Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Bunge lataka wanafunzi wote wajiunge huduma bima ya afya

Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Afya na Masuala ya Ukimwi, Stanslaus Nyongo.

Dodoma. Bunge limeazimia Serikali iweke mwongozo wa ulazima kwa wanafunzi wote kusajiliwa katika huduma za bima ya afya.

Maazimio hayo yametokana na pendekezo lililotolewa na Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Afya na Masuala ya Ukimwi, Stanslaus Nyongo wakati akiwasilisha taarifa ya shughuli za kamati hiyo kwa mwaka 2023 bungeni jana, jijini Dodoma.

Maazimio hayo yamekuja kukiwa na danadana nyingi tangu Machi 13, mwaka jana ambapo Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF), ulitangaza kubadili utaratibu wa kuwasajili wa watoto.

NHIF ilibadili utaratibu kutoka ule wa awali ulioanzishwa mwaka 2016 wa kuwasajili kwa bima ya afya ya Toto Afya Kadi na kuwasajili kupitia vifurushi au shule wanazosoma.

Utaratibu huo uliwaibua watu wengi waliotaka Serikali kufikiria upya, kwa sababu watoto walio chini ya miaka mitano watashindwa kupata huduma hiyo kwa kuwa hawajafikia umri wa kuanza shule.

Baadhi walipinga mfumo huo wakisema umelenga kuwatenga watoto hasa wanaotoka shule zenye idadi ndogo ya wanafunzi, familia duni na wale tegemezi.

Kilio cha Watanzania wengi kwenye Toto Afya Kadi ilikuwa kutengwa na mfumo wa bima, watoto wenye umri wa chini ya miaka mitano kwa kile kilichoelezwa watumie mfumo wa matibabu bure.

Akiwasilisha taarifa hiyo, Nyongo alisema kukosekana kwa mwongozo wa ulazima kwa wanafunzi wote kusajiliwa katika huduma za bima ya afya kupitia shule kumesababisha watoto wengi kukosa huduma hiyo.

Alisema hakuna mwongozo wa kufanikisha usajili wa watoto katika huduma za bima ya afya shuleni kupitia NHIF.

Alisema kukosekana kwa mwongozo huo kunadhoofisha mwitikio wa usajili wa watoto katika huduma za bima ya afya.

“Bunge limeazimia Wizara ya Afya kwa kushirikiana na Wizara ya Elimu iweke mwongozo wa ulazima, kwa wanafunzi wote kusajiliwa katika huduma za bima ya afya kupitia shule,” alisema.

Pia, Nyongo alitaka Serikali iweke mfumo na utaratibu wezeshi wa bima kwa watoto wenye umri chini ya miaka mitano ambao hawajaanza shule.


Nyongo alitaka Serikali kutafuta ufumbuzi wa haraka wa mvutano kati ya NHIF na sekta binafsi, ili wananchi waendelee kupata huduma za afya bora katika vituo vya afya wanavyopendelea.

Mvutano huo ulitokana na NHIF kutangaza kitita kipya cha mafao Desemba 18, 2023 ambacho kililenga kuongeza au kupunguza gharama katika baadhi ya huduma, ili kuendana na bei halisi ya soko.

Hata hivyo, mabadiliko hayo yalipokelewa kwa hisia tofauti ambapo vituo binafsi vya afya vilisema havikushirikishwa wakati wa maandalizi ya mabadiliko hayo.

Mvutano huo ulisababisha Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu kuunda kamati kwa ajili ya kuchunguza na kuja na mapendekezo yatakayosaidia kuondoa msuguano huo.

Nyongo alisema kamati yake imebaini ushirikiano kati ya NHIF na sekta binafsi ya afya umekuwa ukisuasua kutokana na mambo mbalimbali, ikiwemo sheria ya mfuko wa bima kutokutambua uwepo wa sekta binafsi kama mnufaika wa mfuko huo.

Alisema kamati yake imebaini mambo ambayo yalisababisha mvutano huo ni kutoruhusu sekta binafsi za afya kutumia mfumo wa kuchangia huduma za afya (Co-payment) kwa wanufaika wa NHIF, wakati mfumo huo unaruhusiwa kwa hospitali za umma pekee.

Alitaja jambo jingine ni kukosekana kwa chombo huru na cha kudumu kinachoratibu na kusimamia bei za huduma za afya, “Kwa kuzingatia changamoto hizo, kamati inaona ipo haja ya Serikali kutafuta ufumbuzi haraka.”

