Nemc yatoa kibali kudhibiti taka za kielektroniki

Muktasari:
- Mkurugenzi wa Uzingatiaji na Ufuatiliaji Sheria wa NEMC, Hamadi Taimur amesema kibali hicho kitasaidia kupunguza athari za taka hizo ambazo zina kemikali zenye madhara na hatarishi kwa mazingira na afya za watu.
Dar es Salaam. Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) limetoa kibali cha kukusanya na kusafirisha taka za kielektroniki ili kuepuka madhara zinayosababisha kwenye mazingira.
Kibali hicho cha kukusanya na kusafirisha taka za kielektroniki kimetolewa kwa kampuni ya WEEE Central Tanzania, ikiwa ni hatua ya kudhibiti madhara yanayosababishwa na taka hizo.
Akizungumzia hatua hiyo leo Mei 9, 2025, Mkurugenzi wa Uzingatiaji na Ufuatiliaji Sheria wa NEMC, Hamadi Taimur amesema kibali hicho kitasaidia kupunguza athari za taka hizo.
“Tumetoa kwa ajili ya kukusanya na kusafirisha taka hizo ili kupunguza hatari zake kwa kuwa kuzuia uingizaji wa bidhaa za kielektroniki zilizotumika ni changamoto kwa sababu zinatumika na watu wengi kutokana na hali ya kipato chao.
“Tulichofanikiwa hadi sasa ni kudhibiti taka hatarishi za hospitali kwa kuandaa taratibu za kuchoma taka za kibaiolojia, lakini kwa upande wa taka za kielektroniki bado tunaendelea kutafuta njia bora za udhibiti,” amesema.
Mkurugenzi na mwanzilishi wa WEEE Central Tanzania, Fadhil Sembago amesema hatua hiyo ni muhimu kwa kuwa Tanzania inakabiliwa na changamoto kubwa ya taka hizo.
Amesema hadi kufikia mwaka 2030, inakadiriwa nchi itakuwa inazalisha takribani tani milioni 74 za taka za kielektroniki.
“Tanzania inakumbwa na changamoto ya usimamizi wa taka hizi kutokana na ukosefu wa elimu, teknolojia na miundombinu bora. Taka za kielektroniki ni hatari na zinamgusa kila mtu kuanzia mijini hadi vijijini kwa sababu bidhaa nyingi tunazotumia ni za mitumba kutoka mataifa mbalimbali,” amesema Sembago.
Ameeleza kuwa licha ya kupata kibali cha kukusanya na kusafirisha taka hizo, bado wanakamilisha taratibu za kupata kibali cha kuzichakata ili kuongeza ufanisi wa udhibiti.
Tom Musili, mwenyekiti wa WEEE Central Kenya, amesema Tanzania ni nchi kubwa yenye watu wengi, hali inayosababisha uzalishaji wa taka za kielektroniki kuwa mkubwa na hivyo elimu kwa umma ni muhimu katika kukabiliana na changamoto hiyo.
“Kuchoma taka hizi kunasababisha madhara makubwa kwenye anga na ni hatari kwa afya, kwani watu wanavuta hewa hiyo. Ni muhimu kufuata sheria za NEMC na TCRA ili kulinda afya za Watanzania,” amesema Musili.
Ripoti ya Taifa ya Takwimu za Taka za Kielektroniki ya mwaka 2019 (NEWSR, 2019) inaonyesha kuwa kiasi cha vifaa vya kielektroniki (EEE) vilivyoingizwa sokoni Tanzania Bara, kiliongezeka kutoka tani 21,692 mwaka 1998 hadi tani 47,504 mwaka 2017.
Ongezeko hili limepelekea kuongezeka kwa uzalishaji wa taka za kielektroniki kutoka takriban tani 2,000 mwaka 1998 hadi tani 35,755 mwaka 2017.
Pamoja na ongezeko hilo, Sheria ya Kanuni ya Usimamizi wa Mazingira (Udhibiti na Usimamizi wa Taka za Vifaa vya Umeme na Elektroniki) ya mwaka 2021, kifungu cha 12(2), inazitaka mamlaka za serikali za mitaa kuhakikisha taka za vifaa vya kielektroniki zinadhibitiwa ipasavyo.
Hata hivyo, hali halisi bado hairidhishi, kwani kanuni hizo zinataka taka hizo zitenganishwe na aina nyingine za uchafu na zikakusanywe kwenye vituo vilivyoidhinishwa,suala ambalo halitekelezwi ipasavyo huku mamlaka zikihimizwa kuratibu mafunzo juu ya udhibiti wake.
Hata hivyo, sera ya urejelezaji wa taka ngumu jijini Dar es Salaam ya mwaka 2020, kifungu cha 1.2, imetaja taka za kielektroniki miongoni mwa taka zinazoweza kurejelezwa. Sera hiyo inasisitiza kuwa “kurejelezwa kwa taka husaidia katika kulinda rasilimali.”