Prime
Waliofeli darasa la saba wafanye kazi hizi

Muktasari:
- Wadau wa elimu wameshauri ajira salama kwa wanafunzi waliofeli darasa la saba kutokana na kushindwa kutambulika katika mfumo rasmi wa elimu
Dar es Salaam. Wakati jamii ikiwa kwenye maswali juu ya kazi gani wanazoweza kufanya waliofeli darasa la saba, wadau wa elimu wameeleza namna ya kuwakwamua.
Wadau hao wamesema kazi nyepesi za ujuzi ni suluhu ya ajira kwa wahitimu wa darasa la saba waliofeli mtihani wa Taifa na kushindwa kuchaguliwa katika ngazi ya sekondari.
Maoni ya wadau hao wameyatoa mitandaoni baada ya Mwananchi Digital, kuchapisha habari iliyohoji darasa la saba waliofeli wanaenda wapi na wanafanya nini?
Makala hiyo ilionyesha zaidi ya wahitimu 600,000 wa ngazi hiyo kwa miaka mitatu kuanzia 2021 hadi 2023 walifeli na kushindwa kujiunga na kidato cha kwanza huku baadhi yao wakigeuka kuwa watoto wa mtaani.
Kamishna wa Elimu wa Wizara ya Elimu, Dk Lyabwene Mtahabwa alisema kwa sasa hakuna mfumo rasmi wa kuendelea na wanafunzi waliofeli darasa la saba, zaidi ya masomo ya ufundi stadi.
“Kwa sasa hatuna mafunzo labda tutafute njia mbadala, lakini kuna njia nyingi kwa waliopata chini ya alama hizo (A hadi C) ikiwamo mafunzo ya ufundi stadi yanayotolewa na Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi nchini,” alisema.
Akichangia mada hiyo katika mtandao wa Instagram @sonsoge_tz anasema kazi zinazoweza kufanywa na aliyefeli darasa la saba ni nyepesi zinazohitaji ujuzi au maelekezo na usimamizi zikiwemo kazi za ndani na ufugaji.
“Wengi wanaofeli wanaenda kufanya kazi za ndani, kuchunga mifugo, wanakuwa wajasiriamali pia kuna fursa katika kuosha magari japokuwa wasipoonyeshwa fursa hizi baadhi wanakuwa vibaka au kwa wasichana wanaolewa,”anasema.
Naye Esther Sinodya kupitia mtandao wa Instagram amesema licha ya uwepo wa vyuo vya ufundi stadi lakini ujasiriamali ni njia bora ambayo itasaidia kuleta tija kwa Taifa miongoni mwa waliofeli darasa la saba.
“Baadhi yao huenda kuanzisha miradi baada ya kujifunza ujasiriamali na wakiimudu wanawaajiri hata waliosoma, kufeli mtihani si kufeli maisha,”ameandika.
Siwema Rajabu, mkazi wa Wilaya ya Nachingwea mkoani Lindi ambaye ni mwanachama wa kikundi cha ujasiriamali cha ushindi amesema baada ya kufeli darasa la saba 2013 alitafuta ujuzi ambao utamfanya aingize kipato.
“Nilifeli darasa la saba 2013, sikukata tamaa nilianza kujifunza kazi za mikono kama kutengeneza nguo za batiki na kujifunza kushona.
“Haikuwa rahisi kwangu mpaka nilipojiunga na kikundi cha wajasiriamali cha ushindi ambacho nikaongeza ujuzi mwingine wa kutengeneza sabuni na sasa hivi nauza bidhaa zangu ambazo zinaniendeshea maisha,”amesema Siwema.
Kazi zenye fedha nyingi
Wakati wadau wakizitaja kazi hizo, tovuti ya ajira ya kimataifa ya ‘indeed’ imeziorodhesha kazi tano zinazoingiza fedha nyingi katika wastani wa kimataifa zinazoweza kufanywa na mtu asiye na elimu.
Tovuti ya ‘indeed’ imeitaja kazi ya ulinzi kuwa na wastani mzuri wa malipo katika soko la ajira la dunia kwa wastani wa Dola 13.92 kwa saa (Sh34,800), ikifuatiwa na mhudumu wa shamba ambayo ni Dola 13.25 (Sh33,125) na msaidizi wa ndani anapaswa kulipwa Dola 12.9 (Sh32,250).
Kazi nyingine ni udereva wa malori ya mizigo mshahara wake ni Dola 12.59 (Sh31,475) na wafanya usafi ambao mshahara wao ni Dola 12.09 (Sh30,225)
Miradi ya kazi hizo zilizotajwa na tovuti ya ‘indeed’ pia imetajwa kutoa ajira nyingi kwa Watanzania mwaka 2022 katika ripoti ya ‘Tanzania in figures 2022’ inayotolewa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS).
“Wafanyakazi wa ndani (hoteli, majumbani) jumla ya ajira 1,109 zilitengenezwa, usafirishaji (magari ya mizigo ikiwemo) ilizalisha ajira 9,838, miradi ya kilimo jumla ya ajira 3,199 na miradi ya utoaji huduma (ulinzi ukiwemo) ilitoa ajira 1,271.
