Papa Potwe: Kiumbe adhimu wa Mafia

Utalii wa Papa Potwe umekuwa ni miongoni mwa vyanzo vikuu vya mapato kisiwani Mafia.
Muktasari:
- Wamejizolea umaarufu wa kuwa miongoni mwa viumbe wakubwa na wenye sura mbaya zaidi na hii huenda ikawafanya watu wengi kuamini kuwa ni miongoni mwa viumbe hatari baharini.
Wamejizolea umaarufu wa kuwa miongoni mwa viumbe wakubwa na wenye sura mbaya zaidi na hii huenda ikawafanya watu wengi kuamini kuwa ni miongoni mwa viumbe hatari baharini.
Hata hivyo ukweli ni tofauti, kila kitu kuhusu kiumbe huyu ni cha kusisimua na kushangaza na tofauti na hisia za watu. Tuanze na jina lake: Anaitwa Papa Potwe, Je yeye ni Papa au ni Potwe? Ukweli ni kuwa samaki huyu mkubwa duniani ni Papa na sio Potwe.
Wengi tukisikia Papa tunapata hofu kwa kuamini kuwa ni kiumbe hatari kabisa kwa maisha ya binadamu huko baharini.
La hasha, huyu ni miongoni mwa aina ya Papa wengi ambao sio hatari hata kidogo. Kiukweli samaki huyu anajulikana kwa kuwa mkubwa na mpole. Ingawa ni Papa lakini pia ana tabia nyingi zinazoshabihiana na Potwe na huenda ndiyo maana akaitwa Papa Potwe.
Ni mkubwa kama Potwe na pia ulaji wake unafanana zaidi tofauti na samaki wa jamii yake. Hebu turejee kwenye imani ya wengi kuwa hawa ni samaki wenye sura mbaya kuliko wote, ukweli hili nalo linabaki kuwa 50/50 wengi wanamchukulia kama samaki mwenye muonekano mzuri kutokana na rangi yake na madoa madoa ya kipekee ambayo yako tofauti kwa kila Papa Potwe.
Papa Potwe mkubwa anaweza kufikia kimo cha mita 12 mpaka 18. Kiumbe huyo mmoja aliyepatikana miaka michache nyuma alifikia kiasi cha mita 18.8, fununu nyingine zinasema wanaweza kufika mpaka kimo cha mita 20, sawa na basi kubwa la kubeba wanafunzi.

Ingawa Papa Potwe wana meno madogo madogo kwa maelfu, hawayatumii meno haya kwa kutafuna wala kukata chakula chao.
Ulaji wao mara nyingi huwa mgumu wakilazimika kusafiri kwa umbali mkubwa wakiwa vinywa wazi ili kukusanya visamaki vidogo vidogo na mimea ya baharini ambayo ndio chakula chao kikuu.
Kutokana na ukubwa wa miili yao Papa Potwe hula chakula kingi huku ikikadiriwa kuwa papa potwe mdogo anaweza kula yapata kilo 21 kwa siku moja.
Inaaminika kuwa ni asilimia 10 tu ya Papa Potwe ndiyo hufanikiwa kukua lakini hawa wanaofanikiwa kukua wanaweza kufikia mpaka miaka 70 na kuwa miongoni mwa viumbe wa bahari wanaoishi kwa muda mrefu.
Wanapata uwezo wa kuzaliana kuanzia miaka 30. Kutokana na kuwa na miili mikubwa samaki hawa huogelea kwa mwendo wa pole pole ikikadiriwa kuwa wanaweza kuogelea kwa kilomita 4.8 kwa saa, lakini pia wana uwezo wa kuogelea mwendo mrefu kwa maelfu kwa siku.

