Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Sababu wanafunzi zaidi ya 200,000 kutofanya mitihani ya Taifa

Wanafunzi wakifanya mtihani. Picha kwa msaada wa Akili Bandia (AI)

Muktasari:

  • Matokeo ya mitihani ya kitaifa ya darasa la nne na kidato cha pili yametoka, zaidi ya wanafunzi 200,000 hawajafanya kutokana na sababu mbalimbali, Mwananchi Digital imechimba kwa kina sababu hizo na kushauri njia za kuondoa tatizo hilo...

Dar es Salaam. Matokeo ya mitihani ya kitaifa ya darasa la nne na kidato cha pili yaliyotangazwa leo Jumapili Januari 7, 2023 na Baraza la Mitihani la Tanzania (Necta) yameonyesha bado kuna wimbi kubwa la wanafunzi wanaokatisha masomo yao, huku sababu zikishindwa kubainishwa moja kwa moja.

Matokeo hayo ya mitihani ya upimaji wa kitaifa, yanaonyesha jumla ya wanafunzi 211,997 waliosajiliwa kufanya mitihani hiyo mwaka 2023, hawakufanya.

Akitangaza matokeo hayo Katibu Mtendaji wa Necta, Dk Said Mohamed amesema wanafunzi 1,693,444 walisajiliwa kufanya upimaji wa kitaifa wa darasa la nne, lakini kati ya hao 147,837 ambao ni sawa na asilimia 8.7 hawakufanya mtihani huo, wakiwemo wasichana 60,835 na wavulana 87,002.

Vivyo hivyo kwa kidato cha pili, wanafunzi 759,799 walisajiliwa kufanya mtihani wa upimaji, lakini 64,160 ambao ni sawa na asilimia 8.4 hawakufanya, wakiwemo wasichana 28,951 na wavulana 35,209.

Loading...

Loading...

Hata hivyo, amesema idadi hiyo ya wanafunzi wasiofanya mtihani licha ya kusajiliwa inaendelea kupungua mwaka hadi mwaka, kutokana na mwamko wa elimu kuongezeka ikilinganishwa na miaka ya nyuma.

“Tunaendelea kulifuatilia hili, ingawa ukweli ni kwamba idadi inapungua ikilinganishwa na miaka ya nyuma, sasa hivi kuna mwamko mkubwa wa elimu, lakini niseme kwamba tunalifuatilia na nitoe wito kwa mamlaka nyingine kuangalia kwa nini wanafunzi wanakatisha masomo.

“Dropouts (mdondoko) bado ipo na kuna sababu mbalimbali, hapa cha muhimu ni kuweka mkazo kwa jamii izidi kuona umuhimu wa elimu,” amesema Dk Mohamed.

Loading...

Loading...

Mwananchi Digital imezungumza na wadau wa elimu ambao wameshauri jamii na Serikali kuchukua hatua madhubuti kuhakikisha inaweka mazingira wezeshi yatakayosaidia kuondoa vikwazo na kutoa fursa kwa wanafunzi wahitimu katika ngazi zote wanazosajiliwa.

Akizungumzia hilo, Cathleen Sekwao amesema kukatisha masomo kwa wanafunzi si jambo la kupuuzwa kwa kuwa ni mwanzo wa kuangukia kwenye kundi la watu wazima wasiokuwa na elimu.

Amesema utoro, mimba na ajira za utotoni bado ni changamoto kubwa, hivyo ni muhimu kwa wazazi kushiriki kikamilifu kwenye malezi na usimamizi wa watoto katika ngazi zote za elimu, ikiwa ni pamoja na kuwaondoa katika mazingira hatarishi yanayoweza kuwashawishi kuangukia kwenye mtego huo.

“Hapa tunapozungumzia utoro jamii na Serikali pia ina sehemu yake ya kufanya kwa sababu inawezekana mtoto anaona hana sababu ya kwenda shule kama hakuna walimu au waliopo wachache wanalazimika kujigawa kwenye madarasa mengine.

“Endapo walimu watawekewa mazingira mazuri, ikiwemo nyumba karibu na shuleni itakuwa rahisi kwao kuwepo shuleni muda wote na hata kuwafuatilia watoto,” amesema Cathleen na kuongeza;

“Huko vijijini bado kuna watoto wanashawishika kwenda kufanya kazi kwenye mashamba au migodini kwa ajili ya kupata chochote kitu, sasa mtoto akishafikia hatua hii si ajabu kutoonekana siku ya mtihani. Kwa hiyo unaweza kukuta ni umaskini au tamaa ya kupata fedha.”

Loading...

Loading...

Hoja hiyo haikutofautiana na aliyotoa Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Dk Faraja Kristomus aliyesema hali hiyo inachangiwa na uwepo wa wazazi ambao hawaoni umuhimu wa elimu, hivyo kuwaacha watoto wawe na utoro sugu ambao hatima yake ni kukatisha masomo.

