Meli kubwa nne kujengwa Ziwa Tanganyika, wabunge wanena

Muktasari:
- Wabunge wametembelea Bandari ya Karema kunakojengwa meli kubwa nne za mizigo kujionea maendeleo ambapo wamezungumzia uwekezaji huo.
Katavi. Wananchi wa mikoa inayopitiwa na Ziwa Tanganyika Rukwa, Katavi na Kigoma watanufaika baada ya kukamilika kwa ujenzi wa meli kubwa nne za mizigo zinazojengwa katika Bandari ya Karema.
Meli hizo ambazo kila moja itakuwa na uwezo wa kubeba tani 60,000 kwa mwezi, ujenzi wake unatarajia kukamilika Julai, 2026 na tayari wananchi wa eneo la Bandari ya Karema, Katavi wameanza kuneemeka na fursa za ajira, kuongeza kipato cha kaya na Taifa.
Kutokana na hatua hiyo, Tanzania inaelezwa inaendelea kujijengea heshima na kuwa kitovu cha usafirishaji wa majini katika ukanda wa nchi za Afrika Mashariki.

Hayo yameelezwa jana Jumatatu, Mei 12, 2025 na Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) mbele ya wabunge wanaotoka mikoa ya Kigoma, Katavi na Rukwa kujionea maendeleo ya ujenzi wa meli hiyo, unaofanywa na kampuni kutoka China ambayo inachimba madini nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), eneo la Manono.
Mkurugenzi wa Mipango, Ubora na Vihatarishi wa TPA, Dk Boniphace Nobeji amesema bandari hiyo ya kimkakati inaunganisha Tanzania na nchi za ukanda wa maziwa makuu zikiwamo DRC, Zambia na Burundi.
Amesema bandari hiyo ni lango muhimu kwa biashara, usafirishaji wa shehena hivyo kichocheo cha maendeleo ya kijamii na kiuchumi katika kanda za magharibi.
Dk Nobeji amesema ni kutokana na hali hiyo Oktoba 11, 2023, TPA ilipokea maombi kutoka Kampuni ya Gold Voyage Logistics Limited, kampuni tanzu ya Zijin Mining Group Co. Ltd kutoka China ikiomba kukodishwa eneo la mita za mraba 62,000 katika Bandari ya Karema kwa kipindi cha miaka miwili, kuanzia Februari 2024 hadi Januari 2026.

Lengo la kampuni hiyo amesema ni kulitumia kujenga meli nne zitakazohudumia katika Ziwa Tanganyika, ujenzi wa miundombinu ya kusaidia mradi kama vile ghala, karakana ya maegesho, ofisi na kambi.
"Desemba 12, 2024 TPA iliingia mkataba na kampuni hiyo yenye makao makuu China," amesema Dk Nobeji kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu wa TPA, Plasduce Mbossa.
Amesema katika kipindi cha miaka miwili ya mkataba ya upangishaji, TPA inatarajia kupata kodi ya upangishaji Dola milioni 1.05 sawa na Sh2.8 bilioni: "Lakini zaidi fursa za ajira kwa wananchi wa maeneo haya na Watanzania kwa ujumla, kuchochea uchumi wa maeneo haya na vifaa vya ujenzi vinapita bandarini kwetu bado ni fursa zaidi."
Amebainisha faida za uwekezaji huo unatarajia kuwa na kichocheo cha usafirishaji wa madini ya lithium, shaba na dhahabu kutoka eneo la Manono nchini DRC yanayochimbwa na kampuni hiyo ambapo kupitia Manono, Bandari ya Kalemie hadi Bandari ya Kigoma, Dar es Salaam na Tanga.
"Upande wa Tanzania usafirishaji wa shehena hiyo kutoka Bandari ya Kigoma unategemea kutumia miundombinu ya reli zilizopo za MGR na SGR hadi Bandari ya Dar es Salaam na Tanga.
Kwa kuwa Kalemie itakuwa lango la shehena kutoka Manono na sisi kama nchi itanufaika na ongezeko la shehena kupitia bandari ya Kigoma na Karema kwenda bandari za baharini kama Dar es Salaam na Tanga," amesema Dk Nobeji.
Amesema hali hiyo: "Itaongeza mapato ya Serikali, nafasi za ajira na kuimarisha nafasi ya Tanzania kama njia ya kipaumbele kwa biashara ya kimataifa kutoka na kuingia Afrika Mashariki."
Dk Nobeji amesema mradi huo wa kimkakati unachangia katika kufikiwa kwa lengo la Tanzania la kuwa kitovu cha biashara ya kikanda na unafungua fursa za kimataifa kupitia usafiri wa majini.
Walichokisema wabunge
Mbunge wa Nkasi Kaskazini (Chadema), Aida Kenan alisema: "Tunapongeza kwa hatua nzuri ya mazingira kuwa mazuri nchini kwani yamewezesha watu hawa kuja hapa kwetu."
Kenan alitoa ushauri kwa Serikali kuangalia zile kazi ambazo zinaweza kufanywa na wazawa wapewe wazawa: "Lakini sheria ya ajira kazini itazamwe kama inazingatiwa ili kila mmoja anufaike na mradi huu."

