Walalama uhaba wa maji kuvunja ndoa zao, Serikali yatoa mwongozo

Mkuu wa Wilaya ya Sumbawanga wakati akizungumza na wananchi wa Kijiji cha Mkowe.
Muktasari:
- Inaelezwa kuwa wanawake hulazimika kutembea umbali mrefu kutafuta maji tangu enzi za uhuru hadi sasa.
Rukwa. Wananchi wa Kijiji cha Mkowe, kata ya Miangalua, Wilaya ya Sumbawanga Vijijini, mkoani Rukwa, wamemuomba mkuu wa wilaya hiyo kuwasaidia kupata huduma ya maji safi na salama ili kuokoa ndoa zao.
Wakizungumza leo Jumatatu Aprili 28, 2025, wakati wa hafla ya uwekaji wa jiwe la msingi katika shule shikizi yenye vyumba viwili vya madarasa, wananchi hao wamesema ukosefu wa maji umechangia migogoro ya ndoa kutokana na wanawake kuchelewa kurudi nyumbani, wakiwa wanatafuta maji kutoka visima visivyo salama na vilivyo mbali.
Mwenyekiti wa Kijiji, Patrick James amesema wanawake hutumia muda mwingi kutafuta maji, hali inayochochea migogoro ya kifamilia. Sambamba na hilo, James amesema ofisi yake inapokea malalamiko pia ya umbali wa shule.
Amesema, “wanafunzi walikuwa wanatembea umbali wa zaidi ya kilomita 10 kwenda shule, hali iliyowakwamisha kielimu.”
Naye Godfrey Mwananzumi akizungumza na Mwananchi amesema mazingira hayo yalimkatisha tamaa na kuathiri ndoto za vijana wengi kijijini hapo.
Amesema wananchi waliungana kujenga shule shikizi kwa kushirikiana na Serikali ili kupunguza changamoto hiyo.
“Hii shule shikizi imetusaidia kumaliza changamoto moja ya umbali wa shule, lakini bado hii ya maji, wanawake hawaaminiwi na waume zao, ndoa zinavunjika, tunaomba mtusaidie,” amesema.
Hata hivyo, Mkuu wa Wilaya, Nyakia Chirukile amewahakikishia wananchi kuwa Serikali imejipanga kupeleka huduma muhimu ikiwemo ya maji na elimu katika eneo hilo.
Amesisitiza umuhimu wa kuwapeleka watoto wote shuleni na kuonya dhidi ya kuwatumia watoto wa kike kama vitega uchumi.
Ameahidi kushughulikia haraka changamoto ya maji kwa kushirikiana na wataalamu wa Ruwasa.