Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Mbarawa: Serikali kutengeneza meli mpya mbili za mizigo

Waziri wa Uchukuzi, Profesa Makame Mbarawa akiwa na watendaji wa TPA wakikagua miundombinu ya bandari ya Karema wilayani Tanganyika mkoani Katavi.

Muktasari:

  • Katika kurahisisha shughuli za usafirishaji wa mizigo katika maziwa ya Tanganyika na Victoria, Serikali inakusudia kutengeneza meli mbili za mizigo zitakazotoa huduma katika maziwa hayo.

Dar es Salaam. Waziri wa Uchukuzi, Profesa Makame Mbarawa amesema Serikali inakusudia kutengeneza meli mpya ya mizigo itakayotoa huduma ziwa Tanganyika.

Hatua hiyo inachagizwa na kukamilika kwa ufanisi kwa ujenzi wa bandari ya Karema iliyopo wilayani Tanganyika iliyojengwa kwa Sh47.9 bilioni ambayo itarahisisha shughuli za usafirishaji wa mizigo kati ya mataifa ya Tanzania, Congo (DRC) na Zambia.

Waziri Mbarawa ameeleza hayo Jumapili Oktoba 8, 2023 wakati akikagua miundombinu ya bandari ya Karema iliyopo mkoani Katavi. Amesema Serikali pia itajenga barabara ya kiwango lami na reli ili kuwezesha bandari kutoa huduma zake kwa ufanisi zitakazochochea shughuli za kiuchumi.

“Nimefurahi kuona bandari hii nzuri sana, yenye miundombinu ya kisasa na nafasi ya kutoa huduma bora za kibandari kwa wananchi na wafanyabiashara wa nchi za Tanzania, Zambia na Congo DRC,” amesema Profesa Mbarawa.

Waziri Mbarawa amesema ili uwekezaji wa Serikali wa Sh47.9 bilioni katika bandari hiyo uwe na tija lazima ipatikane meli kubwa ya mizigo sambamba na ujenzi wa barabara ya lami na reli kilomita 110 kutoka Mpanda hadi Karema.

Jumatano Oktoba 11, 2023 Wizara ya Uchukuzi, itasaini mikataba ya ujenzi wa meli mbili za mizigo zitakazotoa huduma katika maziwa Victoria na Tanganyika. Pia itasaini mkataba wa ujenzi wa karakana ya meli, shughuli itakayofanyika mkoani Kigoma.

Mbunge wa Mpanda Vijijini Moshi Kakoso amesema wananchi wa mikoa ya Katavi, Rukwa na Kigoma wanamshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa mradi mkubwa wa bandari ya kimkakati ya Karema.

Kakoso ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Miundombinu, alisema uwepo wa bandari ya Karema utainua uchumi wa mikoa hiyo na kutoa fursa za ajira kwa wananchi

Meneja wa Bandari za Ziwa Tanganyika, Edward Mabula amesema, tangu kuanza kutumika kwa bandari ya Karema, Septemba Mosi mwaka 2022 jumla ya abiria 4, 900 na tani 1,500 za mizigo zimehudumiwa.