Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Haya hapa maeneo hatari kwa ajali Mbeya, Tanroad yataja mwarobaini

Magari yakiwa kwenye foleni katika Mlima Iwambi mkoani Mbeya kupisha magari madogo, ikiwa ni njia ya kupunguza ajali katika mlima huo, ambapo magari madogo na makubwa hupishana kwa dakika 30 yanapofika hapo. Picha na Sadamu Sadick

Muktasari:

  • Ajali za barabarani zinazotokea mara kwa mara mkoani Mbeya zimeendelea kugharimu maisha ya watu kutokana na maeneo korofi ambayo yakifanyiwa kazi huenda yakapunguza au kumaliza changamoto hiyo

Mbeya. Ajali za barabarani zinazotokea mara kwa mara mkoani Mbeya zimeendelea kugharimu maisha ya watu kutokana na maeneo korofi ambayo yakifanyiwa kazi huenda yakapunguza au kumaliza changamoto hiyo.

Katika siku za hivi karibuni, kumekuwapo na ajali kadhaa zilizotokea mkoani hapa na kusababisha vifo na majeruhi, ikiwamo iliyotokea jana Juni 5, 2024 kwenye mteremko wa Simike eneo la Mbembela na kusababisha vifo vya watu 13 papo hapo na wengine 18 kujeruhiwa.

Hata hivyo, vifo vilivyokana na ajali hiyo vimeongezeka leo Alhamisi Juni 6, 2024 na kufikia 16 baada ya majeruhi wengine watatu kufariki dunia.


Magari yakipita katika kona za Mlima  Nyoka mkoani Mbeya. Eneo hilo ni hatari kwa ajali kutokana na jiografia yake, na Serikali imeanza ujenzi wa njia nne kuanzia  ili kuzipunguza . Picha na Saddam Sadick

Ajali hiyo ilitokea baada ya lori kufeli breki na kugonga gari dogo aina ya Toyota Harrier kisha kuligonga basi la abiria aina ya Toyota Coaster lililokuwa likitokea Tunduma mkoani Songwe, kisha kugonga bajaji, pikipiki na baiskeli ya miguu mitatu maarufu ‘Guta.’

Hali hiyo inaelezwa inatokana na kuwepo maeneo matatu hatari ambayo ajali zimekuwa zikitokea zaida hasa zile zenye miteremko mikali.

Maeneo hatari kwa ajali

Mwananchi imefanya uchunguzi mdogo na kubaini maeneo hatari likiwamo la Mlima Iwambi ambako itakumbukwa mwaka 2023 ilishuhudiwa ajali iliyosababisha vifo vya watu 19 na wengine 23 kujeruhiwa, baada ya lori lililokuwa likipanda Mlima Iwambi kufeli breki na kurudi kinyumenyume kwa kasi na kugonga daladala lilotumbukia korongoni.

Kama hiyo haitoshi, Agosti 16, 2023 eneo la Shamwengo, watu 19 walifariki dunia na wengine 10 kujeruhiwa baada ya gari la Kampuni ya Evarest Fretch Ltd kuligonga basi la Super Rojas.

Pia eneo la Mlima Nyoka kunatajwa kuwa sehemu yenye hatari zaidi kutokana na jiografia yake ya kona nyingi kubwa sambamba na mteremko mkali uliopo, hali inayowashinda madereva wengi na kujikuta wakiangusha magari ambayo huua watu na kujeruhi pia.

Hata hivyo, maeneo hayo yanadaiwa kutokuwa na alama za tahadhari za barabarani hasa eneo la Iwambi, Simike na Shamwengo kama ilivyo kwa Mlima Nyoka.


Wananchi washauri

Wakizungumza na Mwananchi Digital leo Alhamisi Juni 6, 2024, baadhi ya wananchi jijini hapa akiwamo Victor James mkazi wa Maghorofani, amesema wenye mamlaka ya ujenzi wa barabara wameshindwa pia kuzingatia uwekaji wa alama za barabara ambazo nyingine zinachangia kutokea kwa ajali.

“Mfano, unakuta eneo lina mteremko, unakwenda kuweka taa za barabarani au matuta, sasa malori yakifeli breki na pale kwenye taa gari zikiwa zimesimama linayakumba kama ajali iliyotokea jana,” amesema James.

Hivyo, ameshauri Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroad) na Tarura (Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini), wazingatie jiografia ya mahali badala ya kuweka tu alama hizo kwa utashi wao.

Pia amesema ili kumaliza mzimu wa ajali hususan Mbeya mjini, Serikali inapaswa kukamilisha ujenzi wa barabara ya njia nne, huku akisisitiza mkandarasi aliyepewa zabuni hiyo aharakishe kumaliza kazi.

