Mvua zaharibu miundombinu Lindi, Serikali yatoa Sh5 bilioni za ukarabati

Meneja wa Tanroad ,mkoa wa Lindi Mhandisi Emily Zengo
Muktasari:
- Mabadiliko ya tabia ya nchi, imetwaja kuwa sababu kubwa ya kuleta athari ya kuharibika kwa miundombinu hasa kwa mkoa wa Lindi kutokana na mvua zinazoendelea kunyesha.
Lindi. Mvua kubwa zinazoendelea kunyesha mkoani Lindi zimesababisha uharibifu mkubwa wa miundombinu, hasa barabara na madaraja, hivyo kusababisha kero kwa wananchi kutokana na kukatika kwa mawasiliano.
Akizungumza na Mwananchi leo Aprili 12, 2024 kuhusu jambo hilo, Meneja wa Wakala wa Barabara nchini (Tanroads) Mkoa wa Lindi, Mhandisi Emily Zengo amesema mvua zinazoendelea kunyesha zimesababisha barabara kukatika na madaraja kubomoka.
“Mkoa wa Lindi upo chini, maji yanayotoka sehemu mbalimbali kama Liwale, Ruangwa na maeneo mengine. Maji yake yote yanakuja huku na kuingia baharini, kwa hiyo, sisi tuliokuwa katika wilaya hizi ambazo tupo karibu na bahari lazima tupate madhara ya mafuriko na kuharibika kwa miundombinu,” amesema Mhandisi Zengo.
Mhandis Zengo amesema kuharibika kwa miundombinu ya madaraja na kukatika kwa mawasiliano ya barabara, baadhi ya maeneo ya mkoa wa Lindi, Serikali imetoa Sh5 bilioni kwa ajili ya matengenezo ya dharura kwa maeneo yaliyoharibiwa na mvua.
“Serikali imetoa Sh5 bilioni kwa ajili ya matengenezo ya dharura kwa barabara zilizoathiriwa na mvua zinazoendelea kunyesha kutokana na mabadiliko ya tabianchi ambapo matengenezo ya miundombinu bado yanaendelea,” amesema Mhandisi Zengo.
Meneja huyo ameteja maeneo ambayo matengenezo ya barabara yanaendelea kwa fedha hizo za dharura kuwa ni pamoja na boksi karavati la Mto Mbwemkuru, barabara ya Nangurukuru-Liwale, Liwale – Nachingwea na barabara ya Tingi – Kipatimo.
“Tunaishukuru Serikali kwa kutuletea fedha za dharura na sisi kama watendaji wa Serikali, tutahakikisha wananchi wanaendelea kutumia barabara hizi kipindi chote,” amesema Mhandisi Zengo.

Mkazi wa Kipatimo, Hamisi Juma amesema mvua nyingi zinazonyesha katika mkoa wa Lindi ni lazima zilete madhara, wanaishukuru Serikali kwa juhudi za haraka wanazozifanya pindi inapotokea changamoto hasa ya barabara.
“Namshukuru Rais Samia kwa juhudi anazofanya pindi anaposikia kumetokea tatizo sehemu, barabara yetu ni ya muda mrefu sana na ni korofi, kila mwaka mvua zinaponyesha kupita inakuwa shida, lakini kwa uongozi wa Rais Samia barabara inatengenezwa, tunamshukuru sana Rais kwa kutenga fedha za dharura kutengeneza barabara ya Tingi – Kipatimo,” amesema.
Mkazi wa manispaa ya Lindi, Mwanahawa Bakari amesema Serikali Kuu na Serikali ya Mkoa, inafanya jitihada kubwa kuhakikisha wananchi wake wanaendelea kufanya shughuli zao kila siku, licha ya miundombinu kuharibika.
“Daraja la Mto Mbwemkuru linalounganisha wilaya za Kilwa na Lindi, lilikuwa linatitia lakini wakandarasi wetu wamejitahidi haraka kurudisha mawasiliano kwa kutengenezeza barabara mbadala, ili shughuli za kijamii zisikwame. Kiukweli mimi binafsi namshukuru Rais Samia kwa kutenga fedha kwaajili ya dharura,” amesema Mwanahawa.
Hata hivyo, miradi yote ya matengenezo inatekelezwa na wakandarasi wazawa zaidi ya wakandarasi 40 waliofanya kazi kwa kipindi cha miaka mitatu na zaidi Sh40 bilioni zililipwa kwa wakandarasi hao.