Miundombinu ya barabarani, madaraja tumejenga wenyewe

Muktasari:
- Imeeleza katika kipindi cha miaka minne barabara za lami zenye urefu wa kilomita 1,365 zimekamilika kujengwa na kilomita 2,380 za barabara za kiwango cha lami zinaendelea kujengwa nchi nzima.
Dar es Salaam. Serikali imeeleza kuwa kwa sasa inajenga miundombinu ya barabara na madaraja kwa kutumia fedha za kodi kwa ajili ya kuboresha usafiri na maendeleo ya wananchi.
Imeeleza katika kipindi cha miaka minne barabara za lami zenye urefu wa kilomita 1,365 zimekamilika kujengwa na kilomita 2,380 za barabara za kiwango cha lami zinaendelea kujengwa nchi nzima.
Hayo yamesemwa usiku wa leo Jumapili Juni 22, 2025 na Waziri wa Ujenzi, Abdallah Ulega wakati akizindua Kongamano la Mwananchi Jukwaa la Fikra lililoandaliwa na Kampuni ya Mwananchi Communications Limited (MCL) kwa kushirikiana na Wizara ya Ujenzi.

Waziri wa Ujenzi, Abdallah Ulega akifungua Mwananchi Jukwaa la Fikra linalofanyika jijini Dar es Salaam leo.Pichaz zote na Sunday George
Kongamano hilo ambalo limewakutanisha wadau mbalimbali wa Serikali na sekta binafsi wakijadili mada isemayo ‘Kujenga Madaraja kujenga Taifa Miundombinu kama Kichocheo cha Ukuaji Jumuishi.’
Kongamano hilo linafanyika siku chache kupita tangu Daraja la JP Magufuli lililojengwa kwa fedha za wananchi Sh718 bilioni, limezinduliwa Juni 19, 2025 na Rais Samia Suluhu Hassan.
Katika kongamano hilo, wageni walianza kuwasili kuanzia saa 12 jioni na saa moja usiku kongamano hilo lilifunguliwa rasmi.
Wageni waliohudhuria katika kongamano hilo ni pamoja na Waziri wa Ujenzi, Abdallah Ulega, Waziri wa Uchukuzi, Profesa Makame Mbarawa, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji, Profesa Kitila Mkumbo na Waziri wa Habari, Utamaduni na Michezo, Profesa Palamagamba Kabudi.

Washiriki wakifuatilia kongamano la Mwananchi Jukwaa la Fikra lililoandaliwa na Kampuni ya Mwananchi Communications Limited (MCL) kwa kushirikiana na Wizara ya Ujenzi.
Pia limehudhuriwa na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila, Katibu Mkuu wa Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM), Jokate Mwegelo, makatibu wakuu, wabunge na viongozi mbalimbali.
Waziri Ulega amesema Rais Samia wakati wa uzinduzi wa daraja hilo aliweka bayana nchi imefanya ujenzi wote kwa miaka minne, kwa sababu ya maono, kutokana na jasho letu wenyewe fedha na ubunifu wetu wenyewe.
Amesema Rais Samia alisisitiza mafanikio makubwa kama Taifa mengi tumeyafanya wenyewe kwa hiyo Watanzania tujipongeze kwa kazi kubwa.
"Fedha hizo zimetokana na kodi zetu sisi Watanzania wenyewe ambazo zimekusanywa na taasisi zetu, ukusanyaji kodi ndiyo imesababisha kujenga Daraja la Magufuli na hapo ndiyo umuhimu wa ulipaji kodi unapoonekana,” amesema.

"Baadaye manguli wa kihistoria kama kina Profesa Kabudi wanajua nchi hii tumejenga mabarabara zetu sisi wenyewe wakati wakoloni wanaondoka hatukuwa na barabara zaidi ya Dar es Salaam kwenda Morogoro, walijenga ili kusafirisha mkonge kama ile ya Tanga kwenda Korogwe," amesema.
Ulega amesema barabara zingine nchi ilijenga yenyewe ikiwa huru tofauti na nchi zingine ambazo walirithi kutoka kwa makucha ya wakoloni na kwamba Watanzania wanapaswa kufahamu historia hiyo.
Amesema katika sekta ya barabara kwa kipindi cha miaka minne, kilomita 1,365 za lami zimekamilika kujengwa na kilomita 2,380 za barabara za kiwango cha lami zinaendelea kujengwa nchi nzima.
"Wastani wa barabara ya lami kwa kiwango tunachojenga inaanzia Sh1.5 bilioni mpaka Sh2 bilioni kwa kilomita moja, kwa hiyo kilomita hizo ukitaka kujua gharama yake huchukua wastani kisha utapata jawabu ni kiasi gani cha fedha kimetumika,” amesema.
"Jumla ya madaraja manane yamejengwa na mengine 12 yanaendelea kujengwa. Huu ni mtazamo wa dhamira ya nchi kwenye kuhakikisha mikoa yote inaunganishwa kwenye mifumo ya barabara na nchi jirani na mfungamano wetu unakua, mfano ni wa daraja la JPM litakalounganisha Afrika ya kati yote," amesema Ulega.
Waziri Ulega amesema mustakabali wa Taifa letu katika maendeleo unaanzia kuhakikisha watu wanaweza kusafiri kutoka eneo moja kwenda jingine bila usumbufu kwa haraka na uhakika.

Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Reli Tanzania (TRC), Masanja Kadogosa kwenye kongamano la Mwananchi Jukwaa la Fikra lililoandaliwa la Mwananchi Communications Limited kwa kushirikiana na Wizara ya Ujenzi.
Amesema lengo la nchi ni kuendelea kuwa na miundombinu imara ya barabara, reli vivuko na madaraja ambayo itafanya kuwa rahisi kwa watu, huduma na bidhaa kusogea kutoka sehemu moja kwenda nyingine.
"Kupitia jukwaa hili tutaangalia mafanikio yapi tulipitia na ili tuweze kujua changamoto zipi tunapitia na namna bora ya kuzitatua kwa pamoja. Barabara zetu zimekuwa kama mishipa ya damu," amesema.
Amesema nchi inayo matamanio makubwa na uhitaji ni mkubwa katika hilo Serikali inaendelea kuwekeza hatua kwa hatua na ili tutumie kidogo tulichonacho kwa umakini ili kuja kuongeza mapato.
Hata hivyo, amesema kutokana na mabadiliko ya tabianchi imesababisha changamoto nyingi.
"Ni dhamira ya Rais kuhakikisha hakuna anayeachwa nyuma na waliokuwa kundi moja la kijinsia linakuwa halijakaa vizuri, wapo kinamama ambao ni makandarasi na kwa maelekezo amesema ni muhimu tuwape aina ya upendeleo na hata juzi tumewapa kandarasi kwa sifa zao.

Rais Samia Suluhu Hassan akizindua daraja la JP Magufuli mkoani Mwanza.
"Kampuni zaidi ya nane za kinamama tumewapa miradi mbalimbali hususan nyanda za juu kusini kama Songwe ili tuendelee kuwajengea uwezo hatua kwa hatua," amesema.
Kwa mujibu wa Ulega sekta ya ujenzi na mipango ya Taifa kuhusu dira ya maendeleo ya mwaka 2050, uwekezaji wa miundombinu ni miongoni mwa uchumi wa kisasa unaojali makundi yote tena shirikishi lakini pia ushirikishwaji wa sekta binafsi.
Ilichokisema MCL
Awali, Mkurugenzi Mtendaji wa Mwananchi Communications Limited (MCL), Rosalynn Mndolwa-Mworia, amesema Jukwaa la Fikra ni muhimu la kitaifa linalotoa fursa ya kutafuta suluhisho la pamoja katika changamoto mbalimbali za maendeleo.
“Kauli yetu inabaki kuwa kutafuta suluhisho la pamoja. Tunaamini kuwa majadiliano ya wazi, jumuishi na yenye mwelekeo ni msingi wa maendeleo endelevu na shirikishi,” amesema Rosalynn.

Mkurugenzi Mkuu wa Mwananchi Communications Limited Rosalynn Mworia (kushoto) akimkaribisha Waziri wa Ujenzi Abdullah Ulega katika Jukwaa la Fikra linalofanyika jijini Dar es Salaam leo.Pichaz zote na Sunday George
Rosalyn amesema Jukwaa la Fikra huwa linalenga kuwapa Watanzania majukwaa ya kuchangia namna mabadiliko chanya yanavyoweza kufanyika.
Pia amesema majukwaa haya husaidia watendaji kupata mbinu za kuboresha utendaji na kuleta tija kwa Taifa.
“Tunajivunia kwani tukio hili ni la kipekee linalofanywa siku chache baada ya uzinduzi wa daraja la JP Magufuli uliofanyika Juni 19, daraja hili si kiunganishi tu cha kijiografia baina ya pande mbili lakini kiunganishi cha mikoa na uchumi wa Taifa,” amesema.
Amesema Mwananchi kama chombo cha habari inaendelea kutekelea kauli mbiu yake ya kutafuta suluhisho la pamoja kwani majadiliano ya wazi na jumuishi yenye mwelekeo ni msingi wa maendeleo endelevu na shirikishi.
“Ni sehemu ya utekelezaji wa dhamira ya MCL kwani kama chombo cha habari si kwa jukumu la kuhabarisha pekee, bali kuunganisha jamii na viongozi wake kuchochea mijadala ya kitaifa na kuwezesha ushiriki wa wananchi katika masuala yenye masilahi mapana kwa nchi,” amesema.
Mtazamo wa Profesa Kitila
Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji, Profesa Kitila Mkumbo amesema kupitia utekelezaji wa baadhi ya miradi iliyofanywa kwa fedha za ndani ni ishara kuwa Tanzania inaanza kujitegemea kiuchumi.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji, Profesa Kitila Mkumbo. akizungumza kuhusiana mada kujenga madaraja ,kujemga Taifa wakati wa Jukwaa la Fikra linalofanyika jijini Dar es Salaam leo.Pichaz zote na Sunday George
Ametolea mfano wa miaka ya hivi karibuni ujenzi uliofanyika wa mradi wa daraja la JPM na bwawa la umeme la Julius Nyerere ambapo takriban Sh7 trilioni zimetumika kukamilisha miradi hiyo.
“Hizi ni fedha za Watanzania kupitia kodi zao maana yake nchi yetu tuna uwezo wa kusimamia ujenzi wa miundombinu ya uchumi wenyewe na huku ndiyo kujitegemea kiuchumi,” amesema.
Amesema awali nchi ilipata uhuru wa kisiasa na sasa kupitia utekelezaji wa miradi hiyo ni hatua za kuelekea uhuru wa kujitegemea kiuchumi.
“Daraja litakwenda kuongeza ufanyaji biashara kati ya wananchi wa mikoa ya Mwanza na Geita na nchi za jirani,” amesema Profesa Mkumbo.
Amesema pia anaamini mchango wa Kanda ya ziwa kutokana na uzalishaji kwa mtu mmojammoja kukua na Taifa kwa ujumla.
Alichokisema Profesa Kabudi
Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Profesa Palamagamba Kabudi amesema Daraja la JP Magufuli linaendeleza sifa ya Tanzania kuwa lango la nchi nyingine za Afrika Mashariki.

