Rais Mwinyi ataja maeneo matatu Zanzibar kushirikiana na Ujerumani

Unguja. Rais wa Zanzibar Dk Hussein Mwinyi ameendelea na ziara yake nchini Ujerumani leo Jumatatu Juni 19, 2023 amekutana na Katibu wa Bunge Upande wa Wizara ya Ushirikiano wa kiuchuni na Maendeleo nchini Ujerumani Dk Barbel Kofler.
Katika mazungumzo yao yalijikita zaidi kuimarisha uhusiano uliopo baina ya Tanzania hususani Zanzibar kwa upande mmoja na Ujerumani.
Rais Mwinyi amemueleza Dk Kofler maeneo matatu ambayo Zanzibar ingependa zaidi kushirikiana na Ujerumani ikiwemo nchi hiyo kusaidia miradi ya maji, michezo na afya.
Pia namna ya kujenga misingi ya kuimarisha usimamizi wa matumizi ya fedha za miradi.
Naye, Dk Kofler amempongeza Rais Mwinyi kwa kuwa na mawaziri sita wanawake ndani ya Serikali anayoiongoza hatua inayodhihirisha kuwaongezea uwezo wanawake.
Katika hoja hiyo, Rais Mwinyi amemuhakikishia Dk Kofler kwamba viongozi wanawake aliowateua kushika nyadhifa mbalimbali wanafanya kazi nzuri na huenda akawapa nafasi wengi zaidi.
Rais Mwinyi yupo nchini Ujerumani pamoja na mambo mengine, alihudhuria ufunguzi wa mashindano ya Olimpiki maalumu ambapo Tanzania inawakilishwa na vijana 20.