Ajali yaua 13, kujeruhi 18 Mbeya

Muonekano wa magari yaliyogongana katika mteremko wa Simike eneo la Mbembela jijini Mbeya leo Juni 5, 2024. Picha na Saddam Sadick

Muktasari:

  • Ajali imehusisha magari matatu, bajaji, pikipiki na guta, chanzo chatajwa dereva wa lori kushindwa kulimudu baada ya kufeli breki kwenye mteremko wa Simike.

Mbeya. “Nilisikia kitu kizito kikiniangukia.” Ni kauli ya mmoja wa majeruhi, James Mwasa mkazi wa Nzovwe, Jijini Mbeya akisumulia jinsi ajali hiyo ilivyotokea na kusababisha vifo vya watu 13 papo hapo na wengine 18 kujeruhiwa ikihusisha magari matatu, bajaji, pikipiki na guta jijini Mbeya.

 Ajali hiyo imetokea leo Jumatano Juni 5, 2024 katika mteremko wa Simike, eneo la Mbembela likihusisha lori linalodaiwa kufeli breki na kwenda kuyagonga magari mengine mawili kabla ya kuifikia pikipili, bajaji na guta.

Majeruhi wa ajali hiyo wamelazwa katika Hospitali ya Kanda, Mbeya kwa matibabu zaidi, huku wanane wakiwa wamewekwa kwenye chumba cha uangalizi maalumu (ICU).

Akizungumza na Mwananchi leo hospitalini hapo, Mwasa amesema akiwa anaendesha guta (baskeli ya miguu mitatu) huku amebeba mzigo, ghafla alidondokewa na kitu kizito kabla ya kupoteza fahamu.

Amesema baada ya hapo akujua kilichoendelea na alijikuta yuko hospitali akiwa na majeraha makubwa na maumivu makali mwilini.

“Nilisikia kitu kizito kikitua kichwani kikanikandamiza, lakini mbele niliiona gari ya abiria aina ya Toyota Coaster kama inarudi nyuma,” amesimulia Mwasa.

Hata hivyo, amesema anamshukuru Mungu kwa kuwa hai kwa sababu ajali iliyotokea ni mbaya na haifai kusimulia.

“Nawashukuru wasamaria wema waliotukimbilia na kutuwahisha hospitali, bila wao huenda na mimi ningefia palepale kama wengine,” anasimulia huku akitokwa na machozi.


Polisi wathibitisha

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, Benjamini Kuzaga ameiambia Mwananchi kuwa chanzo cha ajali hiyo ni dereva wa lori ambaye alishindwa kulimudu baada ya kufeli breki.

Amesema dereva wa gari hilo anashikiliwa na polisi kutokana na ajali hiyo.

“Gari hilo aina ya Scania lilikuwa likitokea Mbeya kuelekea Tunduma lilikosa uelekeo kutokana na kufeli breki na likaligonga gari dogo aina ya Toyota Harrier, kisha kuigonga Coaster ya abiria iliyokuwa ikitokea Tunduma kuelekea Mbeya mjini na kusababisha vifo 13 na majeruhi 18,” amesema kamanda huyo.

Amesema mpaka sasa bado hawajajua wapi walipo madereva wa pikipiki, bajaj na guta, kama ni miongoni mwa majeruhi au waliofariki dunia.

Amesema baadhi ya majeruhi hali zao si nzuri na Jeshi la Polisi litaendelea kutoa taarifa zaidi kadiri zitakvyowafikia kuhusiana na hali za majeruhi hao.

Akizungumzia eneo ilipotokea ajali, Kamanda Kuzaga amesema ni korofi na mara zote askari wa usalama barabarani hutoa tahadhari kwa madereva kuwa makini wanapolifikia eneo hilo pamoja na la Mlima Shamwengo.

