Prime
Alichokisema Jaji Warioba miaka 61 ya Muungano

Jaji Joseph Warioba akizungumza wakati wa mahojiano maalumu na waandishi wa Kampuni ya Mwananchi Communications Limited (MCL), leo, Aprili 16, 2025 katika ofisini kwake jijini Dar es Salaam.
Aprili 26, kila mwaka Watanzania husherehekea Sikukuu ya Muungano, mwaka huu ukifikisha miaka 61. Muungano huo wa Tanganyika na Zanzibar ndio ulizaa nchi ya Tanzania, Aprili 26, 1964.
Wakati Watanzania wakiadhimisha miaka 61, Waziri Mkuu mstaafu, Jaji Joseph Warioba ameielezea miaka 61 ya Muungano huo, ulipotoka na ulipo hivi sasa. Anasema katika miaka 61, Muungano upo imara.
"Wengi wanaposikia kero za Muungano huwa wanafikiri kuna udhaifu, Muungano upo imara," anasema Jaji Warioba katika mahojiano maalumu na Mwananchi yaliyofanyika ofisi kwake jijini Dar es Salaam hivi karibuni.
Katika mahojiano hayo yaliyoangazia masuala mbalimbali, ikiwamo ya uchaguzi mkuu, Jaji Warioba aligusia mwelekeo wa Muungano, ulipotoka na ulipo hivi sasa.
"Kwa wananchi, Muungano upo imara, changamoto zilizopo ni za kiutawala, siyo kwa mwananchi wa kawaida," anasema Jaji Warioba akifafanua.
"Mwananchi wa kawaida katika Muungano anachokihitaji ni kupata haki yake ya kawaida ambayo wanazipata na changamoto iliyobaki ni ya kiutawala.
"Tulipoanza Muungano kulikuwa na matatizo kidogo, kwani tuliuanza bila Katiba ya Muungano na bila sheria za Muungano.
"Hatukuwa na taasisi za Muungano, mwaka 1964 katiba ya Tanganyika ilifanyiwa marekebisho madogo ili iwe ya Muungano, haikuwa imeunganisha nchi, ilisema kutakuwa na Rais wa Muungano na Makamu wa Rais wawili,” anasema.
Akifafanua juu ya muundo huo, Jaji Warioba anasema, makamu mmoja ni Rais wa Zanzibar ambaye majukumu yake ni kumsaidia Rais wa Muungano kwa mambo ya Zanzibar na makamu mwingine ni wa Bara ambaye atamsaidia Rais kwa mambo ya Bara.
"Kabla ya mwaka 1977 tuliendelea kuwa na Serikali ya nchini mbili, ndio maana hata azimio la Arusha halikuihusu Zanzibar.
Mwaka 1977 ndipo ikachukuliwa hatua ya kuunganisha Serikali, tukaondoa makamu wawili tukabaki na mmoja ambaye huyu anamsaidia Rais kwa mambo yote, mtaona Karume hakuwa anakuja Bara kwa mambo ya Serikali, Jumbe baada ya kubadilika katiba alikuwa msaidizi," anasema.
Akiendelea kufafanua hilo, Jaji Warioba anasema wakati huo kila nchi iliendelea na mambo yake na kuyaunganisha ikawa ngumu.
"Ndiyo matatizo yakaanza, wakati ule Zanzibar iliendesha bandari yake.
"Itakumbukwa hadi mwaka 1980 watu wa Bara kwenda Zanzibar ilikuwa ni hadi uwe na pasipoti, hata hivyo changamoto hizo tumezimaliza wananchi wametulia, zilizobaki ni za kiutawala," anasema.
Gundi ya muungano
Katika miaka 61, Jaji Warioba anasema kazi iliyopo ni kuendelea kuunganisha Muungano ambao ameutaja kuwa gundi inayounganisha umoja, mshikamano na amani ya nchi.
Alitolea mfano namna Muungano ulivyowaunganisha Watanzania, akieleza namna Wazanzibari wanavyoishi Bara vivyo hivyo watu Bara wako kule wakifanya shughuli zao.
"Popote utakapokwenda utahudumiwa kama Mtanzania. Kwa wananchi wameridhika, matatizo yaliyopo ni ya kiutawala. Kwa wananchi hatujasikia kwamba watu wa Bara au Zanzibar wanabaguliwa," anasema.
Akikazia hilo, anasema Muungano bado uko imara, ukivurugwa, Watanzania watapata matatizo makubwa.
"Tufikirie tu watu wa Bara waliopo Zanzibar, hata tukikusanya Diaspora tulionao (Watanzania waishio nje ya nchi) haifikii idadi ya watu wa Bara waliopo Zanzibar, vivyo hivyo kwa Wazanzibari waliopo Bara idadi yao ni theluthi ya Watanganyika, fikiria kwa idadi hiyo bila Muungano tutakuwa na diaspora kiasi gani?" anahoji.
