Mtwara inaongoza malaria nchini

Mratibu wa Malaria Mkoa wa Mtwara Dokta Kanuda Nswila akizungumza na Waandishi wa habari hawapo pichani katika mafunzo yaliyoandaliwa na Mradi wa Dhibiti Malaria uliopo chini ya Mpango wa kitaifa wa kudhibiti Malaria, kwa kushirikiana na uongozi wa afya wa Mkoa wa Mtwara kwa hisani ya watu wa Marekani. Picha na Florence Sanawa
Muktasari:
- Asilimia 20 watu waishio katika mkoa wa Mtwara wana maambukizi ya ugonjwa wa malaria ambapo kati ya watu 100 watu 20 wana ugonjwa huo.
Mtwara. Inaelezwa kuwa maambukizi ya ugonjwa wa Malaria kwa Mkoa wa Mtwara yapo juu, ambapo katika watu 100, watu 20 hubainika kuwa na ugonjwa huo huku Wilaya ya Tandahimba ikitajwa kukithiri kwa maambukizi ya ugonjwa huo.
Wilaya ya Tandahimba inatajwa kuongoza katika maambukizi ya ugonjwa wa malaria ambapo kati ya watu 100, watu 47 hubainika kuwa na maambukizi ya ugonjwa huo.
Akizungumza katika mafunzo ya siku mbili ya wanahabari mkoani hapa yaliyoandaliwa na Mradi wa Dhibiti Malaria uliopo chini ya Mpango wa kitaifa wa kudhibiti Malaria, Mratibu wa Malaria Mkoa wa Mtwara Dk Kanuda Nswila alisema kuwa hali ya ugonjwa huo ni mbaya kwa Mtwara.
“Unajua kiwango cha maambukizi kwa Mtwara kipo kwa asilimia 20 yaani ukichukua watu 100 ukiwapima unapata wagonjwa 20 wenye ugonjwa huo shida kubwa ni elimu kuhusu malaria bado iko chini, tunakiri elimu juu yakudhibiti mbu bado iko chini,” amesema.
Dk Nswila amesema kuwa mwananchi anapokuwa na elimu ndogo kuhusu malaria ni shida kukabiliana na ugonjwa huo kwani anapougua hukimbilia hospitali kwa matibabu huku akiishi katika mazingira yanayofuga mazalia ya mbu.
“Usafi wa mazingira ni muhimu ili tuondokane na tatizo la mazalia ya mbu kwani kwani kinyume chake unahifadhi mazalia ya mbu. Unaweza kutibu malaria lakini kama unaishi katika mazingira hatarishi madibabu haya yatakuwa ni kwa muda muda tu,” alisema Dr Kanuda
Kaimu Muuguzi Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Mtwara Martha Lendena amesema kuwa wauguzi hupata changomto kubwa wakati wa kuwahudumia wagonjwa wa malaria ambapo hufika kutibiwa wakati ungonjwa wakati mwingine uko hatua ya mwisho.
“Kwa kweli tunapata changamoto kubwa yaani wagonjwa wa malaria huja katika hatua ya mwisho ambayo ni dalili za hatari ambapo inawalazimu kupelekwa kitendo cha wagonjwa mahututi (ICU) kwa ajili ya hupata huduma za uokozi kabla kuwahamishia wodi za kawaida” alisema Lendena.