Waziri wa Habari, Sanaa na Michezo, Profesa Palamagamba Kabudi akizungumza kuhusiana mada kujenga madaraja ,kujenga Taifa wakati wa Jukwaa la Fikra linalofanyika jijini Dar es Salaam leo.Picha na Michael Matemanga
“Daraja hili linaimarisha diplomasia ya siasa na diplomasia ya kiuchumi. Ni daraja muhimu linalotuunganisha na wenzetu. Daraja hii kwa miaka ijayo Litakua ni kiungo cha Afrika ya Kati na Magharibi,” amesema.
Amesema jiografia ya Tanzania kuanzia mipaka ya nchi, bahari na bandari zilizopo inaunganisha nchi nyingi na ndio nchi yenye majirani wengi kuliko nyingine yeyote ya AfrIka Mashariki ikiwa ndio lango la kwenda nchi hizo kupitia bandari.
Amesema kutokana na umahiri wa Rais Samia Suluhu Hassan katika diplomasia ya kiuchumi umesababisha daraja hilo kumaliza kwa asilimia 100 tayari kwa kufungua uchumi wa ndani na nje ya nchi.
...miaka mitano Tanzania itakuwa mbali
Waziri wa Uchukuzi, Profesa Makame Mbarawa amesema nchi ikitaka kuendelea vizuri inapaswa kuwa na miundombinu ili kukua kiuchumi, huku akiamini baada ya miaka mitano au sita ijayo Tanzania itakua na uchumi wa kati juu.
Akirejea utekelezaji wa miradi mikubwa ya ujenzi ambayo iliachwa na Rais wa awamu ya tano, hayati John Magufuli wakati akiwa Waziri wa Ujenzi, Profesa Mbarawa amesema Rais wa sasa Samia Suluhu Hassan wakati anaingia madarakani Machi 19, 2021 alitoa maelekezo miradi yote ikamilike
“Alipoingia Rais Samia Suluhu Hassan alisema lazima tuhakikishe miradi yote, ikamilike kwa wakati ikiwemo mradi wa reli ya SGR, Daraja la JP Magufuli, uwanja wa Msalato, Rais alitupatia maelekezo na tumeyafanyia kazi, miradi inatekelezwa kwa vitendo na itakamilika kwa wakati.” amesema Mbarawa.
RC wa Mwanza
Mkuu wa Mkoa wa Mwanza (RC), Said Mtanda amesema muda na mwingiliano wa haraka kibiashara ni miongoni mwa faida za moja kwa moja za daraja la JP Magufuli lililozinduliwa na Rais Samia Suluhu Hassan siku tatu zilizopita.
“Wananchi walikuwa wakipata adha ya kutumia muda mrefu kukaa darajani kwa kusubiri kivuko kwa muda wa saa moja hadi kijae kisha saa moja pia kuvuka wakati mwingine hadi saa nne.

Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Said Mtanda akizungumza mada kujenga madaraja ,kujenga Taifa wakati wa Jukwaa la Fikra linalofanyika jijini Dar es Salaam leo.Pichaz zote na Sunday George
“Kwa siku wanavuka watu 9,000 hadi 13,000 na wanalazimika kutoa Sh400 kuvuka maana yake wanatumia Sh1.8 bilioni kwa mwezi. Lakini kwa sasa mwananchi anafaidika kuvuka bure,” amesema.
Amesema kwa sasa wananchi wanatumia dakika tano kuvuka na kurahisisha muda ambao kiuchumi ina faida hata kwa wafanyabiashara.
Amesema kwa mikakati iliyopo sasa ikiwemo ujenzi wa kiwanja cha ndege cha kimataifa anaamini Mwanza itaipita Dar es Salaam kiuchumi na kimapato.