Dodoma. Utafiti uliofanywa na Taasisi ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu (NIMR) umeonyesha ukosefu wa vyumba vya kujisitiri kwa wanafunzi wa kike wakati wa hedhi shuleni, kumefanya baadhi yao kutumia vichaka.
Pia umebaini asilimia 60 ya wasichana wanashindwa kumudu gharama za ununuzi wa taulo za kike, hivyo kutumia vifaa visivyo salama kiafya.
Takwimu za Elimu Msingi (BEST) za mwaka 2022 zinaonyesha mabinti milioni 7.2 sawa na asilimia 51 ni wanafunzi wa shule za msingi na sekondari.
Utafiti huo uliofanyika mwaka 2021, uliwahusisha wanafunzi 10,516,8012 wakiwa wasichana ulifanyika katika shule 294 kwenye mikoa 16 nchini.
Akizungumza katika kikao cha kujadili mifumo wezeshi kwa wasichana kufikia haki ya elimu, Mtafiti Mwandamizi wa Afya kutoka NIMR, Dk Robert Njee amesema utafiti huo ulilenga kubaini mifumo ya wezeshi ya hedhi shuleni.
Amesema utafiti ulibaini miezi mitatu kabla ya utafiti huo asilimia 17 ya wanafunzi walikosa masomo wakati wa hedhi kwa kukosa vifaa salama vya kujihifadhi.
“Tulibaini asilimia 83 ya shule hazikuwa na vyumba maalumu kwa ajili ya kujistiri kwa watoto wa kike wakati wa hedhi,” amesema.
Amesema kutokana na kukosekana kwa vyumba hivyo, asilimia 62 ya wanafunzi hao wa kike walikuwa wakibadilishia chooni, asilimia 27 hawabadilishi, asilimia nane kwenye mabweni huku asilimia mbili wakibadilisha vichakani. Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika lisilo la kiserikali la Msichana initiative, Rebeca Gyumi amesema kukosekana kwa vifaa vya hedhi na vyumba maalumu, kunahatarisha wanafunzi hao katika kupata magonjwa ya kuambukiza.
“Suala la hedhi tunaangalia kama suala la maendeleo, la haki za binadamu lakini suala la uzazi. Tuangalia namna gani mtu anaweza kupata kwa gharama nafuu,”alisema Rebeka.
Naye Msichana kutoka wilayani Nzega, Tabora, Loveness Athumani amesema wapo wasichana hawaendi shule kwa kati ya siku tatu hadi siku saba kwa kukosa vifaa salama vya hedhi.
Ameiomba Serikali kupunguza gharama za taulo za kike, kujenga vyumba maalumu na kuhakikisha shule zinakuwa na maji ili watoto hao waweze kuhudhuria masomo kama wenzao wa kiume. Katibu wa Jukwaa la Hedhi Salama nchini (MHH), Severine Allute amesema kwenye mkutano huo wanajadili na kuangalia ni namna gani ya kupaza sauti zao kuhusu changamoto ya kukosekana kwa hedhi salama kwa wanafunzi.