Mkurugenzi atangaza kuvunja makundi ya WhatsApp

Muktasari:
Mwaka mmoja baada ya watahiniwa wa darasa la saba kufutiwa matokeo ya mitihani na Baraza la Taifa la Mitihani (Necta) Wilaya ya Chemba mkoani Dodoma, Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo ametangaza kuchukua hatua kali za kinidhamu kwa waratibu elimu msingi watakaoendelea kutumia makundi ya WhatsApp katika kuwasiliana.
Dodoma. Halmashauri ya Wilaya ya Chemba mkoani Dodoma nchini Tanzania imevunja makundi yote ya ‘WhatsApp’ ya waratibu elimu msingi ili kuepuka udanganyifu katika mitihani ya darasa la saba inayofanyika kesho na keshokutwa.
Akizungumza leo Jumanne Septemba 10, 2019 na Mwananchi, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo (DED), Dk Semistatus Mashimba amesema hatua hiyo imechukuliwa kuepuka yaliyojitokeza mwaka 2018 ambapo shule za wilaya zote zilifutiwa matokeo ya mitihani ya darasa la saba.
“Last time magroup haya yalitumika haya magroup katika kuwasiliana. Tumeandika barua kuwataka wavunje hayo magroup, ni kwa waratibu wa elimu tu si kwa watumishi wengine,” amesema.
Katika barua hiyo iliyoandikwa kwa waratibu kata elimu wote Agosti 19, 2019 na kusainiwa na Josephat Ambilikile kwa niaba ya mkurugenzi wa halmashauri hiyo imewataka waratibu elimu kata wote kuvunja makundi hayo.
Makundi hayo ni yale yanayotumika kutoa au kupokea taarifa zozote zinahusiana na utendaji wa taaluma.
Ambilikile amesema pia ofisi imebaini kuwepo kwa makundi ya WhatsApp katika halmashauri hiyo yanayotoa taarifa mbalimbali za kielimu na kijamii.
Ameyataja makundi hayo ni ya walimu wakuu waliovuliwa madaraka na walimu wakuu wapya, walimu wakuu waliopo madarakani, maofisa elimu kata na walimu wakuu ngazi ya kata na wilaya na mengineyo yanayofanana na hayo.
“Hatua kali za kinidhamu na kisheria zitachukuliwa dhidi ya kiongozi wa kundi Sogozi (WhatsApp) na wanachama wa kundi husika,” amesema.