RC Chalamila arejea onyo kwa wanaoutamani urais

Askofu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheli Tanzania (KKKT) Dayosisi ya Karagwe, Dk Benson Bagonza (aliyevaa kanzu katikati) akimkabidhi zawadi Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Albert Chalamila wakati wa mkutano mkuu wa 23 wa Dayosisi hiyo iliyofanyika eneo la Murongo mpakani mwa Tanzania na Uganda. Anayeshuhudia kwa kupiga makofi ni Mkuu wa Wilaya ya Kyerwa, Rashid Maimu.
Muktasari:
Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Albert Chalamila amerejea kusisitiza kauli ya kuwataka wateule wa Rais Samia Suluhu Hassan kuacha kutamani nafasi ya aliyewateuwa, badala yake, watimize wajibu katika majukumu waliyopewa.
Kyerwa. Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Albert Chalamila amerejea kusisitiza kauli ya kuwataka wateule wa Rais Samia Suluhu Hassan kuacha kutamani nafasi ya aliyewateuwa, badala yake, watimize wajibu katika majukumu waliyopewa.
Akizungumza wakati wa mkutano mkuu wa 23 wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheli Tanzania (KKKT) Dayosisi ya Karagwe, Chalamila amesema siyo vizuri na ni tabia mbaya mtu kutamani nafasi ya aliyemteuwa au kumwekea mikono kuwa katika nafasi aliyonayo.
Hii ni mara pili Chalamila anatoa kauli hiyo baada ya kufanya hivyo mwezi ulipozungumza na waumini wa KKKT Kanisa la Lukajange mjini Kayanga yaliko makao makuu ya Wilaya ya Karagwe.
Huku akishangiliwa na wajumbe wa mkuyano huo uliofanyika kijiji cha Murongo, Wilaya ya Kyerwa mkoani Kagera na kuongozwa na Askofu wa Dayosisi hiyo, Dk Benson Bagonza, mkuu huyo wa mkoa amesisitiza kurejea kauli hiyo kila wakati kwa sababu huo ndio ukweli anaouamini.
Chalamila ametumia fursa hiyo kuwasihi Watanzania kila mtu kwa nafasi, eneo na imani yake kujenga tabia na hulka ya kusema ukweli na kushauri kwa uwazi badala ya kufanya unafiki katika mambo ya msingi.
"Tusiwe kama wajumbe wa mikutano ya uchaguzi wanaowanyima kura wagombea na baadaye kujitokeza kumpa pole nyingi kuliko idadi ya kura alizopata," amesema Chalamila
Akizungumzia nafasi ya madhehebu ya dini katika ulinzi wa amani, usalama na ustawi wa jamii, mkuu huyo wa mkoa amesema Serikali inatambua na kuthamini ushiriki wa taasisi za dini katika miradi ya elimu, afya na maji na kuomba ushirikiano huo uendelee.
Kauli hiyo imeungwa mkono na Mkuu wa Wilaya ya Kyerwa, Rashid Maimu akiupongeza uongozi wa KKKT Dayosisi ya Karagwe kwa kuwekeza katika ujenzi na uendeshaji wa Zahanati, Vituo vya Afya na Hospitali Teule ya Nyakahanga inayotumika kama Hospitali ya Rufaa kwa Wilaya ya Kyerwa.
Kwa upande wake, Askofu Bagonza ameihakikishia Serikali utayari na ushiriki wa Dayosisi ya Karagwe katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo kwa faida ya jamii.
Pamoja sekta ya afya, Dayosisi ya Karagwe pia imewekeza katika sekta ya elimu kwa kujenga na kuendesha shule z msingi, sekondari na vyuo vya ufundi na maendeleo ya jamii.