Prime
Watu hawa hatarini kuugua bawasiri

Muktasari:
- Kutumia nguvu nyingi unapoenda haja kubwa, na kutokula vyakula vyenye nyuzinyuzi, ni miongoni mwa visababishi vya hali hii.
Dar es Salaam. Iwapo unatumia simu yako unapoenda haja kubwa, huenda ukawa kwenye hatari ya kuathiriwa na kuvimba kwa mishipa ya damu iliyopo ndani au katika eneo linalozunguka njia ya haja kubwa.
Ugonjwa huu unafahamika kwa kimombo kama hemorrhoids au bawasiri/hemoroidi kwa Kiswahili.
Dk Mark Siboe, daktari wa upasuaji, anasema kuwa kutumia nguvu nyingi unapoenda haja kubwa, na kutokula vyakula vyenye nyuzinyuzi, ni miongoni mwa visababishi vya hali hii.
Isitoshe, kuketi kwa muda mrefu, kama wanavyofanya madereva wa malori na wafanyakazi ofisini angalau kwa zaidi ya saa sita kwa siku, huongeza shinikizo kwenye sehemu ya haja kubwa.
“Kazi za kubeba mizigo mizito, kuwa na uzito kupindukia, mazoezi yenye kutumia nguvu nyingi ya mara kwa mara pia yanachangia ugonjwa huu,” anasema Dk Siboe.
Anasema kwa wanaopenda kufanya mazoezi ya kuinua vitu vizito, anashauri kutoa pumzi wakati unainua zaidi ya kilo 25 na kuepuka kuinua uzito mkubwa kama unatatizika mara kwa mara.
Ugonjwa huu huathiri kina nani zaidi?
“Ugonjwa huu huathiri hadi asilimia 40 ya watu wazima, hasa walio na umri wa zaidi ya miaka 50. Lakini aibu na wasiwasi wa kijamii huwakwamisha wengi hasa wanaume kutafuta matibabu,” anaeleza.
Dk Siboe, anasema kuwa hii ni kwa sababu, kadri miaka inavyosonga, hasa kati ya umri wa miaka 40 hadi 60, uzee au jenetiki huleta udhaifu kwenye tishu za mwili.
“Kudhoofika kwa tishu za kolajeni na elastini kutokana na sababu ya umri au jeni, ni kama sofa yako uipendayo inavyoanza kulegea, tishu zako huwa dhaifu vivyo hivyo,” anafafanua.
Dalili za ugonjwa huu ni pamoja na kutokwa na damu wakati wa haja, kuwashwa karibu na sehemu ya haja, uvimbe kwenye tupu ya nyuma, na maumivu hasa katika sehemu zilizofura na kujaa damu.
Kuhusu matibabu yake, anasema: “Krimu za dukani au tiba za nyumbani husaidia kutuliza maumivu tu kwa muda mfupi. Hata hivyo, iwapo dalili za mgonjwa zinazidi baada ya wiki moja, ni bora kufika hospitalini kwa ukaguzi.’’
Isitoshe, hufai kutumia krimu hizi kwa zaidi ya siku saba lakini unaweza kukalia maji ya vuguvugu mara mbili hadi tatu kwa siku kwa dakika 10.
Zaidi ya hayo Dk Siboe anaonya dhidi ya kutumia tiba zisizothibitishwa mshubiri, tangawizi au kitunguu saumu kilichosagwa.
Kando na krimu na tiba za kinyumbani, Dk Siboe anasema kuwa matibabu mengine ambayo mgonjwa hupokea, hulingana na uvimbe kwenye tupu yake ya nyuma.
“Kuna wagonjwa ambao tunashauri kunywa angalau lita 1.5 hadi 2 za maji kila siku, waongezee ulaji wa vyakula vyenye nyuzinyuzi, tunawapa dawa za kulainisha haja yao kubwa na kuwashauri kukalia maji ya vuguvugu.”
Kwa walioathiriwa sana au wanaopata ugonjwa huu mara kwa mara, Dk Siboe anaeleza kuwa hufanyiwa upasuaji.
Kuzuia uvimbe
Ili kuzuia uvimbe huu kwenye tupu ya nyuma, Dk Siboe anashauri kula vyakula vyenye nyuzinyuzi kama sukuma wiki, spinachi, brokoli, maharagwe, dengu, na matunda kama machungwa na mananasi.
Pili, unapaswa kusimama kila baada ya dakika 30-45 na kutembeatembea kidogo.
“Kunywa maji mengi badala ya soda, chai au kahawa,” anasema na kuongeza kuwa mgonjwa asikae msalani kwa zaidi ya dakika tano.
Pia, Dk Siboe anashauri kuwa na mazoea ya kuenda haja kubwa wakati unahisi haja na usitumie nguvu nyingi unapokuwa msalani.
“Zoea kufanya mazoezi kila mara lakini usivute pumzi unapoinua chuma na uhakikishe kuwa uzito wako upo wa wastani,” anaeleza.
Je, ugonjwa huu huathiri tendo la ndoa?
Ingawa ugonjwa huu hauathiri moja kwa moja uwezo wa kushiriki ngono, usumbufu na aibu vinaweza kuathiri maisha ya karibu ya kimapenzi.
“Maumivu wakati wa shughuli fulani huweza kusababisha kuepuka tendo la ndoa, na hivyo kuathiri uhusiano,” anasema Dk Siboe na kuongeza kuwa hali hii pia huchangia upweke kati ya wapenzi au wanandoa.
Visababishi vingine vya ugonjwa
Rejea mbalimbali zinataja yafuatayo kama visababishi vya ugonjwa wa bawasiri kama vile kuwa na uzito wa mwili kupita kiasi, ujauzito, na kula vyakula visivyo na nyuzinyuzi za kutosha, kubeba vitu vizito mara kwa mara.
Pia kuhara kwa muda mrefu na kutopata choo, kujamiiana kinyume na maumbile, historia ya uwepo wa ugonjwa wa bawasiri katika familia na uzee.
Makala haya kwa hisani ya mtandao wa Taifa Leo