Miili 11 yatambuliwa ajali ya Mbeya, majeruhi waendelea vizuri

Picha muonekano wa magari yaliyogongana katika mteremko wa Simike eneo la Mbembela jijini Mbeya na kusababisha vifo vya watu 16 na majeruhi 15. Picha na Saddam Sadick
Muktasari:
- Miili ya watu 11 imetambuliwa, tisa imechukuliwa na ndugu kwa ajili ya mazishi, mitano bado haijatambuliwa huku majeruhi wakionyesha matumaini ya kurejea katika hali zao.
Mbeya. Wakati miili 11 kati ya 16 ya watu waliofariki dunia kwenye ajali iliyohusisha magari matatu katika mteremko wa Simike jijini Mbeya ikitambuliwa, majeruhi wameeleza matumaini kutokana na huduma wanayopata.
Ajali hiyo ilitokea Juni 5, 2024 baada ya lori aina ya Scania ikufeli breki na kuligonga gari dogo, kisha kuligonga basi aina ya Toyota Coster lililokuwa na abiria. Pia ili ajali hiyo ilihusisha pikipiki, bajaji na guta.
Katika tukio hilo, watu 13 walifariki papo hapo na 18 walijeruhiwa, wanane walipelekwa katika chumba cha uangalizi maalumu (ICU), ambapo baadaye idadi ya vifo iliongezeka kufikia 16.
Akizungumza leo Ijumaa Juni 7, 2024 Muuguzi Mkuu wa Hospitali ya Rufaa Kanda ya Mbeya ambapo miili na majeruhi walipelekwa, Petro Seme amesema hadi saa tano asubuhi miili 11 ilikuwa imetambuliwa na tisa imechukuliwa na ndugu kwa maziko. Amesema miili mitano ilikuwa haijatambuliwa.
Muuguzi huyo amesema madaktari wanaendelea kupigania uhai wa majeruhi waliobaki ili warejee katika hali ya kawaida.
“Majeruhi wanaendelea vizuri wakiwamo waliokuwa kwenye uangalizi maalumu, timu yetu ya madaktari inaendelea kutoa huduma, majonzi ni mengi kwa ndugu waliopoteza wapendwa wao,”
Seme ameongeza kuwa hadi sasa wanaendelea kupokea wadau na viongozi mbalimbali wakiwamo wa kisiasa kuwajulia hali majeruhi na kutoa salamu za pole kwa waliopoteza ndugu zao.
Onesmo Richard, mmoja wa majeruhi amesema akiwa anatoka Tunduma kufundisha Kwaya, hakuelewa kilichotokea na badala yake alijikuta hospitalini, ingawa safari ilikuwa nzuri tangu mwanzo.
“Tulipofika milima ya Mbalizi, Iwambi tulipishana na magari mengi ila tulikuwa salama, nashukuru kwa sasa naendelea vizuri na huduma zinatolewa za uhakika. Walijua mguu umevunjika ila wamesema uko vizuri tunashukuru kwa huduma zao,” amesema Richard.
Naye Sophia Kamwela amesema walikuwa wakielekea Tukuyu msibani ndipo walipata ajali hiyo na kwamba hakujitambua kwa chochote zaidi ya kujikuta hospitalini.
“Nimechubuka mkono, mguu na maumivu ya kichwa, nilikuwa na mama yangu Martha Andulile ambaye sijajua kama atakuwa mzima au yuko wapi, tunashukuru huduma ni nzuri za madaktari,” amesema Sophia.