Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Mabadiliko huduma Toto Afya Kadi bado hayajapoa

Dar es Salaam. Miongoni mwa matukio yaliyotikisa mwaka 2023, ni kifurushi cha bima ya watoto, ‘Toto Afya Kadi’ kusitishwa matumizi yake na Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF).

Toto Afya Kadi ilikuwa kifurushi ndani ya NHIF iliyotolewa kwa watoto chini ya miaka 18 wanaosajiliwa na mfuko huo ili kuwezesha matibabu kwa viwango vinavyostahili.

Hadi Machi mwaka huu, kifurushi hicho kilichoanzishwa mwaka 2016 tayari kilishatoa huduma za afya kwa watoto 210,664 walio chini ya miaka 18
Machi, 2023 NHIF kupitia Kitengo cha Mawasiliano kilitangaza kufanya maboresho ya utaratibu wa usajili na huduma kwa watoto waliokuwa wanasajiliwa kupitia utaratibu wa Bima ya Afya ya “Toto Afya Kadi”.

“Kwa sasa wazazi au walezi wanashauriwa kuwasajili watoto wao kama wategemezi wao kwenye bima ya afya au kuwasajili kipitia shule wanazosoma.
Taarifa hiyo ilifafanua kuwa,”Lengo ni kuongeza wigo wa wanachama katika mfumo wa bima ya afya kuelekea bima ya afya kwa wote na kuhakikisha wanachama katika makundi hayo wanajiunga kama familia au kaya au makundi ya wanafunzi kupitia shule wanazosoma,” ilielezwa.

Pia kupitia mabadiliko hayo, mzazi/mlezi alipewa uwezo kuandikisha mtoto kama mtegemezi kupitia bima zao kwa mwajiri au vifurushi vya Najali Afya, Wekeza Afya na Timiza Afya pamoja na wazazi wao.

Kwa kundi la watoto watakaokosa sifa na vigezo vya kuandikishwa kupitia bima za wazazi kwa mwajiri au vifurushi vya Najali Afya, Wekeza Afya na Timiza Afya taarifa hiyo ilieleza kuwa wanaweza kuandikishwa kupitia vyuo, shule au vituo rasmi vya kulelea watoto waishio katika mazingira magumu.

Akizungumzia mabadiliko ya Toto Afya kadi, Japhari Lesso, mkazi wa Kibaha, anasema kufanyika kwa mabadiliko ya kifurushi hicho, watoto wamekuwa wakitibiwa kwa shida.

“Kumtibu mtoto kwa fedha taslimu ni shida kubwa sana, ile ilikuwa inaturahisishia hata ukimuacha mtoto nyumbani na dada akipata homa gafla anaweza kukimbizwa hospitali na akapatiwa matibabu bila mzazi kuwepo, lakini sasa ni lazima awepo ili mtoto apatiwe huduma za afya,” anasema.

Anaeleza kuwa kwa mzazi anayefanya biashara ndogondogo kulipia fedha taslimu za matibabu ni maumivu, hivyo ili kunusuru maisha ya watoto ni muhimu kurudisha kifurushi hicho.

Anasema mama na mtoto ndio wanapaswa kuwa na huduma za afya za uhakika, hivyo Serikali iangalie huduma hiyo kwa jicho la kipekee.

Aisha Joseph, mkazi wa Kijiji cha Kibeye wilayani Chato Mkoa wa Geita anasema mabadiliko ya Toto Afya Kadi yana matokeo chanya na hasi, lakini kwake yalikuwa hasi zaidi.

Mabadiliko yameathiri baadhi ya watoto wasiokuwa na wazazi ambao kama wangekuwa na wazazi wangekatiwa bima na wazazi wao. “Sasa kama huna mzazi kupitia utaratibu mpya uliotolewa na NHIF sharti ni kwamba ni lazima hao watoto wajiunge na bima kupitia shule.

“Sasa ili wajiunge ni sharti wawe 100, asilimia kubwa ya shule watoto hawafiki 100, hivyo wanakosa huduma na akiumwa yupo hatarini kwa kuwa hana bima kutokana na utaratibu uliopo wa kupata bima.

“Tunapokwenda kuanza mwaka 2024, Serikali iliangalie hili kwa umakini, kuna watoto wengi wanaumia kwa kukosa huduma, ni muhimu kuangaliwe namna ya kuja na mifumo rafiki ili kunufaisha makundi hayo bila kubagua,” anashauri.
 

Maoni ya wadau

Mabadiliko hayo yaliibua maoni mbalimbali ya wadau ambapo Kituo cha Sheria ma Haki za binadamu (LHRC) kufuatia mabadiliko hayo kilisema kitendo NHIF kuondoa utaratibu wa watoto kupata huduma za afya kupitia Toto Afya Kadi ni kinyume cha Sheria ya mtoto.

“Taarifa ya NHIF haijaweka bayana kuwa huduma hiyo imesitishwa kwa muda gani, uamuzi huu ni kinyume cha kifungu cha 8 cha Sheria ya Mtoto No 21 ya 2009 kama ilivyofanyiwa marekebisho mwaka 2019 ibara ya 24 ya mkataba wa Kimataifa wa Haki za mtoto 1989 na ibara ya 14 ya mkatana wa Afrika wa haki na ustawi wa mtoto 1989,” iliandikwa kwenye taarifa ya LHRC.

