Mikataba miwili ya gesi asilia yasainiwa Tanzania

Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk Doto Biteko, akishuhudia uwekaji saini mkataba wa mauziano ya gesi asilia kati ya Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) na kampuni ya ARA Petroleum ya Oman na Ndovu Resources ya Uingereza, kushoto ni Mkurugenzi Mtendaji wa TPDC, Mussa Makame na kulia ni Mkurugenzi Mtendaji wa Ndovu Resources, Charles Santos.
Muktasari:
- Huenda kiu ya Watanzania wengi kutumia gesi asilia katika shughuli zao za kila siku ikakatika, baada ya kusainiwa kwa hati ya makubaliano ya kuanzisha mahusiano ya kujenga na kusambaza gesi asilia kwa teknolojia ya miundombinu midogo ya kubadilisha gesi asilia kuwa kimiminika (Mini-LNG).
Unguja/Dar. Habari njema kwa Watanzania baada ya Serikali kusaini hati ya makubaliano inayotengeneza matumaini ya kuanza kunufaika na gesi asilia popote ulipo.
Takribani miaka minane, mikoa ya kusini, Dar es Salaam na Pwani imekuwa ikinufaika na rasilimali hiyo, kwa huduma za umeme na kupikia kupitia mfumo wa uunganishaji wa bomba kutoka Mtwara hadi Dar es Salaam.
Hata hivyo, kwa mara ya kwanza katika mageuzi ya huduma hiyo, Serikali ya Tanzania kupitia Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) na Kampuni ya KS Energy, wameingia makubaliano hayo kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu midogo ya kubadilisha gesi asilia kuwa kimiminika (Mini-LNG).
Hati hiyo ya makubaliano imesainiwa sambamba na mkataba wa mauziano ya gesi asilia itakayozalishwa katika eneo la Ntorya Kitalu cha Ruvuma utakaofanywa kwa kampuni ya ARA Petroleum ya Oman na Ndovu Resources ya Uingereza
Akizungumza baada ya kushuhudia utiaji saini huo leo Jumatano, Januari 10, 2024 visiwani Zanzibar, Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk Doto Biteko amesema pamoja na uwepo wa bomba la gesi asilia nchini, ila njia rahisi ya kufanya iwafikie watu wengi ni kuigeuza kuwa kimiminika.
“Kufanya hivi tutaweza kuisafirisha kwa magari kwenda kwenye maeneo ambayo watu watatumia, hivyo kutiwa saini kwa makubaliano hayo kutawezesha gesi kuwafikia wananchi wengi zaidi,” amesema Dk Biteko
Amesema Serikali iko tayari kushirikiana na wawekezaji hao ili kuwafikishia wananchi nishati ya uhakika kutoka vyanzo mbalimbali, huku akitolea mfano utekelezaji wa mradi wa megawati 50 unaotokana na jua wilayani Kishapu, Mkoa wa Shinyanga na ujenzi wa miradi mingine ya uzalishaji, usafirishaji na usambazaji umeme.
“Lengo la nchi ni kuwa na nishati inayotokana na vyanzo mbalimbali ikiwemo jua, upepo, gesi na maji. Hii itafanya gesi asilia iliyopo itumike pia kwa kiasi kikubwa kwenye maeneo mengine kama viwanda na majumbani badala ya kutumika kwenye umeme na pia kupunguza matumizi ya mafuta,” amesema Dk Biteko
Amesema mkakati mkakati uliopo ni kupunguza kiwango cha gesi asilia kinachotumika katika kuzalisha umeme na badala yake itumike sehemu tofauti kama kwenye viwanda na majumbani.
Ili kufanikisha hilo amesema Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) wanao mkakati utakaowezesha kuwapo kwa mgawanyo wa matumizi ya gesi asilia ambapo kwenye umeme itakuwa asilimia 38, viwandani itakuwa asilimia 32 na asilimia 10 itabaki majumbani.
“Tofauti na ilivyo sasa ambapo matumizi ya gesi viwandani na majumbani ni asilimia 28 na asilimia iliyobaki kwa kiasi kikubwa inakwenda kwenye umeme,” amesema Dk Biteko.
Ametumia nafasi hiyo kuonya juu ya urasimu katika utekelezaji wa mipango iliyowekwa, huku akieleza kuwa uwepo wa mipango hiyo unalenga kuleta manufaa ya kizazi cha sasa na cha badaye.
Amesema Serikali inaangalia vitu muhimu ambavyo vitaondoa watu kwenye umaskini kwa haraka zaidi ikiwemo uwepo wa miundombinu ya barabara, anga, reli, bandari na nishati ya uhakika.
Mkurugenzi Mtendaji wa TPDC, Mussa Makame amesema mradi wa Mini-LNG ni wa kwanza kufanyika nchini.
“Mradi huu pia utapunguza kiu ya watanzania kutumia gesi asilia hata kwa maeneo yaliyo mbali na miundombinu ya mabomba, hivyo kuchochea matumizi ya nishati safi nchini,” amesema Makame.
Kuhusu mradi wa mauziano gesi, amesema utasaidia kuongeza kiwango cha gesi inayogunduliwa nchini kwa unategemea kuzalisha kati ya futi za ujazo milioni 60 hadi milioni 140 kwa siku katika kipindi cha miaka 3.
“Kukamilika kwa mkataba huu kutawezesha shughuli nyingine za uendelezaji kufanyika kama vile, ujenzi wa miundombinu ya kukusanya gesi kutoka visimani,” amesema Makame.
Amesema hilo litahusisha pia ujenzi wa miundombinu ya usafishaji wa awali ikiwemo kutoa maji na ujenzi wa bomba la kilometa 34 la kusafirisha gesi asilia hadi kiwanda cha kuichakata kilichopo Msimbati, Madimba mkoani Mtwara.
Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, Kanali Ahmed Abbas Ahmed amesema miradi hiyo ina umuhimu mkubwa ikiwemo katika mikoa ambayo rasilimali hiyo inazalishwa, huku akieleza kuwa watahakikisha wanaisimamia kwa ajili ya maendeleo ya Mtwara na nchi kwa ujumla.