Rais Samia aomba mjadala changamoto bunifu sekta ya afya

Rais Samia Suluhu Hassan ahutubia katika Mkutano wa Ubunifu wa Afya Duniani (WISH), Doha nchini Qatar.

Muktasari:

Rais Samia Suluhu Hassan ameziomba Jumuiya ya Kimataifa kujadili changamoto tatu zinazorudisha nyuma juhudi za kufanya bunifu kwenye sekta ya afya

Dar es Salaam. Rais Samia Suluhu Hassan ameziomba Jumuiya ya Kimataifa kujadili changamoto tatu zinazorudisha nyuma juhudi za kufanya bunifu kwenye sekta ya afya.

Rais Samia ameyasema hayo leo Jumanne Oktoba 4, 2022 mjini Doha nchini Qatar aliposhiriki kwenye ufunguzi wa mkutano wa Dunia wa ubunifu wa masuala ya afya.

Amesema Tanzania kama zilivyo nchini nyingine imekuwa ikitumia kasi ya mabadiliko ya teknolojia kufanya bunifu ambazo zimekuwa na tija kwenye sekta ya afya.


“Baadhi ya vumbuzi ambazo zimekuwa na tija nchini ni mfumo wa simu wenye kumuwezesha mjamzito kuita usafiri kwa dharura na kupelekwa hospitali M-Mama pamoja na teknolojia inayotembea ya kulea watoto wenaozaliwa kabla ya wakati.

Ametaja teknolojia hizo zimekuwa na manufaa katika kupunguza vifo vya akina mama wajawazito na watoto, hatua ambayo sasa serikali inaendelea nayo ni kuhakikisha teknolojia hizo zinasambaa Tanzania bara na Zanzibar.

Changamoto alizotaja Rais Samia ambazo zinarudisha nyuma juhudi za ubunifu kwenye sekta hiyo ni pamoja na ukosefu wa wafanyakazi wenye ujuzi, uhaba wa miundombinu pamoja na kukosekana fedha kwa ajili ya kufadhili ubunifu,

“Niwaombe wote kuchukua fursa hii kutafuta mawazo ya pamoja kujadili njia bora tunazoweza kutumia kukabiliana na changamoto hizi wakati wa uvumbuzi,” amesema.