Ripoti ya utafiti watu wenye ulemavu kuzinduliwa Desemba Zanzibar

Viongozi na wadau walioshiriki kwenye kikao cha ripoti ya utafiti wa watu wenye ulemavu
Muktasari:
- Zanzibar kufanya maadhimisho ya Siku ya Walemavu siku hiyo kutakuwa na uzinduzi wa ripoti ya utafiti ya watetezi wa watu wenye ulemavu ulioandaliwa na THRDC kwa kushirikiana na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.
Dar es Salaam. Kuelekea kwenye maadhimisho ya Siku ya Walemavu Zanzibar Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu (THRDC) wamekutana na wadau mbalimbali lengo ni kufahamu changamoto zinazowakabili kwa pande zote mbili za Muungano wa Tanzania.
Ripoti ya utafiti huo ikishakamilika itazinduliwa kwenye maadhimisho ya siku ya walemavu Zanzibar yatakayofanyika Desemba ambapo mgeni rasmi anatarajiwa kuwa Rais Hussein Ali Mwinyi.
Hayo yamesemwa jijini Dar es Salaam leo, Jumanne Novemba 14, 2023 na Mratibu Taifa wa THRDC, Onesmo Olengurumwa amesema kumekuwa na changamoto nyingi zinazowakabili watetezi wa walemavu na kushindwa kutekeleza majukumu yao ipasavyo hivyo ripoti za utafiti zitasidia kujua njia za kutatua.
"Ikiwa watetezi wa walemavu wana changamoto inakuaje kwa walemavu wenyewe? Hivyo tumeona tuangalie kile kinachosumbua taasisi ili kupata nafuu ya kuweza kuwasaidia wanaowatetea," amesema Olengurumwa.
Amesema walemavu wanakabiliwa na changamoto nyingi ikiwepo masuala ya afya,elimu na uchumi ambapo wamekuwa wakilalamika kutengwa katika jamii kuwepo kwa sera inayosimamia masuala hayo itasaidia kufanya kazi kwa weledi.
Olengurumwa amesema kuna sheria ambazo zimewekwa na Serikali lakini hazifuatwi na kusababisha ugumu wa kazi kwa watu wenye ulemavu hivyo wanaona kuna haja ya kufanyia marekebisho ili zifuatiliwe.
Pia, amesema ukata wa fedha kwa taasisi za walemavu ni chanzo cha kutofanyika kazi zinazokusudiwa licha ya kuwepo kwa wafadhili ambao wanatoa fedha lakini haziwafikii walengwa.
Katibu Mtendaji Baraza la Taifa Watu wenye Ulemavu, Husi khamis Dede amesema ripoti itakayotolewa itasaidia Serikali kuona changamoto na kuweza kuzifanyia kazi.
"Zanzibar kuna sheria mpya ambayo imeundwa mwishoni mwa mwaka 2022 kwa ajili ya watu wenye ulemavu, kuna Baraza la Walemavu lipo chini ya Serikali yanafanyika yote haya kwa ajili kukabiliana na changamoto za walemavu tunategemea ripoti itatupa matokeo chanya," amesema Debe.
Amesema kutokana na umuhimu wa watu wenye ulemavu Serikali ya Zanzibar wametengeneza shule mbili za watu wenye ulemavu ambazo zimeingia kwenye historia tangu kupatikana kwa uhuru.
Debe amesema Serikali ya Zanzibar imeanzisha mfuko wa maendeleo ya uchumi ili kuwasaidia wananchi kukabiliana na changamoto za kiuchumi na mfuko huo unatoa kipaumbele kwa watu wenye ulemavu.
Ofisa Mkuu wa Ustawi wa Jamii, Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi, Vijana na Watu wenye Ulemavu, Joy Maongezi amesema Ripoti ya Utafiti ya Tathimini ya Watu wenye Ulemavu wataitumia kwa ajili ya kupitia sera, sheria na miongozo ya zamani na kuandaa mipya.
"Bila kufanya tafiti hatuwezi kupata takwimu sahihi ili kufanya kazi hivyo kupitia ripoti hiyo, itatusaidia kuona kwa namna gani tunaweza kufanya majukumu yetu kwa usahihi katika kukabiliana na changamoto za walemavu," amesema Maongezi.
Maongezi amesema Serikali imekuwa ikipingana na tabia ya watu kuwatumia walemavu kujipatia kipato, hivyo kuna haja ya kuandaa sheria itakayosaidia kukabiliana na jambo hilo.
Naye, Ernest Kimaya ambaye ni Mwenyekiti wa Shirikisho la Watu wenye Ulemavu Tanzania amesema nafasi waliyopewa kupitia utafiti uliyofanywa itawasaidia kuboreshwa kwa haki za watu wenye ulemavu ikiwepo sera, sheria na miongozo.
"Tafiti iliyofanywa imelenga kila sekta ambayo kila mmoja anatamani tuwe kwenye haki na hii itakwenda kusaidia kuona umuhimu wetu katika Taifa,"amesema.
Kimaya amesema utekelezaji wa miongozo imekuwa migumu kwa watendaji wa serikali kwa watu wa chini, maana viongozi wa juu wote wanatoa ushirikiano na kushiriki katika uandaaji wa sera mbalimbali.