Pia, Ripoti ya Utafiti wa watu wenye uwezo wa kufanya kazi 2020/21 iliyotolewa na NBS inaonyesha ukosefu wa ajira kwa watu wenye elimu ya darasa la saba umepungua kwa asilimia 1.2.
“Mwaka 2014 ukosefu wa ajira kwa wenye elimu ya darasa la saba ilikuwa asilimia 10 huku ikishuka hadi asilimia 8.8 mwaka 2020/21,”inasema ripoti hiyo.
Isemavyo sheria
Wakati ajira kwa waliofeli darasa la saba zikiainishwa na idadi ya wanaokosa ajira ikizidi kupungua siku hadi siku bado Sheria ya ajira na mahusiano kazini ya mwaka 2004 inakataza ajira kwa watoto chini ya miaka 14 huku ikitoa mazingira mahususi ya kuajiri jambo ambalo linaleta ukakasi kwa waliofeli darasa la saba ambao wengi ni chini ya umri huo.
“Hakuna mtu anayeruhusiwa kumuajiri mtoto mwenye umri chini ya miaka kumi na nne.
“Mtoto mwenye umri wa miaka kumi na nne anaweza kuajiriwa kufanya kazi nyepesi tu, ambazo haziwezi kuwa na madhara kwa afya ya mtoto na maendelo yake; na hazimzuii mtoto kuhudhuria masomo shuleni, kushiriki kwenye ufundi stadi au miradi ya mafunzo iliyothibitishwa na mamlaka yenye madaraka au uwezo wa mtoto kufaidi maelekezo anayoyapata.
“Mtoto mwenye umri chini ya miaka kumi na nane haruhusiwi kuajiriwa kwenye mgodi, kiwanda au kama kufanya kazi katika meli au katika sehemu nyingine za kazi ikijumuisha ajira isiyo maalumu na kilimo, kwenye mazingira ya kazi ambayo Waziri anaweza kuona ni hatarishi. Kwa madhumuni ya kifungu kidogo hiki, “meli” inajumuisha chombo cha aina yoyote kinachotumika kwa usafiri wa maji,”inasema Sheria hiyo katika sehemu ya II, Sehemu Ndogo A inayohusu ajira kwa watoto.
Takwimu za ajira
Wakati takwimu zikionyesha watu wenye elimu ya darasa la saba ukosefu wa ajira unapungua pia ripoti ya Tanzania in figures 2022 ya NBS inaonyesha hali hiyo katika soko la ajira Tanzania kwa ujumla.
“Mwaka 2018 ukosefu wa ajira ulikuwa asilimia 9.7 hali hiyo ilishuka hadi asilimia 9.6 mwaka 2019 na kushuka zaidi mwaka 2020 hadi asilimia 9.5.
“Pia, mwaka 2021 kiwango cha ukosefu wa ajira kilizidi kushuka zaidi na kufikia asilimia tisa na 2022 kilifikia asilimia 8.9,”inasema ripoti hiyo.
Kwa upande wa takwimu za ajira, hali ya upatikanaji wake imeongezeka kwa asilimia 9.5 mwaka 2022 ikilinganishwa na mwaka 2018.
“Hadi mwaka 2018 jumla ya watu milioni 21.98 walio na umri zaidi ya miaka 15 waliajiriwa katika kazi mbalimbali huku mwaka 2022 wakiongezeka hadi kufikia milioni 24.07,”imesema ripoti hiyo inayotolewa na NBS.
Kwa upande wake, Mchumi Mack Patrick anasema kupungua kwa wasiokuwa na ajira ni ishara ya kuimarika kwa uchumi na mzunguko wa fedha.
“Kila mtu anafanya kazi ilia pate mshahara ambayo mara nyingi ni fedha, ina maana kama idadi ya wenye kazi inaongezeka basi hata mzunguko wa fedha unaongezeka.
“Hii ina athari chanya katika uchumi wa nchi na mtu mmoja mmoja, pengine itakuja kuonekana katika Pato la Taifa,”amesema Patrick.
Patrick amesema kundi la walioishia darasa la saba lina umuhimu mkubwa katika uzalishaji mali kwasababu aina ya kazi wanazofanya ni za ujuzi zaidi.
“Kuna kazi mtu wa darasa la saba anaweza kuifanya vizuri zaidi kutokana na ujuzi na kipaji ambayo hata mtu mwenye digrii anaweza asiifanye, kwahiyo hapa unaona umuhimu wa kundi hili katika uchumi,” alisema.
Hata hivyo, bado uhitaji wa watu hawa ni mkubwa ndio maana asilimia 10 ya wafanyakazi wa nchi za GCC (Bahrain, Kuwait, Oman, Qatar, Saudi Arabia, and the United Arab Emirates) ni wasio na elimu na mara nyingi hutoka nchi nyingine.
Wadau wa mitandaoni