Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Sakata la Toto Afya Kadi laibuka tena bungeni

Mbunge wa Viti Maalum, Rehema Migila akiuliza swali bungeni. Picha na Hamis Mniha

Muktasari:

  • Serikali ina mpango gani wa kuwasaidia watoto kupata matibabu baada ya kufuta Toto Afya Kadi huku tukisubiri Sheria ya Bima ya Afya kwa Wote (UHC).

Dodoma. Sakata la Toto Afya Kadi limetinga tena bungeni na Serikali imeendelea kusisitiza msimamo wake kuwa kilichobadilika ni utaratibu wa kujiunga kupitia makundi, badala ya mtoto mmoja mmoja.

Mbunge wa Viti Maalum Rehema Migila ndiye aliyeibua suala hilo katika kipindi cha maswali na majibu leo Mei 27, 2024.

“Je, Serikali ina mpango gani wa kuwasaidia watoto kupata matibabu baada ya kufuta Toto Afya Kadi huku tukisubiri utekelezaji wa Sheria ya Bima ya Afya kwa Wote,” amehoji.

Akijibu swali hilo, Naibu Waziri wa Afya, Dk Godwin Mollel amesema mfumo wa kulipia bima za watoto kupitia Toto Afya Kadi umebadilika.

Amesema watoto wanajiunga kupitia utaratibu wa shule na vifurushi vya bima ya afya vya Najali, Wekeza na Timiza ambapo wanajiunga kupitia wazazi wao.

Dk Mollel amesema kuanza utekelezaji wa Sheria ya Bima ya Afya kwa Wote utawezesha makundi mbalimbali ya wananchi wakiwemo watoto kupata huduma za Afya kwa urahisi pasipo kuwa na vikwazo.

Katika Swali la Nyongeza, Migila ameuliza kwa kuwa mfumo wa Bima ya Afya kwa Wote haujaanza, watoto wamekuwa wakiugua na kupelekwa hospitali huku wazazi wao wakiwa hawana uwezo kulipia vifurushi, kwa nini Serikali isiruhusu watoto walio chini ya miaka 18 kulipa Sh50,400 kama ilivyokuwa awali?

Mbunge huyo amesema sera ya afya inasema matibabu kwa mtoto aliye chini ya umri wa miaka mitano ni bure, hali hiyo inawafanya wazazi wengi mtoto anapoumwa kumpeleka hospitali lakini huko nako hudaiwa barua ya rufaa ambazo wazazi hawana.

“Watumishi wetu hawa wanamuona mtoto kuwa ana chini ya miaka mitano lakini wanadai barua za rufaa, hatuoni kwamba tuna mpango wa watoto wetu wafe,” amehoji Migila.

Akijibu maswali hayo, Dk Mollel amesema ukipiga hesabu ya watoto walio na umri wa miaka 21 wanafika zaidi ya milioni 30 lakini waliokuwa kwenye Toto Afya Kadi walikuwa ni 200,000 tu.

Amesema hivi sasa watoto zaidi ya milioni 30 wanapata matibabu kama kawaida na hakuna malalamiko.

Amesema watoto hao wanaingia katika makundi ili kutimiza sheria na taratibu zinazotakiwa katika bima ya afya.

Amesema kwa utaratibu huo mpya, wanaweza kuulinda Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya.

“Kama tulivyosema walikuwa wanachangia Sh5 bilioni lakini wanatumia Sh49 bilioni, maana yake walikuwa wanatumia fedha za watumishi wa umma au watu wengine waliochangia,” amesema.

Amesema kwa kupitia njia hiyo na nyingine watoto hao milioni 30 wanapata huduma na Serikali itaendelea kutoa huduma na hawatapata shida.

Kuhusu changamoto za watoto chini ya miaka mitani, Dk Mollel amekiri kuwepo changamoto kwa watoto waliochini ya miaka mitano kwenye matibabu.

Amesema licha ya kuwepo kwa utaratibu huo, Serikali haijaweza kutoa matibabu bure kwa asilimia 100, lakini imeweza kufanya hivyo kwa zaidi ya asilimia 70.

Amesema kumekuwa na shida kwa watoto wanapopata tatizo la afya dogo, hata kifua tu, kupelekwa kwenye hospitali za mikoa badala ya kuanzia ngazi ya chini.

Amesema wataalamu wa afya wamekuwa wakisisitiza watoto hao wapate matibabu katika hospitali zilizo karibu na zinazozunguka maeneo wanayoishi.