Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Mkojo wa ngombe udhibiti malaria-IHI

Dar es Salaam. Katika kukabiliana na ugonjwa wa malaria, wanasayansi wamependekeza matumizi ya harufu ya mkojo wa ng’ombe kama njia rahisi na nafuu ya kudhibiti vimelea vya mbu wanaoeneza ugonjwa huo.

Pendekezo hilo ni kwa mujibu wa ripoti ya wanasayansi sita kutoka ndani na nje ya nchi, wakiwemo Dk Nicodem Govella, Godfrey Katusi na Samwely Makayula kutoka Taasisi ya Afya Ifakara (Ihi).

Wataalamu wengine ni Dk Ladslaus Mnyone kutoka Chuo Kikuu cha Sokoine Morogoro (Sua), Profesa Rickard Ignell na Dk Sharon Hill wote kutoka Chuo Kikuu cha Sayansi ya Kilimo cha Sweden (SLU).

Katika utafiti huo waliouita ‘Umbali kutoka makazi ya binadamu unaathiri kwa njia tofauti ufanisi wa kivutio cha harufu ya mkojo wa ng’ombe ili kunasa waenezaji wa malaria,’ wanatetea matumizi ya mbinu hiyo kama nyongeza ya ufuatiliaji na udhibiti wa vijidudu vya malaria.

Kulingana na ripoti hiyo, Tanzania kwa sasa imekosa zana madhubuti za ufuatiliaji na udhibiti wa mbu waenezaji wa malaria na kwamba, kilichofanyika ni kutathmini ufanisi wa dawa hiyo katika kuwavutia wadudu wanaoeneza ugonjwa huo.

“Tathmini ya mbinu hii imefanyika kwa takriban miaka mitano kwa muundo wa kilatini,” inasomeka sehemu ya ripoti hiyo.

Inaongeza kuwa; “Kila mtego uliwekwa na dozi moja kati ya nne za mchanganyiko wa harufu ya mkojo wa ng’ombe au kidhibiti cha kutengenezea (heptane). Mitego ilizungushwa kwa siku 20 za majaribio.”

Kutokana na mtego huo, takriban mbu 1,568 walipatikana kupitia mtego huo, kati yao 783 walikuwa anofelesi na 785 ni culicines.

Katika idadi hiyo ya anofelesi asilimia 41.6 na 58.3 walikuwa vyanzo vya awali vya usambazaji wa vimelea vya malaria.

Hata hivyo, utafiti huo ulibaini mbu jike aina ya Anofelesi arabiensis, walikamatwa karibu na makazi ya watu (mita 1.5) na wengine walikamatwa umbali wa mita tano kutoka katika makazi ya watu.

Malaria inaendelea kuwa janga kubwa nchini, Taasisi ya Afya ya Ifakara inasema Tanzania kwa sasa inatekeleza ufuatiliaji wa malaria (TMSA) wa miaka mitano kati ya Agosti 2022 hadi Agosti 2027, wenye lengo la kupunguza ugonjwa huo na kuutokomeza kabisa.

Mpango mpya wa miaka mitano wa kupambana na malaria Tanzania Bara na Zanzibar, unalenga kuharibu mazalia ya mbu na waenezaji wa vimelea vya ugonjwa huo.

Kwa mujibu wa ripoti ya dunia ya ugonjwa huo mwaka jana, inakadiriwa kuwa Tanzania ni miongoni mwa nchi 10 zenye wagonjwa na vifo vingi vya malaria, ikiwa ni asilimia tatu ya wagonjwa wote duniani na asilimia 4.1 ya vifo duniani.

Kulingana na ripoti hiyo, karibu asilimia 80 ya vifo vyote vinavyotokana na malaria viliwatokea watoto wenye umri chini ya miaka mitano.

Nchini Tanzania, Malaria huenezwa zaidi na mbu aina ya Anopheles gambiae complex na funestus.