Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Profesa Mbarawa: Naiona Tanzania mbali kiuchumi baada ya miaka mitano

Muktasari:

  • Tanzania imeendelea kujenga miundombinu ya kimkakati ambayo ni kiunganishi cha kiuchumi ndani na nje ya nchi.

Dar es Salaam. Ujenzi wa miundombinu bora na ya kisasa, fursa za kiuchumi pamoja na miradi mikubwa ya kimkakati kama reli ya SGR, madaraja, Bwawa la Umeme la Nyerere, viwanja vya ndege vya kimataifa ni miongoni mwa sababu zilizomfanya Waziri wa Uchukuzi, Profesa Makame Mbarawa kuiona Tanzania ikifika mbali kiuchumi ndani ya miaka mitano hadi sita ijayo.

Kwa sasa Tanzania ipo uchumi wa kati ngazi ya chini baada ya Benki ya Dunia (WB) mwaka 2020 kuiorodhesha kwenye nchi za uchumi huo, hata hivyo, tathmini inaonesha uchumi unakua kwa asilimia sita kwa mwaka katika kipindi cha miaka 20 iliyopita.

Waziri Mbarawa amesema utekelezaji wa miradi hiyo ya barabara, reli, madaraja, bandari na usafirishaji ni kichocheo kikubwa cha uchumi katika nchi yeyote ile duniani.

Alitoa kauli hiyo jana Jumapili Juni 22, 2025 kwenye Kongamano la Jukwaa la Fikra lililoandaliwa na Mwananchi Communications Limited kwa kushirikiana na Wizara ya Ujenzi.

Jukwaa hilo lililokuwa likijadili mada isemayo, ‘Kujenga Madaraja, Kujenga Taifa, Miundombinu kama Kichocheo cha Ukuaji Jumuishi.’

Mbarawa amesema nchi ikitaka kuendelea vizuri, inapaswa kuwa na miundombinu bora itakayochochea uchechemuzi wa uchumi huku akiamini baada ya miaka mitano au sita ijayo, Tanzania itakua na uchumi wa kati ngazi ya juu.

Wakati akiyasema hayo, Serikali kupitia Waziri wa Ujenzi, Abdallah Ulega imesema kwa sasa inajenga miundombinu ya barabara na madaraja kwa kutumia fedha zitokanazo na kodi ya wananchi kwa ajili ya kuboresha usafiri na maendeleo ya wananchi kama ilivyo daraja la JP Magufuli.

Daraja hilo la JP Magufuli ambalo awali lilijulikana kwa jina la Kigongo-Busisi, lina urefu wa kilomita 3.2 huk likiunganisha eneo la Kigongo wilayani Misungwi na Busisi wilayani Sengerema.

Kukamilika kwake kumerahisisha usafirishaji katika mikoa ya Mwanza, Geita, Kagera na Kigoma, kadhalika nchi jirani za Uganda, Rwanda, Burundi na Congo (DRC) na  likijengwa kwa Sh718 bilioni.

Hata hivyo, Waziri Mbarawa amesema katika kipindi cha miaka minne, barabara za lami zenye urefu wa kilomita 1,365 zimekamilika kujengwa na kilomita 2,380 za barabara za kiwango cha lami zinaendelea kujengwa nchi nzima.

Akirejea utekelezaji wa miradi mikubwa ya ujenzi ambayo iliachwa na Hayati Rais, John Magufuli wakati akiwa Waziri wa Ujenzi, Profesa Mbarawa amesema Rais Samia Suluhu Hassan wakati anaingia madarakani, alitoa maelekezo miradi yote ikamilike.

 “Nilipoingia, Rais Samia alisema lazima tuhakikishe miradi yote ikamilike kwa wakati ukiwamo mradi wa reli ya SGR, Daraja la Kigongo Busisi na uwanja wa Msalato, Rais alitupatia melekezo na tumeyafanyia kazi miradi inatekelezwa kwa vitendo na itakamilika kwa wakati,” amesema Mbarawa.

Amesema Serikali imeitekeleza miradi hiyo mikubwa ya kimkakati ambayo kwa kiasi kikubwa imetengeneza ajira na kufungua fursa za kiuchumi.

Daraja hilo limetajwa kuja kuimarisha diplomasia ya siasa na uchumi. “Ni daraja muhimu linalotuunganisha na wenzetu. Imeelezwa daraja hii kwa miaka ijayo itakua ni kiungo cha Afrika ya Kati na Magharibi,” amesema Mbarawa.

Awali katika kongamano hilo, Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Said Mtanda alisema muda na muingiliano wa haraka kibiashara ni miongoni mwa faida za moja kwa moja za daraja la JP Magufuli lililozinduliwa na Rais Samia siku nne zilizopita.

Mkuu huyo wa Mkoa amesema ujio wa daraja la JP Magufuli kumeleta athari chanya ikiwamo ya ujenzi wa mji wa kisasa mbele ya daraja hilo linalounganisha eneo la Kigongo na Busisi wilayani Sengerema.

Akitolea maoni yake juu ya maono ya Waziri Mbarawa, Mchumi Oscar Mkude amesema miundombinu ni lazima, lakini si kigezo pekee cha maendeleo ya kiuchumi, bali ni nyenzo ya kuchagiza uchumi na uzalishaji.

“Pamoja na miundombinu, lazima kuwe na jitihada za dhati kwenye kutengeneza ajira za Watanzania wengi ambao hawana ajira leo, hawatakuwa na ajira kesho na wengine kamwe hawatapata nafasi ya kuajiriwa katika maisha yao.

“Ajira ni zao la uchumi na uzalishaji ambazo huonekana sio tu kwenye ukuaji wa uchumi, lakini pia kwenye tabasamu la watu, kwa sababu  wanakuwa na uhakika wa leo na kesho yao. Hivyo, sawa kwa miundombinu, kazi zaidi bado iko mbele yetu kama taifa,” amesema Mkude.