Jambo la msingi ambalo Watanzania wanapaswa kujivunia ni uwepo wa Muungano na wakumbuke kuwa hiyo ni kama gundi inayoendelea kuunganisha umoja, mshikamano na amani ya nchi.
Aonya udini, ukabila
Jaji Warioba katika kuimarisha Muungano, anaonya baadhi ya watu wanaoonyesha ubaguzi wa kidini na kikabila.
Anasena udini na ukabila bado vipo na vinaenezwa na baadhi ya watu wanaoleta lugha ya ubaguzi na wanatakiwa kukemewa.
"Hawa watu wanaturudisha nyuma, nimeona katika matamko, lugha ama sera za watu fulani fulani zinaingilia umoja wetu.
"Bado makabila yapo, bado ukabila upo na haukemewi, pia bado ubaguzi wa kidini upo, ubaguzi wa Kanda nao upo, zaidi ubaguzi huo unaingia na kuanza kuzuka kwenye Utaifa," anasema jaji huyo.
Katika kukazia kauli yake ya ubaguzi, hasa kwenye utaifa, Jaji Warioba alieleza kusikia maneno ya baadhi ya watu wakisema huyu hawezi kuchaguliwa kwa sababu ya eneo analotoka.
"Hii inaweza kuchukuliwa kawaida, lakini ni kitu hatari kwa umoja wetu, huko nyuma hatukuwa na ubaguzi," anasema.
Akitolea mfano wa namna Tanzania inavyosifiwa nje ya nchi kwa kazi ya ukombozi Kusini mwa Afrika, Warioba anasema kazi hiyo ilifanywa na Watanzania bila kuangalia huyu anatoka wapi na yule wapi.
"Mwalimu (Baba wa Taifa, Hayati Julius Kambarage Nyerere) ndiye aliongoza, alikuwa na timu ya washauri, nilikuwa katika ile timu na tulifanya kazi kama Watanzania bila kujali umetoka wapi.
"Tangu nikiwa Mkurugenzi wa Masuala ya Mambo ya Sheria, kisha Mwanasheria Mkuu niliendelea kuwa katika timu ile ya ukombozi, Salim alikuwa New York (Marekani) kama balozi, ndiye aliyekuwa mwenyekiti katika timu ya ukombozi, tulifanya kazi kwa pamoja," anasema.
Warioba anasema mwaka 1976 Mwalimu (Nyerere) aliwatuma kwenda Geneva kwenye mazungumzo ya kwanza ya uhuru wa Zimbabwe.
"Nataka niwaambie tu, ukienda nchi zozote za Kusini, huko Angola, Namibia, Zimbabwe, Msumbiji na Afrika Kusini, wanaishukuru Tanzania kwa msaada iliyotoa kwa nchi hizo huku wakitaja watu kwa majina.
"Jina la kwanza ni la Mwalimu (Nyerere) kisha Brigedia Jenerali Hashim Mbita na Salim Ahmed Salim, hii ni timu ya Kitanzania," anasema.
Akizidi kukazia namna walivyofanya kazi kama Watanzania, Jaji Warioba anasema hata Salim aliporudi nchini alikuja kuwa Waziri mkuu, akimtaja kwamba alikuwa ni Mzanzibari ambaye rekodi yake kama Waziri Mkuu ni kubwa na aliheshimika.
"Mwaka 2005 wakati anagombea urais, waliomshawishi walikuwa ni watu wa Bara, timu ile niliiongoza mimi, katika ile timu Zanzibar alitoka Mohamed Faki.
"Yeye (Salim) hakuwa anapenda, waliomshawishi kugombea ni watu wa Bara, walimuona ni Mtanzania safi na wakamuunga mkono, katika mchakato ule alikuwa wa pili," anasema.
Jaji Warioba anagusia pia mwaka 1985 wakati Mwalimu Nyerere anang'atuka aliyepokea kijiti alikuwa ni Ali Hassan Mwinyi, ambaye alimteua kuwa mshauri wake.
Jaji Warioba anakumbushia pia moja ya hotuba za Mwalimu Nyerere kuhusu ubaguzi, akieleza 'clip' ya hotuba hiyo kwa sasa inasambaa
"Mwalimu alisema dhambi ya ubaguzi ni kama kula nyama ya binadamu, ukishaila hutaacha, utaendelea," anasema Jaji Warioba akinukuu maneno ya Mwalimu Nyerere.
Anasema kwa Wazanzibari, baada ya kuwabagua Wabara, haitaishia hapo, watabaguana wenyewe kwa wenyewe, vivyo hivyo kwa Watanganyika nao wataanza kubaguana kwa kusema huyu wa kanda fulani na huyu ni wa kanda fulani, kisha wataingia kwenye ukabila na hata udini.