“Zipo hatua tunachukua kwa madereva, ikiwamo kuwapatia elimu, lakini hapa ni eneo lenye mteremko mkali na kuna ujenzi wa barabara wa  njia nne unaendelea, ukikamilika huenda ajali kama hizi zinazokatisha uhai wa watu wengi kwa wakati mmoja zitapungua kwa kiwango kikubwa,” amesema kamanda huyo.

Kwa upande wake, Kamanda wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Mkoa wa Mbeya, Gervas Fungamali amesema wamefika eneo la tukio na kutekeleza wajibu wao wa kuokoa watu.

“Sisi jukumu letu ni kuokoa mali na maisha ya binadamu na ndilo jukumu tulilolifanya na tumefanikiwa japokuwa tukio ni kubwa kama mnavyoona, idadi ya waliokufa na kujeruhiwa tutafahamishana,” amesema Fungamali.


Mashuhuda

Mashuhuda wa ajali hiyo walikuwa na maoni tofauti, huku baadhi wakielezea ufinyu wa barabara na wengine wakilia na taa zilizopo eneo la Mafiati na matuta yaliyowekwa eneo la Mbembela kuwa huchangia kuwapo kwa ajali za mara kwa mara.

Mussa Dickson, amesema eneo hilo la mteremko wa Simike hutokea ajali za mara kwa mara kutokana na ufinyu wa barabara na mbele kuna matuta ambayo husababisha foleni kubwa ya magari.

“Kwa hiyo kama gari limefeli breki kama hivi, lazima litaparamia magari mengi kwa wakati mmoja, ni bora hayo matuta wakayaondoa” ameshauri Dickson.

Amesema licha ya dereva wa lori hilo kushindwa kulimudu gari hilo, alijitahidi kadri ya uwezo wake na kujikuta barabara ikimpa changamoto na kusababisha vifo na majeruhi hao.

“Tuliokoa majeruhi wengi, vifo hatukuhesabu, gari za wagonjwa zilibeba kama zilivyoweza, hili eneo ni korofi sana, barabara ni finyu hata namna ya dereva kukwepa wakati wa dharula ni ngumu” amesema Dickson.

Naye Charles Mbando, amesema aliona namna dereva alivyokuwa akihangaika kushika breki, lakini kwa kuwa mbele kulikuwa na taa imewaka ikiashiria asimame hakuweza na akayavaa magari yaliyokuwa mbele yake.

“Zile taa zinasumbua mno, dereva alijitahidi kukwepa lakini akafika eneo kukawa na matuta akaamua kubamiza upande wa ubavuni mwa Coaster, japokuwa alianzia gari dogo na baadaye kuzivaa bajaji, pikipiki na guta,” amesema shuhuda huyo.

Daktari bingwa wa magonjwa ya dharula katika Hospitali ya Rufaa Mbeya, Prosper Bashaka amesema wamepokea maiti 13 na majeruhi 18 na kati ya hao, wanne hali zao ni mbaya na wamelazwa katika chumba cha uangalizi maalumu (ICU).

“Kati ya wale waliofariki dunia, watano ni wanawake na mtoto mmoja. Watu saba ni wanaume na mpaka sasa tunaendelea na huduma kwa hawa majeruhi,” amesema Dk Bashaka.

Hata hivyo, kwa mujibu wa wakazi wa eneo hilo na mashuhuda, hiyo ndiyo ajali ya kwanza kubwa kutokea na kusababisha vifo vya watu wengi, licha ya kuwapo  kwa ajali nyingine ndogondogo ambazo hazina madhara makubwa kwa  wananchi.


Ajali zilizowahi kutokea

Ajali nyingine zilizowahi kutokea eneo hilo ni ile ya  Desemba 31, 2023 na kusababsha kifo cha mtu mmoja na majeruhi watano. Ajali hiyo ilihusisha lori baada ya kufeli breki, kisha kuyagonga magari mengine.

Nyingine ilitokea Desemba 7, 2012 ikihusisha lori na magari matatu ya abiria na kusababisha majeruhi.