Wakati Aida akieleza hayo, Mbunge wa Viti Maalum, Bupe Wakang'ata alisema:"Nipongeze Serikali, meli imefikia hatua nzuri sana, kupitia uwezekaji huu tutapata fursa na nchi itavuna mengi."
Mbunge wa Kigoma Mjini (CCM), Kilumbe Ng'enda amesema jitihada mbalimbali za Serikali kuboresha miundombinu ya bandari, barabara, reli na amani inachochea maendeleo ya wananchi na Taifa.
"Mizigo yake kutoka DRC na kuipitisha kwenye bandari zetu na kuzipeleka huko duniani huu ndio wito wetu siku zote kuwa Serikali ishirikiane na sekta binafsi kwani yenyewe pekee haiwezi. Meli zitatumika kwa kazi zao lakini fursa kubwa ni kwetu," amesema Kilumbe.
Aidha, ameiomba Serikali kuhakikisha inaongeza kasi ya ukarabati wa Meli ya Liemba na mwongozo na ujenzi wa kiwanda cha meli Kigoma ili ziwe zinakwenda kujengwa au kukarabatiwa Kigoma ambapo itafungua zaidi fursa mbalimbali.
Mbunge wa Nkasi Kusini (CCM), Vicent Mbongo amesema, “kukamilika kwa meli hizo na maboresho ya bandari mwambao wa Ziwa Tanganyika kutasaidia pia wakulima kwani zitafungua fursa kwa wawekezaji kwani uchumi wa Rukwa unategemea bandari, hivyo tuipongeze sana Serikali kwa hatua hii kubwa."
Kamati za Bunge
Mwakilishi wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Mitaji ya Umma (PIC), Nicholaus Ngassa amesema wameshuhudia uwekezaji mkubwa umefanyika na kazi yao ni kuangalia tija inayopatikana. “Unapokuwa na bandari unaona fursa kubwa kwa jamii na Taifa kwa ujumla.
"Wito wangu kwa wananchi, wawe walinzi wa mali hizi ili kuongeza matumaini kwani kuna nchi nne DRC, Zambia au Burundi lakini wamechagua kuja hapa kwa sababu ya usalama na kufikika. Jambo hili linampa matumaini mwekezaji na ndio maana mnaona makaa ya mawe hapa, kuna wawekezaji, " amesema Ngassa ambaye pia ni Mbunge wa Igunga (CCM).
Naye Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu, Selemani Kakoso amesema uwekezaji huo unapaswa kuendana na vijana wanaofanya kazi eneo hilo ikiwemo maboresho ya sheria za ajira mahali pa kazi.
Kakoso ambaye pia ni Mbunge wa Mpanda Vijijini amesema kwenye bandari ya Karema licha ya meli hizo nne zitafanya kazi ziwa Tanganyika katika nchi za DRC, Zambia na Burundi lakini Tanzania ni wanufaika wakubwa na tayari wameanza kunufaika kutokana na ujenzi kufanyikia eneo lao.
"Tumewaona wawekezaji, kazi iliyo mbele kwa Serikali ni kuhakikisha barabara ya kwenda bandarini hapo zaidi ya kilomita 100 inajengwa kwa lami haraka, tumeona makandarasi wanaendelea, tuwasimamie ili wamalize kwa wakati," amesema Kakoso huku akishangiliwa na wananchi wa jimboni kwake.
Maelezo ya Serikali
Katika ziara hiyo, Naibu Waziri wa Uchukuzi, David Kihenzile alimwakilisha Waziri wake, Profesa Makame Mbarawa ambapo amesema meli hizo nne zitakuwa zikifanya safari Ziwa Tanganyika ambalo lipo DRC, Zambia na Burundi lakini Tanzania inanufaika kwa kuwa na bahari.
"Sisi ndio tumeunganishwa na bahari, unaweza kuona tupo kwenye eneo la mkakati. Hii kampuni inayojenga hizi meli inachimba madini mbalimbali DRC na hii kwetu ni fursa kwani watayapitisha kwenda," amesema Kihenzile.
Amesema kazi kubwa ambayo Serikali inaifanya kwa ni kuhakikisha inaboresha bandari zake, miundombinu ya reli ya kati na ile ya kisasa (SGR) na jengo la abiria kwenye Uwanja wa Ndege Kigoma ili sekta ya usafirishaji iwe bora na isiwe kikwazo kwa wananchi na wawekezaji.

Amesema reli ya kati kutoka Tabora - Mpanda hadi Karema ikikamilika itarahisisha usafirishaji wa mizigo kutoka bandarini hapo hadi Dar es Salaam na malengo ya Serikali SGR itasambaa nchini na hiyo ndiyo dhamira ya Serikali inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan.
Pia ametumia fursa hiyo kutoa maelekezo kuwa kila anayehusika kusimamia ujenzi wa meli hizo wanatekeleza wajibu wao ipasavyo ikiwemo Mamlaka ya Usimamizi wa Usafiri Majini (Tasac), “Nawaelekeza wasimamie ubora ili kuimarisha usalama na usafiri wa majini."