Kuna maandiko machache juu ya kuzaliana kwa Papa Potwe, lakini samaki hawa hutunza na kutotoa mayai yao kwenye tumbo la papa potwe jike na huweza kupata mpaka watoto 300 kwa mara moja.
Watoto hawa huachiwa wakajitegemee wakiwa wadogo sana na huenda hii ndio sababu ya kuwa na hatari ya kufa wakiwa bado wadogo. Papa Potwe wanapatikana katika bahari zenye ujoto zote isipokuwa Bahari ya Mediteraniani pekee.
Mara nyingi hupendelea sehemu zenye uhakika wa chakula na mahali salama kwao kwa kuzaliana. Je nimekuambia kuhusu uzito wa samaki huyu?
Hakika kutokana na ukubwa wa mwili wake bila shaka atakuwa na uzito mkubwa, lakini je waweza kukadiria uzito wa samaki huyu? Papa Potwe mkubwa anakadirikwa kufika tani 26 hata zaidi, sawa na tembo karibu sita.
Papa Potwe wamejizolea umaarufu wa kuwa kivutio kikubwa katika utalii wa baharini sehemu mbalimbali. Kwa bahati nzuri Tanzania pia tumepata bahati ya kuwa makazi ya Papa Potwe huko kisiwani Mafia.
Hii ni sehemu pekee ambayo Papa Potwe wanapatikana nchini Tanzania. Wakati mzuri wa kuwashuhudia Papa Potwe kisiwani Mafia ni kati ya Oktoba mpaka Februari kila mwaka huku Novemba na disemba ikiwa miezi ambayo utakuwa na uhakika wa kuwaona Papa Potwe kwa uzuri na hata kuogelea nao kama una ujasiri huo!
Utalii wa Papa Potwe umekuwa ni miongoni mwa vyanzo vikuu vya mapato kisiwani Mafia huku Serikali ikikusanya zaidi ya Sh80 milioni kwa mwaka kupitia utalii huo. Pia umekuwa chanzo cha ajira kwa wakazi wengi wa Mafia kupitia shughuli za kutembeza watalii, kuendesha boti za watalii, mahoteli na kadhalika.
Waweza kuwa unajiuliza kwa nini haswa Mafia? Papa Potwe huenda mahali ambako wanakuwa na uhakika wa kupata chakula na hii si tatizo katika kisiwa cha Mafia, baadhi ya Papa Potwe wameendelea kuonekana katika Pwani ya Mafia kila mwaka kwa zaidi ya miongo kadhaa.
Kwa bahati mbaya samaki hawa wakubwa na wapole wako katika hatari ya kutoweka na hakika na jitihada za binafsi na za pamoja wanaweza kubaki historia. Papa Potwe wanavuliwa kwa ajili ya matumizi ya kitoweo na wakati mwing-ine mapezi yao.
Umoja wa Kimataifa wa Uhifadhi wa Maliasili (IUCN) umewaweka Papa Potwe kwenye orodha ya viumbe walio katika hatari ya kutoweka. Nchini Tanzania papa potwe wanalindwa kisheria na hawaruhusiwi kuvuliwa.
Ama kwa hakika wavuvi wa Kisiwani Mafia wanalizingatia sana hili na hata inapotokea papa potwe akakamatwa na nyavu zao basi humnasua kwa haraka na kumuachia huru. Idadi halisi ya Papa Potwe haijulikani huku kukiwa na makadirio ya viumbe wapatao laki mbili, lakini cha uhakika ni kuwa katika kipindi cha miaka 75 tu Papa Potwe wamepungua kwa kiasi cha asilimia 50.
Tanzania mwaka 2012 walikuwepo Papa Potwe chini ya 100. WWF Tanzania imekuwa ikishirikiana na Serikali kisiwani Mafia pamoja na wadau wengine katika uhifadhi wa Papa Potwe ikiwa ni pamoja na kutengeneza mpango mkakati wa uhifadhi wake lakini pia kutoa elimu ya uhifadhi wa Papa Potwe kwa makundi mbali mbali ya kijamii kama wanafunzi, wananchi, wafanya biashara na hata maafisa wa Serikali.
WWF Tanzania pia imesaidia katika utafiti kwa kushirikiana na kundi la watafiti wa Marine MegaFauna Foundation ili kufahamu idadi ya Papa Potwe tabia zao na kadhalika.
Mwaka huu wakati tukiadhimisha siku ya papa potwe duniani Agosti 30 tunayo furaha kusema kuwa idadi yao imeongezeka mpaka kufikia 215.
Tunatoa wito kwako leo wakati tukiwaadhimisha viumbe hawa adhimu kuwa sehemu ya mabadiliko katika uhifadhi wa Papa Potwe kwa kuchukua hatua za makusudi kuwalinda ikiwa ni pamoja na kupunguza au kuacha kutumia plastiki kwani mara nyingi hizi huishia baharini, kuwaelimisha wengine ambao hawajapata bahati ya kuwafahamu Papa Potwe lakini pia kujiandaa kwenda kuwashuhudia Papa Potwe huko kisiwani Mafia na pia kuogolea na viumbe hawa wa ajabu.
Heri ya siku ya Papa Potwe!