Ridhiwani Kikwete amshukuru Mkapa kumlipia ada

Waziri wa Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Ridhiwani Kikwete.

Muktasari:

  • Wahitimu 7,394 wametunukiwa shahada, stashahada na astashahada katika Chuo Kikuu cha Dodoma (Udom) akiwemo Mbunge wa Chalinze, Ridhiwan Kikwete.

Dodoma. Naibu Waziri katika Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Ridhiwan Kikwete amemshukuru Rais mstaafu hayati  Benjamin Mkapa kwa kumshawishi na kumlipia ada ya kusoma katika Chuo Kikuu cha Dodoma (Udom).

Hayati Benjamin Mkapa alifariki dunia usiku wa kuamkia Julai 24, 2020 kutokana na maradhi yaliyokuwa yakimsumbua.

Ridhiwan ambaye ni miongoni mwa wahitimu 7,394 waliotunukiwa astashahada, stashahada na shahada mbalimbali leo Ijumaa Desemba Mosi 2023, alitunukiwa shahada ya Uzamili ya Mahusiano ya Kimataifa kwenye mahafali ya 14 ya chuo hicho.

Wahitimu hao walitunukiwa shahada zao na Kaimu Mkuu wa Chuo hicho, Waziri Mkuu mstaafu Mizengo Pinda kwa niaba ya Mkuu wa Udom, Dk Stergomena Tax ambaye hata hivyo haikuelezwa sababu za kutokuwepo kwake.

Akizungumza baada ya kutunukiwa shahada hiyo, Ridhiwan pamoja na kumshukuru Mungu kwa hatua hiyo, amemshukuru Rais Mkapa kwa kumsukuma kusoma shahada ya pili.

“Yeye alinikuta bungeni pale, akaniuliza nafanya shughuli gani, nikamwambia zaidi ya shughuli za kibunge sina nyingine ninayofanya.

“Akanishawishi kusoma na hata ada ya kuja kusoma hapa yeye ndiye aliyenilipia nguvu ya kumshukuru Mungu bila yeye nisingekuwa nayo,”amesema.

Ridiwan ambaye pia ni Mbunge wa Chalinze amewashukuru wahadhiri kwa kumpa moyo wakati ambapo alitaka kusitisha masomo kwa sababu ya shughuli nyingi alizonazo.

 Amesema katika shahada yake hiyo, alifanya utafiti kuhusu mgogoro wa Burundi ambapo aligundua mambo mengi ambayo asingetamani Tanzania ifikie huko.

Awali Mwenyekiti wa Baraza la chuo hicho, Profesa Rweikiza Mukandala amesema pamoja na mafanikio yaliyopatikana, bado kuna changamoto ambazo wanaendelea kuzipatia ufumbuzi kuwezesha kuendelea na utoaji wa elimu bora.

Amezitaja baadhi ya changamoto ni upungufu wa maji, fedha za kusomesha wanataaluma na upungufu wa miundombinu ya ujifunzaji na ufundishaji.

“Tunaomba Serikali na wadau wengine wa maendeleo kuendelea kushirikiana nasi katika utatuzi wa changamoto hizo ili kuendelea kutoa elimu iliyo bora,”amesema.

Profesa Mukandala amewaasa wahitimu wa chuo hicho kujiendeleza kitaaluma na changamoto watakazokutana nazo wazitumie kama fursa ya kuwaletea maendeleo maishani mwao, na kuepuka tabia mbaya zisizoakisi mila na desturi za Watanzania.

Naye Makamu Mkuu wa Udom, Profesa Lughano Kusiluka amesema wanafunzi wanapofika katika chuo hicho wanajitahidi sana kuwaasa wazingatie masomo yao, kwani  kusoma chuo kikuu siyo lelemama, wafanye juhudi ili watoke na taji.

“Tunawaambia wakichezacheza watatoka bila taji. Lakini kama wazazi tunasikitika sana watoto ambao wamefanya vizuri kwenye ngazi za mwanzo wanafika chuo wakiwa na matarajio,  lakini wengine wanashindwa kumaliza masomo, wengine wanasuasua kwa kweli jambo hili si la chuo pekee,”amesema.

Amewaomba wazazi na walezi kushiriki na kuendelea kuwakumbusha muda wa chuo kikuu ni mdogo hivyo waendelee kufanya vizuri, ili uwekezaji wa Taifa na wao (wazazi) uwe na faida.

Aidha, amesema chuo hicho kimewadahili wanafunzi 13,042 kwa mwaka huu na shughuli hiyo itakapokamilika itawezesha chuo hicho kuwa na wanafunzi 35,000.

Pia amesema wamepokea maelekezo kuwa wanatakiwa kujenga kampasi ya chuo hicho mkoani Njombe ikiwa ni jitihada za Serikali kueneza elimu.