Tanzania yasaini mkataba kupambana na malaria

Waziri Ummy Mwalimu (kushoto) akisaini hati ya makubaliano na kampuni ya SCJohnson kupambana na ugonjwa wa Malaria nchini
Dar es Salaam. Wakati Serikali ikiendelea kupambana na ugonjwa wa malaria, Wizara ya Afya imesaini hati ya makubaliano ya kushirikiana na Kampuni ya SCJohnson iliyopo Marekani kwa lengo la kupambana na ugonjwa huo.
Makubaliano hayo yalisainiwa jana, Aprili 2, 2023 yakihudhuriwa na Makamu Mtendaji wa Rais wa Shirika hilo, Mark Martin, Balozi wa Umoja wa Viongozi wa Nchi za Afrika dhidi ya Malaria (ALMA), Anthony Okara pamoja na Mwenyekiti Mteule wa Baraza la kutokomeza ugonjwa huo nchini, Mhandisi Leodgar Tenga.
Kampuni hiyo kwa kushirikiana na Wizara ya Afya wamesaini hati ya kuwasaidia wananchi wa Tanzania katika kupambana na ugonjwa wa malaria.
Hayo yalifanikiwa kufuatia ziara ya Rais Samia Suluhu Hassan aliyoifanya kwenye makao makuu ya kampuni hiyo yaliyopo Racine, Winscosin nchini Marekani Mei 2022.
Waziri Mkuu Kasim Majaliwa wakati akizindua mbio za Mwenge wa Uhuru, alieleza kuwa wataendelea kuelimisha watu juu ya ugonjwa wa malaria kwa sababu inaendelea kuathiri afya za Watanzania.
Mbali na hayo, Waziri Mkuu aliendelea kueleza kuwa ugonjwa wa malaria umepungua kwa kiwango cha asilimia 45 kutoka asilimia 14.8 ya mwaka 2015.
“Mwaka 2015 kulikuwa na asilimia 14.8 ya ugonjwa wa Malaria, hivyo hadi kufikia mwaka 2022 ugonjwa huo umepungua kwa asilimia 8.1,” amesema.
Aidha, Waziri Mkuu alitaja mikoa inakabiliwa na ugonjwa wa malaria nchini ambayo ni Tabora kwa asilimia 23.4, Mtwara asilimia 19.7, Shinyanga asilimia 15.6, Mara asilimia 15.1 na Kagera asilimia 17.5.
Waziri Mkuu amewaomba wananchi kushiriki katika mbinu mbalimbali za kupambana na ugonjwa wa malaria ili kuinua nguvu kazi nchini na kuongeza uchumi wa Taifa kwa manufaa yao.
“Tushiriki kikamilifu katika kuangamiza viluilui vya mbu kwa kutumia viua wadudu vya kibailojia, tusiruhusu maji kutuama,tutumie vyandarua vyenye dawa ili kujikinga na mbu waenezao malaria, pia wajawazito wapewe vyandarua bure na kauli mbiu ni ziro malaria inaanza na mimi,” amesema.