Usiruhusu mafanikio yavunje ndoa

Muktasari:
Hiki ni kisa cha mwanamama aliyepata uheshimiwa, ukawa sababu ya kuvunja ndoa yake.
Canada. Kuna kisa cha mama mmoja aliyeukwaa uheshimiwa. Tulipata kisa hiki kwenye pitapita zetu kwenye taarifa za mitandaoni na kuthibitisha kuwa ilikuwa ni stori ya kweli.
Tulidurusu na kujua hata jimbo analotoka katika mkoa mmoja wa Kanda ya Ziwa. Huyu mama, kwa kusaidiwa na mumewe, alitumia rasilimali za familia kuukwaa uheshimiwa ambao, hata hivyo, uliishiwa kuwa ‘uhishiwa’. Hii ni kutokana na kuvurunda na kuivunja ndoa yake baada ya ukubwa kumpanda kichwani.
Baada ya kujaa mjengoni, kwanza, mama alianza kuzinyaka na kuuonja unono na utamu wa ukubwa. Mshahara alipata si haba tena kwa mamilioni. Milioni tano kwa mwezi mbali na marupurupu lukuki kiasi cha kuondoka na si chini ya milioni kumi kwa mwezi.
Pili, alianza kwenda ughaibuni akiandamana na waheshimiwa wenzake wa kiume na maofisa wakubwa wakubwa wa Serikali.
Huko, walikaa kwenye mahoteli ya bei mbaya wakila na kunywa na kulala pamoja. Ghafla, uzalendo ulimshinda. Alianza uhusiano usio na heshima na waheshimiwa wenzake.
Walipika na kupakua kiasi cha kunogewa. Jambo hili, lilimsababisha kutokuwa na hamu na mumewe kiasi cha kuanza kuanzisha kasheshe hadi ndoa ikavunjika.
Tatu, badala ya mafanikio kufanikisha ndoa, yalifanikisha kitu kimoja tu ambacho ni kuivunja ndoa na kuacha majuto na mateso si kwake tu bali mume na watoto na hata ndugu na jamaa.
Japo si wengi wala wote wanaojitokeza kueleza ukweli huu wa aibu na uchungu, je hawapo? Je, ni kina mama wangapi wenye madaraka wamevunja ndoa zao?
Je, kwanini ni wanawake pekee ambao ni waathirika wa madaraka au kuna na wanaume? Jibu laweza kuwa sababu ni kwamba jamii yetu inatawaliwa na mfumo dume, ambapo wanaume wana uwezo wa kufanya watakalo na wasifanywe kitu na wenza wao wa kike.
Katika kudurusu kisa hiki, je nani wa kulaumiwa. Je, ni mfumo au mhusika mwenyewe? Je, hii inatoa somo gani kwa wale ambao hawajaingia na yakawakuta haya yaliyomkuta dada huyu ambaye wakati anaupata uheshimiwa alikuwa mdogo miaka 30 na ushei?
Je, hiki hakiwezi kuwa kikwazo kwa wanawake wengi ambao wangetaka kuingia siasa? Wahusika wachague kipi kati ya madaraka na ndoa? Wakati mkitafakari kujibu maswali hayo hapo juu, tunaweza kuwapa mwangaza au ujanja wa kufanya uamuzi bora.
Tutatoa angalizo kuwa madaraka ni ya muda na ndoa ni ya kudumu. Kwa mwenye akili safi na busara, atachagua cha kudumu na kuachana na cha muda.
Ni wangapi wanaweza kuchagua ndoa na kuachana na madaraka? Hivi hatuhitaji kubadili mfumo wetu wa kisiasa ili kulinda ndoa za waheshimiwa wetu na kuwahakikishia usalama kinamama ili wawe na mazingira salama na sawa kushiriki katika siasa?
Je, hili ni tatizo la watu binafsi au la jamii kwa ujumla pamoja na mfumo wake? Maswali ni mengi kuliko majibu.
Pamoja na kwamba makala haya inahusika na ndoa za waheshimiwa na madhara wapatayo, inawakilisha dhana nzima ya madaraka kijinsia. Kwanini wanaume wanapopata madaraka hayavunji ndoa zao? Kwanini madaraka ni tishio kwa ndoa za kinamama wengi japo si wote? Nini kifanyike?
Katika kudurusu kisa husika, wewe kama mwanandoa, unamsikitikia, kumlaumu, kumhukumu, au kutojali kwa vile hayakuhusu? Ungekuwa wewe, ungechagua nini na kwanini?
Tunauliza maswali kutaka kuwaelimisha wasomaji wetu kuwa madaraka si uheshimiwa tu bali ni dhana mtambuka. Kuna haja ya wanandoa kushirikiana katika jambo hata kama ni madaraka au mafanikio vinginevyo, yanaweza kugeuka maanguko si kwa mmoja, bali kwa wao wote, watoto wao, na hata wazazi, marafiki na familia zao.
Tumalizie kwa kuwataka wahusika na jamii kwa jumla kukomesha na kuepusha balaa hili kwa ndoa litokanalo na mfumo dume na fisadi.
Kwenye nchi za magharibi, waheshimiwa huchunguzwa sana na kupewa adhabu kali wanapopatikana kuvunja kanuni za maadili wanazopaswa kuzifuata.
Hata hivyo, wana mazingira mazuri ya kuwezesha waheshimiwa kulinda. Nasi, baada ya kugundua tatizo hili, kama jamii yenye akili timamu, tuchukue hatua kulikomesha ili kuepusha mateso kwa familia nyingi.