Profesa Kitila: Kupungua misaada ituamshe Afrika kujitegemea kiuchumi

Muktasari:
- Tanzania imeshaanza kutekeleza baadhi ya miradi yake ya ujenzi kwa kutumia kodi za wananchi, ikiwemo ujenzi wa Daraja la JP Magufuli (Kigongo-Busisi) na Bwawa la Umeme la Mwalimu Julius Nyerere.
Dar es Salaam. Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – Mipango na Uwekezaji, Profesa Kitila Mkumbo amesema kuendelea kupungua kwa mikopo kutoka nchi mbalimbali, ikiwemo ile ya Ulaya, kunatakiwa kuziamsha nchi za Afrika kuwa wakati wa kujitegemea kiuchumi umefika.
Hiyo ndiyo sababu ya Tanzania kuanza kutekeleza miradi ya ndani kwa kutumia fedha za walipa kodi, ikiwemo ujenzi wa Daraja la JP Magufuli (Kigongo-Busisi) na Bwawa la Umeme Julius Nyerere (JNHPP).

Profesa Mkumbo ametoa kauli hiyo jana, Juni 22, 2025 katika Jukwaa la Fikra lililoandaliwa na Kampuni ya Mwananchi Communications Limited (MCL) kwa kushirikiana na Wizara ya Ujenzi, likijadili mada isemayo “Kujenga Madaraja, Kujenga Taifa: Miundombinu kama Kichocheo cha Ukuaji Jumuishi.”
Amesema tangu mwaka 2020, kupitia mradi wa Kigongo-Busisi na JNHPP ambayo imetumia fedha za Watanzania katika ujenzi wake, ni ishara kuwa Tanzania imeanza kufanya vizuri.
Amesema hiyo ni ishara kuwa baada ya miaka 60 ya Uhuru, nchi inaweza kujenga miundombinu yake yenyewe, jambo aliloliita kujitegemea kiuchumi.
“Mwanzoni tulipata uhuru wa kisiasa, na sasa tumeanza kupitia miradi hii kwenda katika ulimwengu wa kujitegemea kiuchumi. Katika ulimwengu wa leo, ambapo misaada na mikopo kutoka nchi zilizoendelea, ikiwemo za Ulaya, inazidi kupungua kwani kila nchi inaangalia ndani kwake kulivyo, inatuamsha kuwa sasa Afrika inabidi kujitegemea,” amesema.
Waziri huyo amesema kilichofanyika kupitia miradi hiyo ni kama kuwakumbusha Waafrika kujitegemea kiuchumi, jambo ambalo ni muhimu huenda kuliko huko awali.

Katika kutambua hilo, Profesa Mkumbo amesema kazi ya Serikali, mbali na ulinzi na usalama, kutoa na kusimamia haki na sheria, kazi ya tatu ni ujenzi wa miundombinu ya uchumi.
Amesema ujenzi wa Daraja la Kigongo-Busisi unasimama kama sehemu ya ujenzi wa miundombinu ya uchumi na usafiri na usafirishaji.
“Serikali imetekeleza wajibu wake muhimu, kwani itamuwezesha mwananchi kujijenga kiuchumi na apate fedha na hii itawawezesha kushiriki katika shughuli za uzalishaji na kufanya biashara,” amesema Profesa Mkumbo.
Amesema Kanda ya Ziwa yenye takriban watu milioni 16.36, sawa na asilimia 26 ya watu wa Tanzania na uchumi wa Sh49 trilioni, ni muhimu katika uchangiaji wa pato la Taifa.
Kwa upande wa Jiji la Mwanza, amesema ni la pili kwa kuchangia pato la Taifa, kwani huchangia Sh13.5 trilioni, ikiwa na maana kuwa shughuli za uzalishaji Kanda ya Ziwa ni sehemu muhimu katika ujenzi wa uchumi wa nchi.
“Watu wanahitaji uhuru wa kiuchumi, waweze kuzalisha na kusafirisha bidhaa kufikia soko na hapo wanahitaji usafiri wa uhakika unaotumia muda mfupi na gharama nafuu. Hivyo, ujenzi wa daraja hili unatuambia kuwa unaenda kuchochea shughuli za kiuchumi za Mkoa wa Mwanza na mikoa ya Kanda ya Ziwa kwa ujumla,” amesema.

Amesema kupitia ujenzi huo, wananchi wataweza kusafirisha bidhaa zao kwa urahisi na kwamba daraja hilo linakwenda kuchochea uhusiano wa Tanzania kupitia Mwanza na Geita na nchi jirani.
“Rais alipoingia madarakani, ajenda kubwa ilikuwa kuifungua nchi. Huwezi kufungua nchi bila kufungua miundombinu ya usafiri na usafirishaji, hivyo daraja hilo na miundombinu mingine inayoendelea ni sehemu muhimu sana katika kuifungua nchi,” amesema.
Lengo kubwa la Serikali ni kuunganisha na mipango ya muda mrefu ya nchi kupitia Dira ya Taifa 2050, ambayo itawasilishwa bungeni hivi karibuni, inayolenga kujenga uchumi wa Dola trilioni moja ifikapo mwaka 2050. Moja ya kichocheo cha uchumi ni miundombinu fungamanishi ya usafiri na usafirishaji.
“Wizara ya Ujenzi wanatekeleza Dira 2050 kwa ujenzi wa miundombinu ya kiuchumi,” amesema.
Akizungumzia faida za uboreshaji wa miundombinu, amesema watu wengi wanapotaja nchi zilizoendelea, huangalia zaidi miundombinu ya usafiri na usafirishaji.
“Waliofika Mwanza wakiliona daraja hilo linavyopendeza na kuvutia ni dalili kubwa ya maendeleo katika maeneo husika. Watu wa Mwanza na Geita wanatambulika kupitia daraja hili la Kigongo-Busisi . Ni alama kubwa ya maendeleo katika Mkoa wa Mwanza, Kanda ya Ziwa na Tanzania kwa ujumla,” amesema.

Akielezea namna uboreshaji wa miundombinu katika kanda hiyo ni muhimu, Profesa Mkumbo amesema anatambua kuwa wakazi wa maeneo hayo wanategemea kilimo, hivyo usafirishaji wa mazao pande zote mbili na mikoa jirani umekuwa rahisi.
“Usafiri umerahisishwa, pia usafirishaji wa samaki, madini na mazao muhimu unafanyika kwa ufanisi. Biashara na nchi za Uganda, Rwanda tunatarajia zikue sana kati ya Tanzania na Jumuiya ya Afrika Mashariki,” amesema.
Amesema moja ya matarajio ni kuona katika miaka michache ijayo pato la Taifa la wananchi wa mikoa yote ya Kanda ya Ziwa likue, uzalishaji uongezeke na biashara ikue miongoni mwa wananchi na nchi kwa ujumla.