Futi za ujazo bilioni 14.714 za gesi asilia zachakatwa Madimba

Meneja wa kiwanda cha gesi asilia Madimba mkoani Mtwara Leons Mrosso akielezea nishati hiyo inavyochakatwa, leo Juni 9,2023.
Muktasari:
- Wakati kiwango cha uchakataji wa gesi asilia katika kiwanda cha Madimba mkoani Mtwara kikiongezeka kutoka futi za ujazo milioni 20 mwaka 2015 hadi kufikia futi za ujazo milioni 110 kwa siku mwaka huu, kwa miaka nane kiwanda hicho kimechakata futi za ujazo bilioni 14.714 za gesi asilia.
Mtwara. Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) limesema, katika kipindi cha miaka nane iliyopita (2015-2023), kiwanda cha kuchakata gesi asilia cha Madimba mkoani Mtwara kimezalisha gesi zenye ujazo wa futi bilioni 14.714.
Pia kiwango cha uchakataji wa gesi hiyo kwa siku kimeongezeka kutoka futi za ujazo milioni 20 mwaka 2015 hadi kufikia futi za ujazo milioni 110 mwaka huu.
Na kwamba ongezeko hilo limetokana hitaji la nishati hiyo kuongezeka japo TPDC imebainisha kuwa kiwanda hicho kinauwezo wa kuchakata futi za ujazo milioni 210 za gesi kwa siku.
Hayo yameelezwa na leo Juni 9, 2023 na Meneja kiwanda cha kuchakata gesi asilia eneo la Madimba Mhandisi Leons Mrosso mbele ya waandishi wa habari kutoka Dar es Salaam waliotembelea visima vya gesi vya Mnazi bay na kiwanda hicho kujifunza namna gesi inavyozalishwa na kusafirishwa kwa matumizi mbalimbali.
"Kiwanda cha Madimba kinauwezo wa kuchakata futi za ujazo milioni 210 za gesi asilia, kiwanda cha Songosongo nacho kinauwezo wa kuchakata futi za ujazo milioni 140 ukijumuisha zote ni sawa na futi za ujazo milioni 350 zinachakatwa kwa siku na viwanda hivi viwili," amesema na kuongeza;
"Tuna bomba la gesi hapa Madimba ambalo linaelekea Dar es Salaam na maeneo mengine urefu wake ni km 551 na uwezo wa kusafirisha gesi yenye ujazo wa futi milioni 784 kwa siku."
Kwa upande wake Meneja Mawasiliano TPDC Marie Msellemu, amesema mpaka sasa zaidi ya asilimia 60 ya nishati ya gesi inavyozalishwa nchini inatumika kwenye gridi ya taifa kuzalisha umeme.
Mbali na umeme, amesema nishati hiyo pia tayari imewafikia wananchi 2,000 majumbani na magari zaidi ya 2,000 nayo yameunganishwa na mfumo wa gesi asilia.
"Wananchi waliounganishwa gesi ni pamoja na wakazi wa Mtwara ambao ndio walinzi wakubwa wa mradi huu, na katika kuhakikisha wananchi hawa wanaendelea kunufaika, tunatekeleza miradi mingi inayowagusa, kama vile kujengea vituo vya afya, shule, miradi ya maji pamoja na kutoa ajira hasa usafishaji eneo la Mkuza zoezi ambalo hufanywa na wazawa," amesema.
Amesema lengo la ziara hiyo, ni kuwajengea uwezo waandishi habari kufahamu namna gesi inavyochimbwa, kusafishwa hadi kwa mtumiaji wa mwisho hatua ambayo itawapa maarifa namna ya kuandika habari zinazohusu gesi asilia.
Tanzania inakadiriwa kuwa na mita trilioni 230 za ujazo za gesi asilia, ingawa zilizothibitishwa mpaka sasa ni futi trilioni 57.5, hivyo kuiweka kwenye ramani ya dunia ikishika nafasi ya 82.
Gesi hiyo tayari imeanza kuchimbwa katika visiwa vya Songosongo wilayani Kilwa, mkoani Pwani na eneo la Msimbati mkoani Mtwara, ikitumika kuzalisha umeme na kuendesha mitambo ya baadhi ya viwanda nchini.