Ndege mpya ya mizigo kuibeba ATCL

Muktasari:
- Ndege hiyo itakayokuwa na uwezo wa kubeba tani 54 kwa safari moja, inatarajiwa kuondoa adha ya wafanyabiashara wanaosafirisha bidhaa nje ya nchi, kukosa nafasi kwenye ndege za abiria.
Dar es Salaam. Shirika la Ndege la Tanzania (ATCL) limesema ujio wa ndege ya mizigo ifikapo Aprili utaiwezesha kubeba mizigo hadi tani 3,000 kwa mwaka na kuondoa adha ya wafanyabiashara waliokuwa wakipeleka mizigo yao nje ya nchi.
Akizungumza na waandishi wa habari wakati wa mkutano na wadau wa usafirishaji wa mizigo kwenda nje ya nchi leo Machi 20, Mkurugenzi wa ATCL, Ladislaus Matindi amesema ndege hiyo itakayoingia nchini Aprili ina uwezo wa kubeba tani 54 kwa safari moja.
“Tumekuwa tukitumia ndege za abiria, sasa kidogo ina changamoto kwa sababu haitupi nafasi ya kutosha kusafirisha mizigo.
“Lakini baada ya kupata ndege maalum ya kusafirisha mizigo itakayokuja mwanzoni au mwishoni mwa mwezi ujao aina ya Boing 767 itatatua changamoto hii,” amesema.
Amesema lengo la mkutano waliofanya jana ni kuwasikiliza wadau wakiwamo wasafirishaji wa mizigo na taasisi za Serikali.
“Tumeona watu wasikilize changamoto zetu, tunasafirishaje, changamoto ni zipi? Ili tuhakikishe mizigo iliyokuwa ikipitia nchi nyingine isafirishwe moja kwa moja kutoka Tanzania.
“Ndege inayokuja itakuwa na uwezo wa kubeba tani 54. Tunazungumzia soko kubwa la China na India na masoko makubwa yanayozyunguka yanayotegemea bandari zetu kama Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), Zambia, Zimbabwe na Comoro.
“Mwaka uliopita tumesafirisha tani 2,600, hilo ni ongezeko kubwa maana tulipoanza mwaka 2017 tulikuwa tunasafirisha tani 350 hivi, tunahakika kwa mwaka huu tutakwenda zaidi ya tani 3000,” amesema.
Kwa upande wake Msajili wa Hazina, Nehemia Mchechu aliyefungua mkutano huo, amewaambia waandishi wa habari kuwa uwekezaji unaofanywa na Serikali kwa ATCL unalenga kukuza uchumi.
“Uwekezaji huu umekuja wakati mwafaka kipindi ambacho Serikali ya awamu ya sita imejikita katika ukuaji wa uchumi, ukiangalia ukuaji wa GDP (pato la ndani) unakwenda vizuri, ukiangali uwekezaji unakwenda vizuri, ukiangalia imani ya watu hususani wawekezaji imekuwa nzuri,” amesema.
Akizungumzia ujio wa ndege hiyo, Amani Temu ambaye ni Meneja Mkuu wa kampuni ya Taha Fresh Ltd alisema changamnoto ambayo wamekuwa wakiipata ya ukosefu wa nafasi kwenye ndege zinakosa abiria, sasa inakwenda kwisha.
“Tunashukuru Serikali imesikia kilio chetu na inaleta ndege ya mizigo, tunategemea kuitumia kwa sababu itatoa suluhisho,” amesema.
Naye Samira Abdallah Suleiman kutoka kampuni ya kusafirisha mizigo, Express Cargo Services amesema changanoto walizokuwa wakizipitia ni ukosefu wa ndege kusafirisha mizigo.
“Unakuta tuna mzigo wa tani mbili au tatu, lakini ndege inayokuja inachukua kilo 400 au 500, inakuwa changamoto kwetu na wateja wetu,” amesema.