‘Mikopo kausha damu ni rahisi lakini inadhalilisha’

Muktasari:
- Kampuni ya Mwananchi Communications Limited imeendesha mijadala wa TwitterSpace wenye mada ‘ongezeko la taasisi za mikopo nchini, ni fursa au changamoto kwa jamii?’ na kushirikisha wadau mbalimbali.
Dar es Salaam. Mwandishi wa Gazeti la Mwananchi, Elizabeth Edward amesema taasisi za mikopo kwenye jamii zina faida na hasara zake.
Amesema wakati benki zikisubiri wakopaji lakini watu wamekuwa wakitumia taasisi hizo za mitaani kutokana na ufikiwaji wa kirahisi.
Elizabeth amesema hayo leo Jumatano, Julai 12, 2023, wakati akichokoza mada ya TwitterSpace ya Mwananchi yenye mada ‘ongezeko la taasisi za mikopo nchini, ni fursa au changamoto kwa jamii?’
Amesema mikopo yao inapatikana kwa urahisi, unaweza kwenda leo na ukarudi na fedha zako kwahiyo hiyo inaweza kuwa fursa kwa mtu mwenye shida ya haraka.
“Lakini upande wa pili inaweza kuwa changamoto kwasababu taasisi nyingi riba ni kubwa, kweli ni rahisi kupata mikopo lakini riba ni kubwa na masharti yake yanaumiza na ndio maana inaitwa mikopo kausha damu.
“Mfano mtu anakopa Sh100,000 na riba Sh30,000 huku unatakiwa kurejesha kila siku ndani ya mwezi mmoja, sasa tukiangalia wanaokopa ni watu wa hali ya chini sasa kama umekopa Sh50,000 kila siku unaambiwa ufanye rejesho,” amesema Elizabeth
Amesema kwahiyo masharti yanayoendana na hii mikono ni changamoto kwenye jamii, utakuta vitu ambavyo watu wanaweka dhamana kupata huo mkopo mfano umeweka dhamana friji kwa mkopo wa Sh100,000 ukishindwa kulipa huo mkopo unakosa friji yako.
Elizabeth amesema kuna baadhi ya mikopo kwenye jamii, mama anakopa baba hajui, labda anashughuli ya rafiki yake anataka kukopa akaonyeshe ana kitu.
Amesema kuna watu wanalazimika kukopa kwa ajili ya kusomesha, unakuta mtu anakwenda kuchukua kausha damu ili mtoto aendelee na shule sasa kurejesha huo mkopo ndio shughuli.
Amesema kama umeweka dhamana televisheni alafu umeshindwa kurejesha watu wanakuja kuchukua. Kwahiyo kuna migogoro ndani ya ndoa inatokea kwasababu ya hii mikopo kausha damu, mtu anakopa anakwenda kununua nguo.
“Mbagala kuna madalali wanauza vitu vilivyokombolewa kwenye mikopo, mkopo umeshindwa kulipa watu wanauza nguo zako jambo ambalo ni udhalilishaji,” amesema
Naye Ben Bella akichangia mada hiyo amesema, “tassisi za mitaani zinakuambia zinatoza asilimia 40 ya fedha unazochukua na baadaye mnakubaliana mnalipa kwa muda gani, huyu mtu ni rahisi kwasababu mfumo wake ni mzuri ameniongezea asilimia 40 inayoeleweka.”
“Benki unaambiwa asilimi 17 ya fedha unayochukua, unaweza kukopa milioni tatu unaambiwa ulipe milioni 12. Mikopo ya mitaani inauma lakini ya benki inaumiza zaidi riba ni kubwa,” amesema
Hata hivyo, Sheria ya biashara ya fedha ‘The Microfinance Act 2018’ inatoa katazo kufanya biashara ya fedha kwa kutoza riba bila kuwa na leseni. Kifungu cha 16 cha sheria hiyo kinatoa adhabu ya kifungo kisichopungua miaka miwili na kisichozidi miaka mitano kwa anayekiuka sheria hiyo.