Pamoja na LHRC kuungana na wadau wengine kupinga utaratibu huo wa Serikali, akiwasilisha bajeti yake ya mwaka 2023/24 Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu alisema sababu ya kusitishwa kwa kifurushi hicho ni tathmini iliyofanywa kwa huduma hiyo kuonyesha wazi kuwa kundi hilo lina matumizi makubwa na hivyo kutishia uhai na uendelevu wa mfuko huo endapo hatua hazitachukuliwa.

Kufikia mwaka 2020/21, Mfuko ulikuwa umesajili watoto 205,796 ambao michango yao ilikuwa ni Sh5.99 bilioni na matumizi yao ni Sh40.58 bilioni sawa na uwiano wa asilimia 677.

“Kutokana na tathmini hii, ni wazi kuwa kundi hili lina matumizi makubwa na hivyo kutishia uhai na uendelevu wa mfuko endapo hatua hazitachukuliwa,”alisema.
Pamoja na ufafanuzi huo, wadau wa afya, wazazi na walezi waliendelea kusisitiza Serikali isitishe maboresho hayo yanayowanyima fursa watoto huduma ya afya.
Kupitia mjadala uliofanywa mtandaoni na kampuni ya Mwananchi Septemba mwaka huu, Ummy aliwaomba wadau kutoa maoni kuboresha mfumo huo.

“Zipo sababu za msingi kwa nini NHIF wamebadilisha utaratibu wa kusajili watoto wanaojiunga na NHIF kwa hiari. Huwezi kuwa na bima inayokusanya Sh5 bilioni fedha inayolipwa kwa watoa huduma, yaani matumizi ni Sh40 bilioni!

Tanzania, watoto ni takribani milioni 31, watoto waliokatiwa Toto Afya Kadi ni kama laki mbili tu, hawajafika hata asilimia moja ya watoto wote nchini. Sasa leteni ushauri ni vipi NHIF wataweza kuvutia watoto wengi zaidi ambao hawana changamoto za kiafya kujiunga na bima ili pale watakapougua waweze kuchangiana,” aliandika Waziri Ummy.

Kilio cha Toto Afya Kadi mwarobaini wake ulitajwa kuwa ni ‘Bima ya Afya kwa Wote’ ambapo baada ya danadana ya muda mrefu baada ya kukwama mara mbili kujadiliwa katika Bunge la Tanzania.

Muswada wa sheria ya Bima ya Afya kwa Wote ulisomwa kwa mara ya pili Bungeni, ambapo Serikali kupitia Wizara ya Afya iliainisha marekebisho ambayo wabunge waliyahitaji.

Marekebisho hayo ni Serikali kuweka wazi vyanzo vya mapato katika safari ya kutunga sheria ya Muswada wa sheria namba 8 ya Bima ya Afya kwa Wote ambavyo ni kodi za vipodozi, kodi ya vyombo vya moto na vinywaji vikali.

Muswada huo ambao ulikwama kuwasilishwa mwaka jana kwa kilichoelezwa ni kukosekana kwa vyanzo halisi vya kugharamia matibabu ambapo kulikuwa na mvutano baina ya Serikali na Kamati ya Bunge.

Ikiwa ni mwezi mmoja tangu Bunge kupitisha muswada wa Sheria ya Bima ya Afya kwa Wote, Rais Samia Suluhu Hassan Desemba mosi mwaka huu ametia saini na kuwa sheria kamili.


Nini kinachofuata

Akizungumzia hatua hiyo, Rais wa Chama Cha Madaktari Tanzania (MAT) Dk Deusdedit Ndilanha anasema wanasubiri kauli ya Waziri Ummy kueleza ni lini utekelezaji unaanza.

“Mwenye mamlaka sasa ni waziri atuletee kanuni na kutupa muundo wa utumikaje utakuwaje, sisi wadau tunasubiri maelekezo.

“Tumesubiri hii hatua muda mrefu, ukiniuliza sasa nilitaraji uwe tayari ulishasainiwa sijui tulichelewa nini,”anasema.

Kwa upande wake, Ofisa Mtendaji Mkuu wa Chama cha watoa huduma za afya Tanzania (Aphta), Dk Samwel Ogilo anasema kwa sasa wanasubiri kanuni na wanaimani wadau wote watahusishwa.

“Wadau wote wahusishwe kwenye utengenezaji wa hizi kanuni ili zilete maendeleo chanya kwa nchi kwa ujumla, sisi kama sekta binafsi tunahitaji tuhusishwe tuwe na kanuni chanya ili kuyafikia malengo yaliyotarajiwa,”

Akitoa maoni yake, Rais wa Tanzania Health Summit, Dk Omary Chillo anasema kusainiwa kwa muswada huo nchi imefikia katika hatua nzuri kwa sababu bima ya afya ni msingi wa kuwapa wananchi afya njema.
Anasema baada ya hatua hiyo ni wadau kukaa na kuchambua vifurushi kulingana na vipato vya wananchi ili kila mtu awe na uwezo wa kuchangia.

“Huu ni mchakato utakuwa mrefu kwa maana kuangalia ni kwa kiasi gani watu watachangia, waliopo makazi ni rahisi kwa sababu wanapata mishahara, changamoto kubwa ni kwa wale ambao wanafanya shughuli zao za kila siku, kwa hiyo itachukua muda kujadili kwa kina

Dk Chillo aliongeza kuwa “Bado tuna kazi ndefu ya kufanya itakayoleta msuguano, lakini tutafika mbele na wananchi watachangia, pia kuongezwe elimu ya watu kuelewa bima ya afya ni nini kabla ya kuanza kuchangia,”anasema.