Mchengerwa awaonya ma-DED wanaosubiri bajeti kutengeneza madawati

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Mohamed Mchengerwa
Muktasari:
- Serikali imesema itawachukulia hatua wakurugenzi wa halmashauri wanaosubiri bajeti ya Serikali kuu kuchonga madawati.
Dar es Salaam. Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Mohamed Mchengerwa amesema hatamvumilia mkurugenzi wa halmashauri atakayesubiri bajeti kutoka Serikali Kuu kwa ajili ya kutengeneza madawati katika shule zinazojengwa.
Amesema yeyote atakayefanya hivyo, atalazimika kusubiri bajeti hiyo akiwa nje ya mfumo wa Serikali, huku akiwasisitiza kutumia makusanyo ya ndani ya halmashauri kutekeleza hilo.
Katika hatua nyingine, ameielekeza Tume ya Utumishi wa Walimu (TSC), kupitia upya muongozo wa walimu, kisha iishauri Serikali namna bora ya kulinda hadhi ya wanataaluma hiyo.
Mchengerwa amesema hayo leo, Novemba 27, 2023 alipohutubia hafla ya kukabidhi vifaa mbalimbali zikiwemo kompyuta mpakato, pikipiki na gari aina ya Coaster kwa TSC kwa ajili ya shughuli za kila siku.
Amesema Serikali haitakubali kumuona mkurugenzi wa halmashauri yoyote atakayesingizia bajeti ya Serikali kuu kuchonga madawati kwa ajili ya shule za eneo lake.
Ili kutekeleza hilo, ametaka mipango ya maendeleo ya kila halmashauri iweke kipaumbele mahitaji yanayowasaidia wananchi.
"Wakurugenzi wa halmashauri (ma-DED), mpango wa maendeleo uendane na mahitaji ya wananchi katika eneo husika, maana yake mahitaji ya kwanza yawe yale yanayokwenda kusaidia Watanzania katika maeneo husika," amesema.
Amesema zipo halmashauri zinazojiwekea mpango wa matumizi makubwa ambayo si ya msingi kwa wananchi wa eneo husika.
"Yapo maeneo ambayo wananchi wanahitaji madawati 50, mkurugenzi anasema anasubiri bajeti ya Serikali Kuu kupeleka madawati 50 au 100 na eneo hilo lina mkurugenzi, mkuu wa wilaya, hili halikubaliki," amesema.
Amesema wanaosubiri bajeti ya Serikali kuu kupeleka vipaumbele vya maendeleo ya wananchi watasubiri wakiwa nje ya mfumo.
"Haiwezekani tujiwekee mpango wa matumizi makubwa ya fedha ambayo hayana faida kwa wananchi na mkuu wa wilaya na mkuu wa mkoa yupo," amesema.
Katika hatua nyingine, Mchengerwa ameitaka TSC ifanye tathmini ya muongozo wa walimu, kisha iishauri Serikali namna nzuri ya kuhakikisha wanataaluma wanapata stahiki zao.
"Mkajipange kuhakikisha mnafanya tathmini, ili kuishauri Serikali juu ya walimu wanaokwenda kusoma mishahara yao iendane na ngazi za elimu yao.
"Lakini mkakae kuishauri Serikali namna bora ya kulinda maslahi ya walimu," amesema.
Kwa kuwa Serikali imejenga zaidi shule na miundombinu ya elimu, amesema kwa sasa inatarajia kuelekeza katika ujenzi wa nyumba za walimu.
Katika hotuba yake hiyo, amewataka wakurugenzi wa halmashauri zote nchini kuhakikisha shule zinazojengwa katika maeneo yao zinakamilika ndani ya muda zikiwemo zile za Novemba 30 na Desemba 30, mwaka huu.
Akizungumzia vifaa hivyo, Katibu Mtendaji wa TSC, Paulina Nkwama amesema vifaa vilivyokabidhiwa ni Coaster moja lenye thamani ya Sh258 milioni.
Vingine ni pikipiki 62 kwa ajili ya watumishi wa TSC ngazi za wilaya na kompyuta mpakato 159 kwa ajili ya ofisi za tume hiyo.