Mvua yasababisha adha Dar, wananchi wakwama

Muktasari:
- Baadhi ya wakazi wa Dar es Salaam wameshindwa kutoka makwao kwenda kwenye shughuli zao kutokana na mvua zilizonyesha usiku wa kumkia leo.
Dar. Mvua zilizoanza kunyesha usiku wa kuamkia leo Jumatatu, Aprili 14, 2025 maeneo mbalimbali ikiwemo jijini Dar es Salaam imesababisha adha kwa wakazi wa Jiji hilo.
Mvua hizo zinanyesha maeneo mbalimbali ya jiji hilo ambalo ni kitovu cha uchumi wa Tanzania na kusababisha adha, baadhi ya makazi kuzungukwa na maji, njia za kupita kwenye makazi kujaa maji.
Baadhi ya wananchi wameshindwa kutoka makwao kwenda kwenye shughuli zao kutokana na mvua hizo. Foleni nayo kwa baadhi ya barabara imeshika kasi.

Utabiri wa hali ya hewa uliotolewa jana Jumapili na Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA), unaonesha mvua hizo zinanyesha leo Jumatatu maeneo mbalimbali ya Dar es Salaam, Tanga, Morogoro, Pwani, Lindi, Mtwara na visiwa vya Unguja na Pemba.
TMA ilieleza kuwa kutokana na mvua hizo kubwa, kuna uwezekano wa kutokea kwa athari kwa baadhi ya makazi kuzungukwa na maji
Utabiri huo wa TMA unaonesha kwa kesho Jumanne hadi Alhamisi ya Aprili 17, 2025 hakutakuwa na tahadhari yoyote ya mvua nchini.

Mvua hizo zimesababisha adha kubwa kwa wakazi wa maeneo ya Tabata Segerea kutokana na kukosekana kwa usafiri wa pikipiki na daladala.
Katika kituo cha Segerea Mwisho kuanzia saa moja asubuhi mpaka saa tatu asubuhi kulikuwa na abiria wengi ambao walijazana katika vituo wakijikinga mvua kutokana na mzunguko mdogo wa daladala kituoni hapo.

Hata hivyo baadhi ya barabara za kuingia katika mitaa mbalimbali zimejaa maji, hali iliyosababisha nyingine kutopitika kutokana na utelezi.
Baadhi ya mitaro iliyo barabarani nayo ilionekana kujaa maji, kutokana na kuziba katika maeneo ya Tabata Liwiti.

Mkazi wa Kimara, Dar es Salaam, Issihaka Said amesema mvua hizo zimesababisha baadhi ya barabara hasa za mitaa zishindwe kupitika kwa gari na pikipiki, kutokana na utelezi.
“Kila wakati njia hizo zinachongwa na mvua zinaponyesha zinaharibika, hayakuwahi kufanyika matengenezo ya kudumu, zinatengenezwa ilimradi,” amesema Said.Utu Khamis, Mkazi wa Chanika na mfanyabiashara wa samaki, amesema ameshindwa kwenda kununua samaki Feri kutokana na mvua hizo.
"Maeneo ninayokaa mvua ikinyesha siku mbili mfululizo maji huwa yakijaa kwenye barabara tunayotumia ambapo huwezi kupita na leo ndio yamezidi kabisa kwa kuwa mvua imenyesha usiku kucha na tumeamka nayo," amesema Utu.

Laurance Mbise, mwendesha bodaboda amesema leo kazi kwake imekuwa ngumu kwa kuwa watu wengi hawajatoka kwenda kazini.
"Siku za kazi kama leo nimezoea napigiwa simu na abiria hata 10 mpaka wengine nawaomba wenzangu wakawachukue. Lakini leo sijapata simu hata moja na siwezi kutoka kwenda kijiweni kunyeshewa zaidi ya kusubiri kupigiwa simu ndio nitoke," amesema Mbise.
Asnat Hamza, mkazi wa Homboza, amesema:"Niliamka asubuhi kujiandaa kwa ajili ya kwenda kazini, lakini nimeshindwa kutoka kwani kila nikisubiri labda mvua itakata lakini wapi, nimeisubiri zaidi ya saa tatu ikabidi nivue tu nguo niendelee na shughuli za nyumbani," amesema.
Endelea kufuatilia Mwananchi