Mchengerwa: Waliochoma Kariakoo mnadani, wakamatwe

Muktasari:
- Moto katika eneo hilo la Manadani ulizuka Oktoba mosi, 2023 na kuteketeza bidhaa zilizokuwa kwenye vibanda na maduka yaliyo na jirani na eneo hilo.
Dar es Salaam. Waziri Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Mohammed Mchengerwa, ameagiza kukamatwa na kufikishwa mahakamani watu waliobainika kuhusika na tukio la kuchoma moto vibanda eneo la Kariakoo Mnadani.
Mchengerwa ametaoa maagizo hayo leo Jumatano Novemba 15, 2023 alipotembelea soko la Kariakoo kuona ujenzi wake unavyoendelea.
Moto katika eneo hilo la Mnadani ulizuka Oktoba Mosi, 2023 na kuteketeza bidhaa zilizokuwa katika vibanda vya wafanyabiashara na maduka yaliyokuwa jirani na eneo hilo.
Kutokana na tukio hilo, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Albert Chalamila, aliunda kamati kuchunguza tukio hilo ambayo majibu yake aliyatoa Oktoba 21 na kueleza kuwa ilikuwa ni hujuma.
Kwa mujibu wa Chalamila, Kamati hiyo iliyokuwa inaundwa na watu saba, ilibaini kuwa ni hujuma miongoni mwa wafanyabiashara waliokuwa na mgogoro kati yao na uongozi uliopo, ndiyo kiini cha tukio la uchomaji moto eneo hilo.
Katika ziara yake hiyo, Mchengerwa alipongeza hatua zilizochukuliwa na Chalamila lakini akasema hajasikia maelekezo ya nini wamefanyiwa waliobainika kuhusika na tukio hilo huku akidai kuwa wanajulikana.
“Nichukuae fursa hii kumpongeza Mkuu wa Mkoa kwa hatua ambazo amekuwa akizichukua kutokana na madhara ya moto ambayo yamekuwa yakitokea, ikiwemo kuunda kamati ya uchunguzi na kuja kutoa taarifa ya uchunguzi iliyoufanya.
“Niseme kwamba Mkuu wa Mkoa wakati huo wewe unafanya uchunguzi na mimi nilituma watu wangu kufanya uchunguzi, kwa hiyo ile ripoti niliyonayo nitakuletea uingunishe na ripoti uliyo nayo wewe,” amesema Mchengerwa.
Aidha alisema kuwa makossa ya uchomaji majengo ni makosa makubwa kwani inaweza kupelekea aliyefanya kosa hilo kufungwa miaka 30 au kifungo cha maisha jela.
“Kwa hiyo maelekezo yangu, wale waliohusika wote wakamatwe kwa sababu wanafahamika waliopelekea moto huu kuzuka na kusababisha hasara, kusababisha maumivu makubwa kwa Watanzania ambao walikuwa wanafanya shughuli zao eneo lile,” amesema Waziri Mchengerwa.
Kwa upande wake Chalamila, amesema amepokea maelekezo yote na kuahidi baada ya muda atampa Waziri huyo taarifa ya namna watakavyoshughulika na watu hao.
Aleza kuridhika ujenzi soko la Karikaoo
Akizungumzia kuhusu ujenzi wa soko la Kariakoo, Waziri huyo amesema ameridhika na hali ya ujenzi ilipofikia na kuwapongeza wasimamizi wake.
“Leo nimefanya ukaguzi na nimeridhika ujenzi unakwenda vizuri kabisa, na takribani asilimia 85 imeshatekelezwa na tunaamini mkandarasi kufika Februari mwakani atakuwa amemaliza na tungependa Rais Samia Suluhu Hassan aje mwenyewe kuja kuwakabidhi wana Dar es Salaam soko hili,” amesema Mchengerwa.
Amesema ujenzi wa soko hilo umeongeza maduka mengi kuliko yaliyokuwa awali huku akimtaka mkandarasai kuhakikisha viwango vilivyokusudiwa katika ujenzi huo vinaendelea hadi umaliziwaji wake.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Shirika la Masoko ya Kariakoo, Hawa Ghasia, amesema kukamilika kwa soko hilo, wafanyabaishara wengi wataingia na watakaa katika maeneo ya kisasa na bora zaidi kuliko ilivyokuwa hapo awaliambapo kulikuwa na waliopanga bidhaa chini.
“Pia katika ujenzi wa soko hili, zile changamoto zimeshughulikiwa ikiwemo mifumo ya kuzuia moto, mifumo ya maji taka na mifumo ya kisasa ya umeme yote imezingatiwa,” amesma Ghasia na kuongeza;
“Hivyo tunategemea wafanyabiashara wale watakoarudi na wengine wapya wakija hapa wabadilike na wasipobadilika soko lenyewe litawabadisha.”
Akizungumzia mipango waliyonayo baada ya soko hilo kukamilika, Chalamila amesema moja ya masharti makubwa kwa watakaoingia katika soko hilo ni kuwa na mikataba huku kodi iliyokuwepo awali itajadiliwa upya ili kuendana na thamani ya Soko la Kariakoo.
Pia amesisitiza kuwa mara baada ya kuanza kazi, soko hilo litafanya kazi saa 24 na tayari ukarabati wa mifumo ya umeme imeshaanza kushughulikiwa pamoja na kukutana na wadau kuona namna watakavyojipanga katika suala zima la ulinzi na usalama kwenye eneo hilo.