Mnada zao la korosho kuanza Oktoba 21

Kaimu Mrajis wa Vyama Vikuu vya Ushirika Mkoa waLindi ,Cesilia Sositenes, akiongea jambo na waandishi wa habari (Hawapo pichani). Picha na Bahati Samwel
Muktasari:
- Wakati mnada wa kwanza wa msimu wa zao la korosho wa 2023/2024 ukitarajiwa kuanza rasmi October 21 mwaka huu, Chama Kikuu cha Ushirika Lindi, Mwambao kimeandaa mafunzo kwa viongozi wa Amcos ili kuwajengea uwezo na uwajibikaji katika nafasi zao kutokana na kile kilichoelezwa kuwa baadhi yao kutokuwa waaminifu katika nafasi zao kwenye kusimamia mazao ya wakulima.
Lindi. Katika kujiandaa na mnada wa kwanza wa msimu wa zao la korosho kwa mwaka wa fedha 2023/2024 unaotarajiwa kuanza rasmi Oktoba 21, Chama Kikuu cha Ushirika Lindi, Mwambao kimeandaa mafunzo kwa viongozi wa Amcos ili kupambana na uadilifu kwa makarani hao.
Akizungumza leo Jumapili October 8, 2023 Kaimu Mrajisi wa Vyama vya Ushirika Mkoa wa Lindi, Cesilia Sositenes, amesema lengo la kuwapati mafunzo hayo ni kuwaandaa viongozi kuelekea kwenye msimu wa korosho kwani viongozi walio wengi hawana uadilifu na sio wawajibikaji kwenye nafasi zao.
Amesema kuwa msimu uliopita wa ufuta na mbaazi kulikuwa na changamoto ndogo ndogo ambazo zilisababishwa na baadhi ya viongozi wa amcos kutokuwajibika ipasavyo katika maeneo yao.
"Baadhi ya viongozi na makarani sio waaminifu kabisa kutokana na changamoto hizo, ndio maana chama kikuu cha Lindi Mwambao wameamua kutoa mafunzo kwa viongozi ili kuepuka changamoto kama hizo kuja kujitokeza tena kwenye msimu wa mwaka huu," amesema Cesilia.
Naye Mkurugenzi wa bodi ya Korosho Tanzania, Alfred Fransis amesema msimu unapoanza wakulima wanatakiwa kukusanya korosho zote zenye ubora ili kuimarisha mnyororo wa thamani kwani soko kubwa la korosho lipo India na Vertinamn na kuwausia wakulima kujitahidi katika ubora kwavile nchi nyingi kwa sasa zinalima korosho.
"Tunaelekea kwenye msimu wa korosho niwaombe wakulima na viongozi wa Amcos tujitahidi kukusanya korosho ambazo zina ubora na kuzipeleka ghalani, kwa kufanya hivyo korosho yetu itapanda thamani na kupata bei nzuri kwenye soko la India na Vertinamn,” amesema Alfred.
Kwa upande wake Makamu Mwenyekiti wa Chama Kikuu cha Ushirika Lindi Mwambao, kinachaounganisha Halmashauri tatu ikiwemo ya Kilwa, Mtama pamoja na Manispaa ya Lindi, Yassin Hashim amesema mafunzo hayo wameyaandaa ili kuwajengea uwezo viongozi wao wa Amcos ili kujiweka sawa na msimu wa korosho unao anza October 21.
"Kila msimu wa mazao unapoanza lazima tuwape mafunzo viongozi wetu wa Amcos kwakuwa wale ndio wanaopokea mazao ya wakulima kutoka kwenye vyama vyao vya msingi na kupeleka ghala kuu,” amesema Hashim.
Mjumbe wa Amcos ya Mmanga Manga, Hawa Matingo amesema kuwa mafunzo waliyoyapata yatawasaidia ipasavyo kwa kufanya kazi kwa uwajibikaji na kuondoa changamoto ambazo zilijitokeza kwenye msimu uliopita wa ufuta baada ya baadhi ya wakulima kupeleka ufuta mchafu na viongozi ambao sio waadilifu waliupokea bila kuwa na mashaka.
"Mafunzo haya yatatusaidia sisi viongozi na tutajitahidi kuondoa changamoto zote zilizokuwa zimejitokeza wakati wa msimu wa ufuta, kikubwa niwaombe wakulima wajitahidi kupeleka korosho zilizokauka kwenye Amcos zetu ili na sisi tusipate kazi kubwa ya kuzianika tena," amesema Hawa.