Prime
Zijue sababu zinazokufanya uishiwe fedha

Katika maisha ya kila siku, changamoto ya kuishiwa fedha ni jambo la kawaida na linaweza kumpata mtu yeyote, bila kujali kipato au nafasi yake katika jamii. Watu wengi wamejikuta katika hali ya kukosa fedha za kutosha kwa ajili ya mahitaji yao ya msingi au malengo yao ya muda mrefu. Sababu za hali hii ni nyingi na zinatofautiana kati ya mtu na mtu. Kuna sababu kadhaa, nitaainisha chache.
Kwanza kabisa, kutokuwa na bajeti ya matumizi ni sababu kubwa inayosababisha watu wengi kuishiwa fedha. Bila kupanga matumizi, mtu anaweza kutumia fedha zake hovyo bila kujua kiasi gani kinapaswa kutumika na kiasi gani kinapaswa kubaki.
Hali hii husababisha matumizi yasiyopangwa na mwisho kwenye kipindi ambacho anahitaji fedha kwa ajili ya malipo fulani muhimu anajikuta hana fedha. Ni rahisi kukosa nidhamu ya matumizi na kutumia fedha hovyo kwenye starehe, sherehe, au vitu visivyo na umuhimu iwapo hutakuwa na bajeti. Ni rahisi pia kununua kwa kushawishika na matangazo, kutoa misaada kwa watu mbalimbali wakati hujapangilia.
Kutokufanya kazi, kuishi kwa kubahatisha kama kutumia fedha kwenye kamari na michezo mingine ya kubashiri au kutegemea chanzo kimoja cha mapato. Usipofanya kazi kwa ufanisi na kwa moyo wako wote usitegemee malipo. Endapo una chanzo kimoja cha mapato, iwapo kitayumba au kukoma, unajikuta huna njia nyingine ya kupata fedha na hivyo kuishiwa kabisa.
Kutoweka akiba. Watu wengi hawana utaratibu wa kuweka akiba kwa ajili ya dharura au malengo ya baadaye. Hii inamaanisha kwamba linapotokea jambo la ghafla kama ugonjwa, ajali, au uharibifu wa mali, mtu analazimika kutumia fedha zote alizonazo au hata kukopa, na hivyo kujikuta ameishiwa kabisa.
Kukopesha wengine bila mpango ni chanzo kingine cha kuishiwa fedha. Mara nyingi, watu hutoa mikopo kwa ndugu, marafiki, au wafanyakazi wenzao bila kuzingatia uwezo wao wa kurejesha. Kutoa mikopo inaweza kukufanya ukajisikia vizuri na kuonekana mwema, lakini kukopesha ni taaluma. Mara nyingi fedha za kukopeshana marafiki na ndugu hazirudi kabisa, na mkopeshaji anajikuta hana fedha za kujikimu.
Kununua vitu feki au visivyo na ubora hupelekea mtu kutumia fedha mara kwa mara kufanya matengenezo au kununua upya. Hii ni hasara isiyoonekana moja kwa moja, lakini kwa muda mrefu huathiri hali ya kifedha ya mtu. Ni vizuri kuwa makini kwenye manunuzi ya vitu, hasa vya kielektroniki na vya matumizi ya kila siku.
Kupata majanga yasiyotarajiwa kama ugonjwa, ajali, au uharibifu wa mali, ni sababu nyingine inayoweza kumfanya mtu aishiwe fedha. Matukio haya yanahitaji matumizi ya haraka na makubwa ambayo hayakuwa yamepangwa.
Kuchelewa kulipwa haki zako kama mshahara, malipo ya biashara, au fidia, kunaweza kukufanya ukose fedha za matumizi ya kila siku na hivyo kujikuta umeishiwa.
Kukosa elimu ya fedha ni sababu ya msingi inayosababisha watu wengi kushindwa kupanga na kutumia fedha zao kwa ufanisi. Bila uelewa wa masuala ya fedha, mtu anaweza kufanya maamuzi mabaya ya kifedha na kujikuta ameishiwa.
Kwa ujumla, sababu za kuishiwa fedha ni nyingi na zinatokana na tabia, mazingira, na matukio mbalimbali. Kila mtu anapaswa kutambua sababu hizi ili aweze kuchukua tahadhari na kujiepusha na hali ya kuishiwa fedha mara kwa mara. Hata hivyo, ni muhimu kukumbuka kwamba nyakati ngumu za kuishiwa fedha huwa hazidumu kama ukiwa na mipango thabiti ya kifedha.