Polisi walivyoimarisha ulinzi Msikiti wa Kichangani anakoswali Sheikh Walid
Muktasari:
- Katika hali isiyo ya kawaida, Msikiti wa Kichangani, Magomeni Jiji I Dar es Salaam, umezingirwa na Askari wa Jeshi la Polisi.
Dar es Salaam. Askari wa Jeshi la Polisi nchini, wakiwa nje ya Msikiti wa Kichangani uliopo Magomeni, ambao awali ilidaiwa aliyekuwa Sheikh wa Mkoa wa Dar es Salaam, Walid Omari Kawambwa, angekwenda kuswali Swala ya Ijumaa.
Katika mitandao ya kijamii kulisambazwa taarifa za waumini kujikusanya katika msikiti huo kwenda kufanya ibada na kumwona kiongozi huyo wa kidini aliyesimamishwa siku nne zilizopita.
Sheikh Kawambwa, alisimamishwa uongozi na Baraza la Ulamaa la Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (Bakwata), pamoja na masheikh wengine wawili wa Mkoa wa Singida na Kigoma, kwa tuhuma za ukiukaji wa maadili.
Tangu kusimamishwa kwa viongozi hao, katika mitandao ya kijamii kumekuwa na jumbe na machapisho mbalimbali ya waumini wa dini ya Kiislamu wakimtia moyo Sheikh Walid, huku wengine wakichapisha picha zake kuonyesha mapenzi yao kwake.
Machapisho hayo yalikwenda mbali zaidi, hadi baadhi ya waumini walipotaka kwenda kufanya ibada ya Ijumaa leo, Julai 17, 2026 katika msikiti huo ambao huwa kiongozi huyo ni Imamu na ndiko anakoswali.
Askari wa Jeshi la Polisi nchini, wakiwa nje ya Msikiti wa Kichangani uliopo Magomeni leo Ijumaa Julai 17, 2026.
Kwa mujibu wa baadhi ya machapisho katika mitandao hiyo, kwenda kwao katika msikiti huo, kulilenga kumwona Sheikh Walid, kadhalika kumtia moyo kwa hatua alizochukuliwa na viongozi wake wa Bakwata.
Ilivyokuwa misikitini
Tofauti na Ijumaa nyingine zisizo ndani ya Mwezi wa Ramadhan, Ibada ya leo ilikuwa na idadi kubwa ya waumini kiasi cha wengine kukosa nafasi ndani na wakaswali nje ya jengo.
Pia, kulikuwepo minong'ono kutoka kwa baadhi ya waumini wakisema wanasubiri kumwona Sheikh Walid kwenye mimbari akitoa neno lolote baada ya hatua zilizochukuliwa dhidi yake.
Hata hivyo, Swala ya Ijumaa ilianza saa 6:30 mchana na Sheikh Walid hakuwa miongoni mwa walioongoza Swala wala kuhutubia na hata msikitini hakuwepo kabisa.
Lakini, nje ya msikiti kulikuwa na gari tatu za askari polisi, huku wengine wakiwa wameuzunguka msikiti huo mikononi wakishika silaha za moto.
Kundi moja la askari lilikuwepo ilipo kona ya barabara inayotokea mjini kati, lingine ulipo mlango wa msikiti huo na lingine lilikuwa karibu na eneo la Magomeni Mikumi, kilipojengwa Kituo kipya cha Mabasi Yaendayo Haraka.
Askari wa Jeshi la Polisi nchini, wakiwa nje ya Msikiti wa Kichangani uliopo Magomeni leo Ijumaa Julai 17, 2026.
Mwisho wa Ibada hiyo iliyoisha saa 7:49 mchana, aliyesoma dua pamoja na maombi mengine alilitaja jina la Sheikh Walid akimwomba Mungu ampe busara, hekima na amlinde na mitihani inayomkabili.
Walichosema waumini
Akizungumza na Mwananchi, muumini katika msikiti huo, Hassan Khalid, amesema wingi huo wa waumini si kawaida, mara chache inajitokeza katika Ijumaa za Mwezi Ramadhan.
Amesema hata yeye alikwenda msikitini hapo pamoja na kuswali, pia alitaka kumwona na kumsikia Sheikh Walid, maana aliamini angepewa nafasi ya kuhutubia au kuzungumza na waumini.
"Sheikh Walid ni mtu wa watu, hana makuu, wala makundi. Ukimsikia unaona kabisa huyu ni mtu wa watu, ndio maana nimekuja kuswali hapa lakini hakuwepo," amesema.
Muumini mwingine, Zubeyda Maalim, amesema wanashangazwa na idadi ya polisi waliozingira msikiti huo, kwa kuwa si kawaida katika Ijumaa nyingine.
"Hawa wamekuja kwa ajili ya sheikh Walid walijua atakuja kuswali na ana wafuasi wengi sana hapa. Sisi tunampenda kwa sababu ya uongozi wake ni mtu mwema," amesema Zubeyda.
Licha ya ibada kumalizika, bado askari waliendelea kuwapo nje ya msikiti huo, huku baadhi ya waumini pia wakiwa wamejigawa katika vikundivikundi nje ya msikiti