Nzega wapewa wiki mbili wanafunzi kwenda shule

Mkuu wa Wilaya ya Nzega Mkoani Tabora, Naitapwaki Tukai akizungumza kwenye kikao cha Baraza la Madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Nzega leo ijumaa Februari 3. Picha na Joseph Lyimo

Muktasari:

  • Katika Mkoa wa Tabora hadi hivi sasa ni asilimia 67.3 pekee ya wanafunzi walioripoti kuanza kidato cha kwanza kwenye shule za sekondari

Nzega. Mkuu wa Wilaya ya Nzega Mkoani Tabora, Naitapwaki Tukai ametoa muda wa wiki mbili kwa wazazi na walezi kuhakikisha wanafunzi wote wanaopaswa kuanza masomo wanakwenda shuleni mara moja.

 Tukai ameyasema hayo leo Ijumaa ya Februari 3 wakati akitoa maelekezo ya Serikali kwenye kikao cha Baraza la Madiwani wa halmashauri ya wilaya ya Nzega.

Amesema wazazi na walezi wa wilaya ya Nzega wanatakiwa kuhakikisha watoto wanaopaswa kwenda shule wanahudhuria kwani atahakikisha anasimamia hilo kwa mapana.

"Tunapaswa kuhakikisha hizi wiki mbili nilizozitoa wazazi na walezi wa wilaya ya Nzega wanazitumia kwa kuwapeleka watoto wao shule kwani elimu ndiyo msingi wa maisha," amesema Tukai.

Amesema japokuwa mkoa wa Tabora ni asilimia 67.3 pekee ya wanafunzi walioripoti kuanza kidato cha kwanza, anataka Wilaya ya Nzega ifanye vyema kwa kupeleka watoto wao shule.

Kwa upande wake Mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya Wilaya ya Nzega, Kiomoni Kibanda amesema watahakikisha wanatekeleza maagizo ya mkuu huyo wa wilaya katika kufanikisha kupeleka watoto shule.

Awali, aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Nzega Advera Bulimba ambaye amehamishiwa Wilaya ya Biharamulo mkoani Kagera amesema Nzega ina watu 592, 252.

Bulimba amesema Wilaya ya Nzega ina majimbo matatu ya uchaguzi ya Nzega mjini ya Mbunge Hussein Bashe ambaye ni Waziri wa Kilimo, Nzega vijijini ya Hamisi Kigangwalah na Bukene ya Sueiman Zedi, Halmashauri mbili za Nzega mjini na Halmashauri ya Wilaya ya Nzega, Tarafa nne Kata 46, mitaa minne na vijiji 179.