Vifo ajali ya lori, Coaster Mbeya vyafikia 16

Picha muonekano wa magari yaliyogongana katika mteremko wa Simike eneo la Mbembela jijini Mbeya na kusababisha vifo vya watu 16 na majeruhi 15. Picha na Saddam Sadick

Muktasari:

  • Ajali hiyo ilitokea jana Juni 5, 2024 ambapo watu 13 walifariki dunia papo papo hapo, leo vifo vimefikia 16, huku miili minane ikitambuliwa na kusubiriwa ndugu kuwachukua.

Mbeya. Idadi ya vifo katika ajali iliyotokea jana Juni 5, 2024 imeongezeka na kufikia watu 16, huku miili minane ikitambuliwa na ndugu zao na majeruhi wengine wakiendelea na matibabu katika Hospitali ya Rufaa Kanda ya Mbeya.

Ajali hiyo iliyotokea katika mteremko wa Simike, eneo la Mbembela lilihusisha lori lililofeli breki na kugonga magari mawili, ikiwamo Coaster iliyokuwa na abiria ikitokea Tunduma mkoani Songwe.

Ilielezwa wakati lori hilo likiteremka mlima huo, lilifeli breki ambapo lililigonga gari dogo, kisha kugonga Coaster iliyokuwa imesimama eneo la Mbembela,  kisha bajaji, pikipiki na guta na kusababisha vifo na majeruhi.

Akizungumza na Mwananchi Digital leo Alhamisi Juni 6, 2024, Muuguzi Mkuu wa hospitali hiyo, Petro Seme amesema jana walipokea jumla ya watu 22, ambapo kati yao 14 walikuwa wamefariki na wengine majeruhi.

Amesema katika majeruhi hao, wawili walifariki wakati wakiendelea kupatiwa matibabu na kuongeza kuwa jopo la madaktari wanaendelea kutoa huduma kwa majeruhi wakiwamo watatu ambao walikuwa katika uangalizi maalumu.

"Hadi sasa asubuhi hii vifo vimefika 16, baada ya majeruhi wawili kufariki dunia wakati wakipata matibabu, madaktari wanaendelea kupambania wale majeruhi ili kuwa salama.

"Kati ya waliofariki dunia mtoto ni mmoja, wanaume wanane na wanawake watano, huku majeruhi wakiwa mmoja mtoto, mwanamume mmoja na wanawake watano." amesema Seme.

Muuguzi huyo ameongeza kuwa hadi sasa miili minane imetambuliwa na inasubiri ndugu zao kuja kuichukua kwa ajili ya taratibu za mazishi.

Hiio inakuwa ajali ya tatu kubwa kutokea mkoani Mbeya ndani ya miaka mitatu, ikiwamo iliyouwa watu tisa katika mlima Iwambi, baada ya lori kufeli breki na kugonga kwa nyuma Coaster na kutumbukia korongoni.

Katika ajali hiyo iliyotokea Septemba 22, 2023 mbali na kuua watu hao, kulikuwa na majeruhi 23.

Agosti 17, 2022 katika eneo la Shamwengo watu 19 walifariki dunia na wengine 10 kujeruhiwa, baada ya gari ya kampuni ya Evarest Fretch Ltd kuligonga basi la Super Rojas lililokuwa likitoka Mbeya kwenda mkoani Njombe.