Mikopo umiza balaa, Gavana atoa tahadhari
Nani anakopa nini?
Akichangia mada hiyo, mhariri wa takwimu wa gazeti la Mwananchi, Halili Letea alisema Watanzania wengi wanaochukua mikopo hutumia fedha katika shughuli zisizo za uzalishaji, hivyo kuwawia vigumu katika urejeshaji.
Alisema ripoti ya utafiti wa ufuatiliaji wa kaya uliotolewa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS), iliyoonyesha matokeo ya namna Watanzania wanatumiaje fedha baada ya kukopa, asilimia 26.4 pekee ndio wanakopa kwa ajili ya kufanyia biashara.
“Asilimia 31.8 wanakopa kufanya matumizi ya kawaida kwa maana ya kununua chakula, asilimia 13 wanakopa kwa ajili ya elimu, yaani kulipa ada, asilimia 12.4 sawa na mtu mmoja kati ya 8 wanakopa kwa ajili ya matibabu, asilimia 11.7 kwa ajili ya kulipa kodi na kujikidhi kwenye makazi na asilimia 8.5 ni wakulima wanakopa kwa ajili ya kununua mbegu,” alisema Letea.
Waziri Kivuli wa Uchumi na Fedha wa Chama cha ACT Wazalendo, Ester Thomas alisema ni muhimu wananchi kuwezeshwa kupata mikopo ya halmashauri ambayo haitakuwa na riba.
Alisema mikopo hiyo maarufu kama ya asilimia 10 ipelekwe kwenye mifuko ya hifadhi ya jamii na itakwenda kumwezesha Mtanzania kuanzisha biashara na kuepukana na mikopo ya kausha damu.
Alichokisema Gavana
Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Emmanuel Tutuba alisema wananchi wanatakiwa kuwa makini na taasisi ndogo za ukopaji.
Alisema taasisi hizo zimegawanyika katika makundi matatu--- zile za ngazi ya jamii (vicoba), ngazi ya vyama vya ushirika (Saccos) na kampuni au mtu binafsi ambazo haziruhusiwi kukusanya dhamana.
Tutuba alisema kuna vigezo wameviweka ambavyo kwanza ni asajiliwe na Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (Brela), huku akieleza inapaswa kuwa taasisi inayotambulika na kufahamika.
“Lazima awe na ofisi na chumba wanachotolea mikopo, ili mtu akiwa na malalamiko anatakiwa kuyaleta na wayafanyie kazi na benki wanapopita kukagua wayakute na waanze kufuatilia,” alisema.
Gavana huyo alisema kigezo kingine ni lazima wawe na mtaji kuanzia Sh20 milioni hadi Sh20 bilioni na zaidi ya hapo, anapotoa huduma anatakiwa awe na andiko la kisera linaloelezea huduma anazotoa.
Alisema kwa wale wenye kampuni, wakisoma kwenye sheria ya makampuni, kuna kitu kinaitwa mkataba na vifungu vya ushirika.
“Kupitia mkataba huo anatakiwa aeleza anatoa mikopo na anaendesha shughuli gani za halali zinamfanya asajiliwe kama kampuni,” alisema.
Tutuba alieleza hata wakati wanapowasilisha maombi, ni lazima aonyeshe huduma atakazozitoa na sera yake. Pia atoe taarifa, kufunga hesabu na kulipa kodi.
Alisema baada ya kujisajili ndipo taasisi hiyo inatoa leseni ambayo kunakuwa na masharti.
“Unatakiwa kutoa mikopo riba isizidi asilimia 3.5 kwa mwezi. Kuna baadhi wanavuka kiwango hicho na wengine unakuta hata hawajasajiliwa,” alisema.
Alisema bahati mbaya watu na baadhi ya wafanyabiashara wakitangaziwa sehemu kuna mikopo wanajipeleka bila kuulizia na kujua masharti yake.
“Tunatoa leseni na tunawataka waweke hadharani masharti kusudi mtu anayeenda kukopa ajue riba ni kiasi gani na anavyokopa atakaporejesha ni kiasi gani,” alisema.
Tuzo Mapunda, Elizabeth Edward na Devotha Kihwelo