Hata hivyo, Dk Kristomus amekwenda mbele zaidi na kueleza kuwa lugha ya kufundishia imekuwa tatizo kwa baadhi ya wanafunzi wa sekondari, hivyo kufikia uamuzi wa kukatisha masomo na wengine kugeukia mafunzo ya ufundi.

“Hili suala la lugha ya kufundishia bado linawapa changamoto wanafunzi, ingawa hatutaki kuliona, mtoto amesoma kijijini amemaliza darasa la saba na kupata Kiingereza C au D anachaguliwa kwenda sekondari, huko anakuta hilo somo lililomsumbua ndiyo lugha inayotumika kufundishia masomo yote, atajaribu kujifunza, akiona haelewi anaona bora aache shule.

“Kuna wengine wanawaambia wazazi wao kuliko kupoteza miaka minne sekondari, ni heri ajifunze kitu kingine na hili nimelishuhudia, watoto wanatoka sekondari wanakwenda kujifunza ufundi kwa sababu anaona anaweza kumaliza na akaambulia sifuri, hivyo bora apate ujuzi,” amesema Dk Kristomus.

Mhadhiri huyo ameshauri ifike wakati Serikali iliangalie kwa umakini suala la lugha ya kufundishia kwa kuboresha ufundishaji wa somo la Kiingereza kwa shule za msingi, ikiwa ni pamoja na kuboresha uandaaji wa walimu wa somo hilo, ili wafundishe katika viwango vinavyostahili kusiwe na changamoto sekondari.

Mbadala wa hilo ni kutoa uhuru kwa wanafunzi kuchagua lugha wanayoimudu ili kufanyia mtihani.


Wanafunzi wakifanya mtihani. Picha na Maktaba

Ufaulu waongezeka

Akizungumzia matokeo ya darasa la nne, Dk Mohamed amesema asilimia 83.34 ya waliofanya mtihani huo wamefaulu kwa kupata madaraja A hadi D, ikiwa ni ongezeko la asilimia 0.39 ikilinganishwa na mwaka 2022 ambapo ufaulu ulikuwa asilimia 82.95.

Matokeo hayo yanaonyesha wanafunzi 257,396, sawa na asilimia 16.66 wamefeli na wanatakiwa kurudia darasa kabla ya kufanya mtihani huo kwa mara nyingine.

Kwenye upande wa masomo ufaulu wa somo la Kiswahili ni asilimia 84.15, ikiwa ni ongezeko la asilimia 0.96 ikilinganishwa na matokeo ya mwaka 2022, Kiingereza asilimia 72.5, ikiwa ni ongezeko la asilimia 0.82.

Ufaulu kwenye somo la maarifa ya jamii ni asilimia 86.75, uraia na maadili asilimia 85.52, sayansi na teknolojia asilimia 86.86 na hisabati asilimia 54.00, ikiwa ni ongezeko la asilimia 4.30 ikilinganishwa na mwaka 2022.

Katika matokeo ya kidato cha pili, wanafunzi 592,741 ambao ni sawa na asilimia 85.31 wamefaulu kwa daraja la kwanza hadi la nne.

“Ufaulu huu ni ongezeko la asilimia 0.13 pamoja na ongezeko la idadi ya wanafunzi 53,096, sawa na asilimia 9.84 ya waliopata fursa ya kuendelea na kidato cha tatu ikilinganishwa na mwaka 2022.”

Upande wa masomo matokeo hayo yanaonyesha ufaulu wa somo la hstoria ni asilimia 50.71, jiografia asilimia 53.78, uraia asilimia 48.27 ikiwa ni ongezeko la asilimia 17.15 ikilinganishwa na mwaka 2022 ambapo ufaulu katika somo hilo ulikuwa asilimia 31.12.

Ufaulu wa masomo ya biashara umetajwa kuwa ni wastani ambapo commerce ni asilimia 50.28, ikiwa ni ongezeko la asilimia 0.01 na book keeping ni asilimia 52.84, ikiwa ni ongezeko la asilimia 1.36.

Mambo yameendelea kuwa mazuri kwenye masomo ya lugha ambapo ufaulu wa Kiswahili ni asilimia 95.18, Kichina asilimia 93.39, Kiingereza asilimia 68.27, Kifaransa asilimia 55.61 na Kiarabu asilimia 48.72.

Masomo ya fizikia, kemia, kilimo na hesabu yana ufaulu ulio chini ya wastani, ni kati ya asilimia 19.06 hadi asilimia 39.23. Hata hivyo, ufaulu wa fizikia, hesabu na kilimo umepanda kati ya asilimia 0.85 hadi asilimia 4.52, huku ufaulu wa somo la kemia ukishuka kwa asilimia 5 ikilinganishwa na mwaka jana.

Hata hivyo, katibu mtendaji huyo alibainisha kuwa Necta imefuta matokeo kwa wanafunzi 178 wa darasa la nne na 28 wa kidato cha pili kwa kufanya udanganyifu kwenye mitihani hiyo, huku wengine 17 ni kwa kuandika lugha chafu kwenye mitihani yao.