa na wenzao 15,000 kwenye hafla hiyo, Misungwi ikiwakilishwa na sungusungu 7,000 kati ya 20,000 waliopo, huku Magu ikiwakilishwa na sungusungu 3,000 na Sengerema 500.

“Tukisema tuwaite sungusungu wote wa mkoa huu, uwanja huu usingewatosha. Uwepo wao ni ishara ya shukrani kwa jinsi Serikali inavyowatendea haki,” amesema.


Kuhusu bodaboda

Rais Samia akiwazungumzia bodaboda amesema Serikali itaendelea kuweka mazingira bora ili kurahisisha shughuli zao ndani ya nchi, akiwaomba kuongeza umakini barabarani na kuchunga usalama wa abiria.

“Kuna wachache wanaowaharibia sifa kwa kutumia usafiri wenu na kufanya vitendo vya kihalifu, naomba mlindane. Kuweni walinzi wenyewe kwa wenyewe, lakini chungeni usalama wa abiria zenu,” amesema.

Mwenyekiti wa Umoja wa Waendesha Bodaboda Mkoa wa Mwanza, Mohamed Idd ameipongeza Serikali kwa kufuta kodi ya mapato ya Sh65,000 kwa mwaka kwa waendesha bodaboda na kupunguza ada ya leseni kutoka Sh70,000 hadi Sh30,000.

Amesema wameanzisha Saccos ya Maafisa Usafirishaji, ambayo tayari imekusanya Sh3 milioni, wakiwa na lengo la kufikia Sh50 milioni ili kuwezesha mikopo nafuu kwa wanachama.

“Tunaamini kwa Saccos yetu tutapunguza utegemezi wa mikopo kandamizi ya pikipiki na kuweza kujenga uchumi wa madereva nchini,” amesema na kumuomba Rais Samia kuwachangia ili watimize lengo la kukusanya kiasi hicho. Amekubali ombi lao.


Mradi wa maji

Mapema, Rais Samia aliwataka Watanzania kudumisha amani na utulivu kwa ajili ya maendeleo na sifa nzuri ya Tanzania.

Amesema hayo jijini Mwanza alipozungumza na wananchi baada ya kuzindua mradi wa maji wa Butimba, akiwaeleza kwamba Tanzania ina amani na utulivu na utashi wa kisiasa katika kutekeleza miradi ya maendeleo.

“Kama ni maendeleo, Tanzania ina maendeleo, kama ni utashi wa kisiasa, utashi wa kisiasa wa kuleta maendeleo ndani ya Tanzania upo na utaendelea kuwepo.

“Niwaombe ndugu zangu kutunza amani na utulivu. Tulete utulivu wa kisiasa nchi yetu ibakie kuwa na amani... Tutulie tufanye kazi zetu tulete maendeleo,” amesema.

Samia amesema kwa kuwa kuna utulivu, wahisani na wafadhili wanachangia na kutoa mikopo nafuu kwenye miradi.

“Mkianza kutawanyana hapa, hakuna litakalofanyika na hili ndilo wengine wanapenda litokee, niombe sana ndugu zangu tuweke sifa ya nchi yetu... Tanzania ni salama twende tukafanye kazi,” amesema.

Rais Samia amesema katika ziara zake mbili mkoani Mwanza alikutana na kilio cha wananchi wakililia maji na kuwa chanzo hicho kilichojengwa kwa zaidi ya Sh71 bilioni kitaboresha upatikanaji wa majisafi na salama kwa wakazi 450,000 wa jijini Mwanza na viunga vyake.

Amezishukuru taasisi na wadau wa maendeleo walioshirikiana na Serikali kutoa ruzuku na mikopo nafuu kutekeleza mradi huo ambao wawakilishi wake wameahidi ushirikiano katika utekelezaji wa mradi kwa awamu ya pili.

“Uwekezaji uliofanywa na unaoendelea kufanywa umegharimu fedha nyingi. Hivyo niwaombe wote tulinde na tutunze miradi hii ili iwe endelevu kwa kizazi hiki na kijacho," amesema.

"Mradi huu umehusisha ujenzi wa matundu ya vyoo 107 katika maeneo ya umma ikiwamo shuleni, sokoni na stendi za magari na mabasi," amesema.

Rais Samia amewataka wakazi wa Kanda ya Ziwa kutunza mazingira hasa yanayozunguka Ziwa Victoria kwa kuwa ndiyo chanzo kikuu cha upatikanaji maji.

"Naagiza juhudi za kuhifadhi mazingira ziendelee kufanyika kikamilifu kwa kushirikiana na taasisi zote. Huu ni mradi mkubwa lazima tutunze mazingira ili ziwa liendelee kuwepo na liwepo kwa vigezo vyake, lisikauke tukarudi tena huko nyuma," amesema.

Amewataka wananchi kulipa ankara za maji ili zitumike kuendesha miundombinu na kutoa huduma hiyo endelevu, huku watumishi wa idara ya maji wakiagizwa kutobambikizia wananchi malipo ya ankara za huduma hiyo.

Katibu Mkuu Wizara ya Maji, Mwajuma Waziri amesema mradi huo utazalisha lita milioni 48 za maji kwa siku.