Akitoa majibu, Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu alitoa angalizo kwamba hawatafanya uamuzi bila kuzingatia tathmini ya uhai na uendelevu wa mfuko.

“Tumeunda timu ya watalaamu kutoka ndani na nje ya Serikali tutawaita sekta binafsi, tutawaelekeza. Bima ya afya ni namba kama itatuelekeza tutafanya uamuzi. Maazimio yote tumeyapokea,” alisema na kusisitiza;

“Bima ya afya kwa wote ndiyo mwarobaini, pamoja na wale wasiojiweza tulishawajumlisha tutatoa kwa wasio na uwezo asilimia 26 ya Watanzania.”

Pamoja na malalamiko ya watoa huduma, kupitia maboresho ya kitita cha mafao yaliyofanywa na NHIF, wananchi watanufaika kutokana na kuongezwa kwa huduma ambazo hazikuwepo.

Punguzo hilo lilihusisha wanufaika kuanza kupata huduma ya vifaa pandikizi, kupandikizwa viungo, upasuaji wa moyo, huduma za upasuaji kwa njia ya video/mtandao na vifaa bandia kupitia bima hiyo.

Fursa nyingine ya matibabu kwa wananchi ni kuongezwa kwa dawa 124 kwenye kitita cha mafao ya mfuko kutoka kwenye orodha ya dawa muhimu ya taifa.

Kundi lingine litakalonufaika na mabadiliko hayo ni watoa huduma za afya ambao wataongezewa motisha kuanzia ngazi ya afya ya msingi ambapo kumuona daktari ilikuwa Sh1,000 sasa inakwenda kuwa Sh2,000.

Licha ya manufaa kwa wanachama, Mwenyekiti wa chama cha watoa huduma za afya binafsi Tanzania (Aphta), Dk Egina Makwabe alisema mabadiliko hayo yataumiza sekta binafsi kwa kiwango kikubwa na uwezekezaji kwenye sekta ya afya utakuwa mgumu.

Dk Makwabe alisema ugumu utakuwepo katika ulipaji wa mishahara utakaoanza kuwa kizingiti kwao.


Nyongo aliitaka Serikali kuona umuhimu wa kutoifuta Taasisi ya Chakula na Lishe (TFNC) kwa sababu ni chombo mahususi kinachoshughulikia na kusimamia masuala yote ya lishe nchini.

Desemba mwaka jana, Serikali kupitia Msajili wa Hazina ilitangaza TFNC kuwa ni miongoni mwa taasisi zilizofutwa.

“Bunge linaazimia Serikali kuona umuhimu wa kutoifuta TFNC, kwani ni chombo mahususi kinachoshughulikia na kusimamia masuala yote ya lishe nchini,” alisema.


Lavalia njuga mfumuko wa bei

Akiwasilisha taarifa ya shughuli za Kamati wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara, Kilimo na Mifugo kwa mwaka 2023, Mwenyekiti wa kamati hiyo, Deodatus Mwanyika alipendekeza Bunge liazimie Serikali ifanye tathmini ya hali ya mfumuko wa bei.

Pia Bunge liazimie Serikali kuchukua hatua za haraka, ili kupunguza madhara yake katika uchumi na maisha ya watu.

Alisema mfumuko wa bei unaoendelea kwa sehemu kubwa unagusa bidhaa muhimu, zikiwemo za chakula kama vile sukari, ngano, mchele, mahindi, maharage na vitoweo (nyama, samaki).

Alisema bidhaa muhimu kwa maisha ya watu zinapoguswa na mfumko wa bei zinagharimu maisha ya mtu mmoja mmoja, jamii, uchumi wa taifa na ustawi wa watu kwa ujumla.

“Bunge liazimie Serikali ifanye tathmini ya hali ya mfumko wa bei nchini na kuchukua hatua za haraka ili kupunguza madhara yake katika uchumi na maisha ya watu na Serikali iweke mikakati ya muda mrefu ya kuzuia mfumko wa bei na kudhibiti madhara,” alisema Mwanyika.

Kuhusu upungufu wa sukari nchini, Mwanyika alilitaka Bunge liazimie Serikali ichukue hatua haraka, madhubuti na za kudumu kuhakikisha upatikanaji wa sukari ili kukidhi mahitaji.