James amesema maeneo yote ambayo ajali kubwa zinatokea, changamoto ni ufinyu wa barabara na ndizo zinatumika na magari mengi ya ndani na nje ya nchi, yakiwamo malori makubwa ya mizigo.

"Barabara za Mbeya ni finyu, japo tunaona ujenzi wa njia nne unaendelea, labda unaweza kusaidia kumaliza au kupunguza, lakini kasi ya mkandarasi hairidhishi, hatujajua itaisha mwaka gani, ili wananchi turejeshe matumaini,” amesema James.

Hata hivyo, amezungumzia wingi wa matuta huku akitolea mfano maeneo ya Iwambi, barabara haina kingo za kutenganisha barabarani na makazi ya watu.

“Hapa gari likifeli kutoka kule juu, kwa kuwa barabara haina kingo, linapitiliza moja kwa moja kwenye nyumba za watu na ilishawahi kutokea hivyo halafu hakuna alama inayoonyesha huu ni mteremko mkali,” amesema James.

Naye Yusuph John, amesema licha ya mpango walioweka Polisi wa kuruhusu magari eneo la Mlima Iwambi, onyesha mafanikio chanya akidai kuwa muda waliotenga wa dakika 30 kuruhusu upande mmoja kabla ya wa pili, unaathari kwa malori na daladala ambazo ni nyingi.

Amesema baada ya magari kusimama kwa dakika hizo 30 yanaporuhusiwa, madereva huendesha kwa mwendo kasi tena bila kufuata utaratibu na kujikuta wakigongana na magari mengine yanayotoka upande mwingine.

"Dereva akitoka pale kwenye foleni hukimbiza kama mwizi, lakini kama gari zimeruhusiwa kutoka juu, hukutana na zile za zinazopanda mlimani, hivyo kero inabaki palepale,” amesema John.

Hata hivyo, ameshauri askari wa usalama barabarani wasimamie kikamilifu utaratibu huo usiendelee kuleta madhara na wawe wanajiridhisha kabla ya kuruhusu magari upande mwingine, ule uliosimamishwe, yawe yamesimama kweli.

“Kwa sababu huu ni mlima, wapo wanaopanda na kushuka, mara nyingi kama trafiki atayaruhusu magari yanayoshuka kabla ya kujiridhisha yale yanayopanda yamesimama kweli, ndiyo hali hii ya kugongana hutokea na hawa wanaoshuka mlima huwa wanakimbia sana,” amesema.

Naye Christina Mwankenja, amesema maeneo hatari zaidi kwa sasa ni Iwambi na Mlima Nyoka ambako ujenzi wa njia nne umeanza.

"Badala ya kuanzia sehemu tambarale, ujenzi wa njia nne ungeelekezwa sehemu muhimu waanze na Iwambi, Mlimanyoka na Inyala ambako kuna kona, miteremko na milima mikali,” amesema Christina.

Mwananchi pia imezungumza na Jordan Joram, dereva anayeendesha malori yanayokwenda nchi jirani ya Congo aliyesema kinachoigharimu Tanzania hasa kwa barabara ya Mbeya -Tunduma kuanzia eneo la Mlima Nyoka ni wembamba.

Amesema kama barabara hiyo ingepaanuliwa, huenda kusingekuwepo na ajali za mara kwa mara.

“Mfano hii ajali ya jana, barabara ingekuwa pana yule mwenye lori wala asingeyaparamia haya magari mengine, lakini alijitahidi sana kuyakwepa akashindwa matokeo yake amua,” amesema Joram.


Tanroad Mbeya

Akizungumzia ujenzi wa barabara, Meneja wa Tanroad Mkoa wa Mbeya, Masige Matari amesema ujenzi wa njia nne uko katika hatua nzuri na mkandarasi anaendelea na kazi.

"Kimsingi ujenzi unaendelea vizuri, ingawa kwa sasa siwezi kuongelea zaidi nipo safarini. Jumatatu ya wiki ijayo, nitatoa taarifa kamili hususan ujenzi wa barabara za pembezoni kwa ajili ya malori,” amesema Matari.

Hata hivyo, amesema kukamilika kwa ujenzi wa barabara hiyo kutapunguza kwa kiwango kikubwa ajali zinazoweza kuepukika kwa sababu barabara hiyo sasa itakuwa na maeneo ya vituo vya kupumzikia malori ya mizigo.

Kabla ya ajali ya jana, ajali iliyotokea eneo la Shamwengo Agosti 16, 2023, iliua watu 19 na kujeruhi 10 na ile iliyotokea eneo la Iwambi Septemba 22, 2023 iliyoua watu 9 na kujeruhi 23.